Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amewataka watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kuratibu na kusimamia vyema taarifa za utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa sahihi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
Akizungumza leo Machi 14, 2025, wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ngome, Jijini Dodoma, Waziri Lukuvi alisema watendaji hao wana jukumu kubwa la kusimamia shughuli za Serikali na kuzitangaza kwa wananchi.
“Tunalo jukumu la kuwaambia wananchi kazi zilizofanywa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi. Tunapaswa kuzipambanua kwa ufasaha ili wananchi wazijue kwa uhakika huko waliko,” amesema Waziri Lukuvi.
Aidha, amesisitiza kuwa uratibu mzuri wa taarifa za Serikali unapaswa kuanzia ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha majukumu yote yanasimamiwa ipasavyo kabla ya kufikisha taarifa kwa umma.

Waziri Lukuvi pia amempongeza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Jim Yonazi, pamoja na timu ya menejimenti kwa usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali na kuhimiza mashirikiano zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Dk. Jim Yonazi, amemshukuru Waziri Lukuvi na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo kwa miongozo wanayoitoa ambayo inasaidia katika utendaji kazi wa kila siku.
“Viongozi wetu wakuu wanafahamu kazi tunazofanya na kupitia nyie, tunaomba mtufikishie shukrani kwao,” amesema Dk. Yonazi.
Naye Msaidizi wa Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Maisha Mbilla, amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mazingira mazuri ya kazi na kuhakikisha watumishi wake wanapata stahiki zao kwa wakati.

“Hii inatutia faraja na moyo. Tuna wajibu kama chama cha wafanyakazi kuhimiza watumishi waendelee kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni, na taratibu za Utumishi wa Umma,” amesema Mbilla.
Kikao hicho kimekuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha watendaji wa Serikali wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi, kwa lengo la kufanikisha maendeleo na ustawi wa taifa.
Crédito: Link de origem