Tabora. Watumishi wa taasisi zinazohusika na ununuzi wa umma wametakiwa kufanya kazi kwa weledi badala ya kukwamisha kazi kwa visingizio visivyo na tija kama vile kuchelewa kwa Mfumo wa Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Nest).
Mafunzo hayo yanayotolewa kwa muda wa siku tano yenye washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyoanza Aprili 7, 2025 na kuhitimishwa Aprili 11,2025 yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa taasisi zinazohusika na ununuzi wa umma juu ya matumizi sahihi ya mfumo huo.
Akizungumza leo Aprili 8,2025, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk John Mboya katika mafunzo yanayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa wataalamu kutoka taasisi mbalimbali nchini, amesema kufanya ununuzi kwa mfumo huo ni lazima kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kujiridhisha na makandarasi wanaoomba kazi kwani bila kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuingia mkataba na makandarasi hewa.
“Niseme tu, lazima tufanye kazi na tuzingatie maadili, mtu akiwa na maadili hawezi kuwa mzembe, lakini pia tuwe makini na makandarasi wanapoomba hizi kazi maana kazi inaweza kuwa inachelewa kumbe mkataba ni wa mkandarasi hewa,”Dk Mboya.
Aidha, Meneja wa PPRA Kanda ya Magharibi na Kati, Summa Atupele amesema ni lazima mtumishi afahamu sheria ya ununuzi inataka nini ili aweze kutimiza wajibu wake vizuri huku akiwasisitiza kuacha tabia ya kuwa kikwazo katika kazi kwa kisingizio cha mfumo.
“Yaani mtumishi akishajua mfumo unataka nini na akiwa muadilifu ni vigumu sana kuleta hoja za kwamba mfumo sijui ni mzito na mambo mengine kama hayo lakini pia wameshajua kuwa ununuzi wa dharura unataka nini,” amesema Atupele.
Kalenzo Eliazeli amesema mafunzo yamewasaidi kujenga uelewa zaidi kwani mfumo huo unaboreshwa kila wakati huku akiahidi kufanya vizuri zaidi ya awali.
Naye Mwanaidi Makao, amesema awali alikuwa haelewi hatua za kufuata ili kukamilisha ununuzi katika mfumo huo, hivyo kwa sasa amepata uelewa mzuri zaidi.
“Mwanzo nilikuwa miongoni mwa watu wanaosema mfumo unasumbua sana kumbe mimi ndio nilikuwa sijui hatua za kufuata kwa mfumo wa kawaida na ule wa dharura,”amesema.
Crédito: Link de origem