Dodoma. Umewahi kusikia maneno; ualimu ni wito? Ni msemo wa miaka mingi japo mabadiliko ya kimaisha yamewavaa baadhi ya watu wanaomini msemo huo hauna maana tena katika dunia ya sasa. Kwao ualimu ni ajira, mengine yatafuata.
Hata hivyo, kwa baadhi ya walimu akiwamo Zainab Yamlinga, hadithi ni tofauti. Pengine kwake ualimu ni zaidi ya wito. Fuatilia simulizi yake…
Ni chumba kilichopambwa kwa vyungu vya kupikia, picha za marais wa Tanzania, wanyama, vyakula, fedha, herufi na namba mbalimbali.
Katikati ya chumba hicho kumefungwa kamba inayoning’iniza picha mbalimbali ambazo zinatumika kama zana za kufundishia watoto.
Chumba hicho ndilo darasa wanalotumia wanafunzi wa elimu ya awali katika Shule ya Msingi Medeli iliyopo jijini Dodoma
Ni darasa la kuwanoa watoto wenye miaka mitano, ikiwa ni maandalizi ya kwenda kuanza darasa la kwanza.
Hayo niliyoyaeleza awali ni tisa, kumi ni ubunifu ndani ya darasa ambapo kuna kona zilizotengwa maalum kwa ajili ya masomo ya sanaa na michezo, sayansi, hesabu na tehama, kusoma, lugha na mwasiliano.
Ubunifu huo umefanywa na mwalimu wa darasa hilo, Zainabu Yamlinga ambaye pia amebuni mbinu ya kuwafanya watoto kuelewa kwa urahisi maelekezo ya taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa saa tatu na nusu wanazokuwa shuleni hapo.
Utaratibu huo si mwingine bali kutumia nyimbo ambazo watoto huimba na kisha kwenda kufanya jambo linalotakiwa kufanyika kwa wakati huo.
Kwa mfano, akitaka waende kwenye kona zao, anaimba wimbo na hivyo watoto huelekea huko wanapotakiwa kwenda.
“Tunatumia nyimbo kuondoa kelele na kuwafanya wote wa concentrate (waelekeze mawazo yao) kwenye jambo wanalokwenda kulifanya kwa wakati huo,”anasema Mwalimu Zainabu.
Anaushukuru uongozi wa Shule ya Msingi Medeli na wazazi wa watoto hao, kwa kusaidia katika kuhakikisha darasa hilo linachangamka na kuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia.
“Si vifaa vyote vinavyotumika kutengenezea tumenunua, vingine ni vya kuokota. Ninapokuwa katika mazingira ya nyumbani ama mengine nikiona kifaa chochote cha maboksi naokota naleta hapa, visoda naokota naleta hapa,” anasema mwalimu huyo anayeonyesha kila dalili ya kuiupenda kazi yake na wanafunzi wake.
Zainabu anasema watoto wakishaenda nyumbani yeye hubaki kuangalia kama kuna picha zimebanduka ama kuziondoa picha zilizokaa kwa muda mrefu ili kuwafanya kutozoea kujifunza kitu kimoja.
“Inawezekana kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa pili tukajifunza hiki (kwa kutumia picha) basi nabadilisha tunajifunza kingine. Kwa hiyo kuna ubanduaji wa picha kila mara,”anasema.
Anasema wanafunzi hao hufika shuleni kuanzia saa 1.30 hadi saa 2.00 asubuhi, ambapo husaidia kufanya usafi katika darasa lao na kisha kwenda katika mduara wa asubuhi ambapo hufanya ukumbusho wa vitu ambavyo walijifunza siku iliyopita na vile ambavyo ni endelevu.
Anasema baada ya hapo wanaingia darasani ambapo kipindi huanza saa 2.20 asubuhi na kutokana na umri wa watoto hao, kila kipindi chao kina dakika 20 kabla ya kuwapumzisha.
“Kwa hiyo unawapumzisha kwa kuimba nyimbo ili kujiaandaa kwa mahiri nyingine inayofuata, inapofika saa 4.20 asubuhi wanaenda kunywa uji na kisha wakirudi wanakwenda kwenye kona hadi saa 5.20 ambapo wanarudi katika mduara wa kuagana,”anasema.
Katika mduara huo, wanakumbushana walichokisoma, wanaimba nyimbo za kuagana na kuhamasisha elimu na kisha wanaondoka kwenda nyumbani kwa wale ambao wanaweza kwenda wenyewe na wale wasioweza, ana hakikisha anabaki nao hadi mzazi atakapokuja.
Mwalimu Zainabu anasema kuna upimaji wa awali ambao hufanyika pale mtoto anapofika kuandikishwa, ukifuatia na upimaji endelevu ambao hufanyika darasani. Kisha kuna upimaji tamati ambao mtoto hupimwa wakati wa uamuzi wa kwenda darasa la kwanza.
“Upimaji wa awali naupata wakati anapokuja mtoto na mzazi wake. Utambuzi wa awali unanifanya kumtambua mtoto palepale mwenye hofu nimtoe hofu. Yule aliyechangamka namweka karibu ili kumpunguza uchangamfu wake ambao unaweza kuleta usumbufu,” anasema.
Anatoa mfano watoto wanaojulikana kuwa wanafanya fujo huwekwa mbele ili akiwahi kumaliza kazi zake, aweze kuwasaidia wasifanye usumbufu kwa wengine.
Mwalimu huyo anasema ndani ya mwaka mmoja wa elimu ya awali, mtoto anatakiwa awe amejua irabu, silabi kwa kuzisoma na kuziandika, kuchora maumbo rahisi na kufanya hesabu rahisi za kujumlisha na kutoa.
“Watoto wa elimu ya awali wanasoma moja hadi 20 hatumvukishi hapo. Ndani ya mwaka mmoja unahakikisha mtoto ameiva anaweza kuandika moja hadi 20 bila kubabaika na kuisoma,” anasema.
Kuhusu matumizi ya bakora kwa wanafunzi wake, anasema bakora anayotumia kuwachapa ni ndogo sana, ilimradi ionekane kuwa ni fimbo na inatumika iwapo ametenda kosa kubwa ambalo lisipodhibitiwa linaweza kuwaathiri wengine.
“Lakini kafimbo hako kanatumika baada ya kumuonya mara kadhaa na kuona tatizo linajirudia na kwa hawa watoto wadogo, wanatakiwa kuonywa mbele za wenzake ili nao wajifunze kutoka kwake,” anasema.
Anasema upendo sio tu unamsaidia kuwa karibu na watoto, lakini pia unasaidia kuzuia utoro, akieleza watoto hao wamekuwa ni marafiki zake hata wakati anaposhindwa kwenda kazini, ni lazima apige simu kuzungumza na watoto hao. Kwake hatua hiyo ni wito anaouamini kama mwalimu aliyekabidhiwa jukumu la kuwalea na kuwaandaa watoto hao ili kujiunga na elimu ya msingi.
“Hadi kuna mwalimu mmoja huwa ananiuliza hawa watoto wote umewazaa?Mtoto wangu mmoja akikosa uji hapa niko tayari kwenda kwa walimu kuomba gesi nimpikie mwanangu,”anasema.
Zainabu ambaye neno mtoto mzuri haliondoki kinywani mwake, anasema hata wakati wa kuagana na wanafunzi hao kwenda majumbani, lazima wagongesheane mikono lengo likiwa ni kuwasogeza karibu.
Zainabu anasema amekuwa akiwasafisha watoto ambao wanajichafua, jambo ambalo limefanya hata walimu wa madarasa ya juu kumuita kwa maelezo kwamba hana kinyaa.
“Mimi nafanya kwa moyo mmoja, sina neno, namwambia mtoto pole mtoto, usijisikie vibaya na nazuia pia wenzake wasimuuite majina mabaya. Na wakimuita majina mabaya nawachapa mbele yake ili iwe fundisho kutomwita mwenzao majina mabaya kwa ajili tu ya bahati mbaya zinazotokea,”anasema.
Anawashauri walimu wenzake kuondoa unyanyapaa kwa watoto hao wadogo, kwa kuwasafisha pale wanapojichafua darasani, wakiwaacha anasema hali hiyo huwaathiri kisaikolojia.
“Kwa mfano mimi hapa darasani mtu akijichafua, akipata haja, mimi namsafisha, ninafua zile nguo na kumbadilisha nguo kwa sababu ninazo nguo za watoto wa kike na kiume kwa sababu ya dharura kama hiyo. Nina sabuni, nguo za kubadilisha, nina mafuta ya nazi,”anasema na kuongeza:
“Namrudisha darasani, halafu nampigia simu mzazi kuwa mwanangu leo amepata changamoto naomba usimuadhibu, yuko salama na nguo zake ziko shuleni. Kesho anakuja na nguo zake.”
Anasema anatamani walimu wenzake wafanye kitu kama hicho ili kuwafanya watoto wasijisikie vibaya katika kujifunza, kwa sababu hali hiyo huwa ni bahati mbaya hata wao pengine iliwahi kuwatokea.
Zainabu anasema shule hiyo awali ilikuwa na madarasa matano, hivyo iliwalazimu watoto wa elimu ya awali kusoma nje ya vyumba vya madarasa.
“Tulikuwa tunasoma kipindi ambacho mvua hakuna, ikifika kipindi cha mvua ina maana watoto walikuwa hawasomi katika kipindi chenye mvua kubwa, wanawaambia wazazi watoto wasije shule,”anasema.
Hata hivyo, anaishukuru Serikali kwa kuboresha shule hiyo kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuwajengea madarasa ya kutosha na hivyo watoto hao kuwa na darasa la elimu ya awali.
Anasifu mabadiliko kwenye mtaalaa mpya, akisema mtaala wa awali haukuwekewa mkakati na wala haukuwa na mkazo wa umri rasmi wa mtoto kuanza kusoma, jambo analosema ilifikia kuwapokea watoto hata wenye umri wa miaka miwili na nusu.
“Tunaishukuru sana Serikali imeweza kutambua kuwa mtoto wa miaka mitano anaweza kujifunza mahiri husika na akawaeka kichwani anachofundishwa, lakini faida nyingine mtalaa huo unarahisisha mtoto kuelewa kwa haraka ikiwa mwalimu atauzingatia na kuufuata kikamilifu,”anasema.
Zainabu anasema kupitia mada chopeko, wanaweza kuwafundisha watoto uzalendo kwa kufahamu rangi za bendera, awamu za urais zilizopita na kuzitaja na pia namna wanavyoweza kuzingatia alama za barabarani wakati wanapotaka kuvuka barabara.
Anasema mtalaa huo pia umewezesha elimu jumuishi kutekelezwa kwa kuwaingiza katika madarasa ya awali na hivyo katika darasa lake lenye watoto 64, watatu wana mahitaji maalumu.
Lugha mama bado ni changamoto
Anasema watoto kuzungumza lugha mama wanapofika shuleni kwa mara ya kwanza, ni miongoni mwa changamoto ambayo ipo kwa kiasi kikubwa vijijini na mijini kwa kiasi kidogo.
“Kuanza kubadili lugha yake ya nyumbani na kumfanya atumie lugha ya shule inakuwa ni changamoto japo sio kubwa sana kwa mijini,”” anasema mwalimu huyo.
Anasema ushirikiano kati ya wazazi na walimu nayo imekuwa changamoto, kwani elimu ya awali inahitaji nguvu ya mzazi, mwalimu na mtoto kwa kushirikiana kwa kuwa kitu kimoja.
Zainabu anashauri elimu itolewe kwa wazazi kuwa wanalo jukumu la kuchangia lishe ya watoto kwa kuwa wapo baadhi yao hawafanyi hivyo na hivyo kuwajengea chuki walimu katika suala hilo.
Zainabu ambayo yuko katika taaluma hiyo kwa miaka 22 sasa, anasema alimaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mwembeni iliyoko Wilaya ya Manyoni mkoani Singida mwaka 1990.
Anasema mwaka 1994 alimaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mkwese, Wilaya ya Manyoni na kwenda kusoma ualimu katika Chuo cha Ualimu Tabora ambapo alihitimu mwaka 1997.
Anasema shule ya kwanza kuanza kufundisha baada ya kutoka chuoni ilikuwa ni Mlowa.
Zainabu ambaye ana miaka tisa tangu aanze kufundisha darasa la awali, anasema alibobea kupenda kufundisha elimu ya awali baada ya mtalaa mpya ulioboreshwa.
Mtalaa huo ulianza kutumika mwaka 2024 kwa baadhi ya madarasa likiwemo la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
Crédito: Link de origem