Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia leo ambapo mkoa wa Dar es Salaam imeshuka na Mtwara ikipaa zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ewura leo Jumatano Juni 4, 2025 bei hizo zimezingatia mabadiliko ya bei katika soko la dunia, gharama za uagizaji, viwango vya kubadilisha fedha za kigeni pamoja na viwango vipya vya usafirishaji wa mafuta vilivyotangazwa Aprili mwaka huu.
Katika jiji la Dar es Salaam, bei mpya kwa lita moja ya petroli itakuwa Sh2,885, dizeli Sh2,826 na mafuta ya taa Sh2,877. Ikilinganishwa na awali ambapo petroli ilikuwa Sh2,912 dizeli Sh2,859 na mafuta ya taa Sh2,877 kwa lita.
Bandari ya Tanga bei ya petroli itakuwa Sh2,946, dizeli Sh2,887 na mafuta ya taa Sh2,938 huku Mtwara itakuwa na bei ya juu zaidi, ambapo petroli itauzwa Sh2,978, dizeli Sh2,918 na mafuta ya taa Sh2,969.
Ewura imeeleza kuwa kwa Juni 2025, bei ya mafuta katika soko la dunia imepungua kwa wastani wa asilimia 0.9 kwa petroli, asilimia 3.4 kwa dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.
Hata hivyo, gharama za uagizaji zimeongezeka katika baadhi ya bandari ikiwa ni pamoja na ongezeko la hadi asilimia 51.55 kwa petroli kupitia Bandari ya Mtwara.
Kwa mujibu wa Ewura, kampuni za mafuta zinaruhusiwa kuuza kwa bei ya ushindani ilimradi zisizidi bei kikomo au kushuka chini ya kiwango cha chini kilichowekwa kisheria.
Wateja wanashauriwa kununua katika vituo vinavyotoa bei nafuu zaidi ili kuendeleza ushindani wa kibiashara.
Aidha, vituo vya mafuta vinatakiwa kuonyesha wazi bei zao na kutoa stakabadhi kutoka kwenye mashine za kielektroniki (EFPP) kwa kila muamala, kama njia ya kuthibitisha uhalali wa bei na ubora wa mafuta yanayouzwa.
Wakati bei hizi mpya zikianza kutumika kesho, Ewura imeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wafanyabiashara watakaokiuka miongozo hiyo.
Kwa wakazi wa mikoa mingine, bei za mafuta pia zimebadilika kwa mujibu wa umbali na gharama za usafirishaji ikiwemo Mwanza ambapo petroli ni Sh3,070, na dizeli Sh3,011
Arusha petroli ni Sh2,994 na dizeli Sh2,935 na Mbeya petroli ikiuzwa Sh3,017, dizeli Sh2,958 huku Kigoma petrol ikiuzwa Sh3,083, dizeli Sh3,023.
Crédito: Link de origem