Unguja. Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji imepanga kutekeleza vipaumbele vitano ikiwa ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa ajira za staha 20,000 ndani na nje ya nchi mwaka 2025/26.
Kati ya ajira hizo, 4,000 ni za nje ya nchi na zingine 16,000 ni za huku ikipambana na ajira za watoto katika sehemu za kazi kwa ajili ya kuzuia utumikishwaji wa watoto chini ya miaka 18.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi 20,000, kuwezesha vikundi vya kijamii, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kukuza masoko ya bidhaa.
Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26 leo Mei 14, 2025 kwenye kikoa cha Baraza la Wawakilishi, waziri mwenye dhamana, Shariff Ali Shariff ameliomba baraza hilo kuidhinisha Sh42.456 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele hivyo.
“Kwa mwaka wa fedha 2025/26 ofisi itaendelea kusimamia upatikanaji wa ajira kwa vijana, kusimamia sheria za kazi pamoja kuimarisha uwekezaji na uwezeshaji ili kuimarisha uchumi wa nchi na ustawi wa jamii yetu,” amesema.
Shariff amesema pia wataratibu kuimarisha mazingira ya kazi na uhusiano kazini, kusimamia ulinzi wa haki za wafanyakazi, ulinzi wa afya na usalama kazini na utatuzi wa migogoro ya kazi na kufanya mageuzi ya kitaasisi ili kuimarisha utendaji kazi.
“Utekelezaji wa vipaumbele vilivyotajwa vitakwenda sambamba na uimarishaji wa sera, sheria, mipango, ufuatiliaji, tathmini na tafiti, pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa ofisi ili kuleta ufanisi,” amesema Waziri Shariff.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kipaumbele kingine ni kukuza na kuwezesha uwekezaji binafsi kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, mifumo rafiki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), miundombinu ya uwekezaji katika maeneo huru, na kurahisisha taratibu za utoaji huduma ili kushajihisha uwekezaji wenye tija zaidi wa kimkakati na wa visiwa vidogovidogo.
Pia, watasajili vyama vya ushirika 2,000, kukagua vyama 500 na kufuatilia vyama vya ushirika 1,000 na kuthibitisha mikataba ya kazi 10,500 kwa ajili ya kuhakikisha kama inakidhi viwango vya kimataifa.
Katika mpango huo, wizara inatarajia kusajili miradi ya uwekezaji 90 yenye thamani ya Dola za Marekani 390.670 milioni sawa na Sh1.052 trilioni inayotarajiwa kutoa ajira 3,000 kwa wazawa.
“Kuimarisha upatikanaji wa masoko kupitia ushirikiano na ndani na nje ya nchi, kuweka mifumo madhubuti ya ukaguzi na usimamizi wa fedha, kuhimiza uwazi, maadili na uwajibikaji pamoja na kujenga uelewa kuhusu misingi ya ushirika yenye tija,” amesema Waziri Shariff.
Katika hatua nyingine Shariff amesema wizara itashajihisha uwekezaji wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi katika miradi ya kimkakati ya nishati, utalii wa daraja binafsi la juu, teknolojia, uchumi wa buluu, anga, afya na michezo.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa sheria za kazi na uhusiano kazini zinafuatwa, wizara itafanya ukaguzi kazi kwa taasisi binafsi 708 na vyama vya wafanyakazi 13 na jumuia za waajiri mbili.
Kuridhia mikataba sita ya Shirika la Kazi Duniani inayohusiana na usalama na afya kazini, hifadhi ya jamii, mafao ya wafanyakazi wanaopata majanga kazini, wafanyakazi wa majumbani, sera ya ajira na mfumo wa uhamasishaji wa masuala ya usalama na afya kazini.
Hata hivyo, waziri huyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa mifumo ya kielektroniki katika kurahisisha utendaji kazi ili kutoa huduma bora.
Amesema ofisi yake imeshaanza matayarisho ya awali ya kukusanya taarifa zote zinazohitajika kwa ajili ya kuziwasilisha kwa mtaalamu elekezi ili aweze kujua mahitaji ya mfumo unaotakiwa.
Akiwasilisha maoni ya kamati ya Utalii Biashara na Kilimo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtumwa Peya Yussuf amesema wanaishauri Serikali kumaliza mchakato wa sheria ya usalama na afya kazini ili kuipa meno idara hiyo iweze kufanya kazi vizuri.
Kamati inaipongeza wizara kwa kuratibu upatikanaji wa ajira za staha ndani na nje ya nchi, kwani hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kauli hiyo pia imetolewa na mwakilishi wa Mtambwe, Dk Ali Mohamed Suleiman ambaye amesema licha ya kuratibu jambo hilo lakini ni muhimu kuhakikisha ajira zinazopatikana zinaendana na haki na misingi ya Kizanzibari, kwani kumekuwapo na ajira zinazotweza utu wa watu.
Naye mwakilishi wa Viti Maalumu, Mwantantu Mbaraka Khamis ameitaka wizara kuhakikisha inaratibu masilahi ya vijana ambao wameajiriwa katika sekta binafsi kwani kumekuwapo changamoto za baadhi ya taasisi kukiuka mikataba ya kazi.
Crédito: Link de origem