top-news-1350×250-leaderboard-1

Watetezi Kanisa la Gwajima waongezeka

Dar es Salaam. Wakati waumini 84 kati ya 86 waliokamatwa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima wakiachiwa huru na Polisi, taasisi na watu mbalimbali wameendelea kujitokeza kupinga iliyochukuliwa na Serikali ya kufuta kanisa hilo linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima.

Waumini hao ni miongoni mwa waliokamatwa usiku wa kuamkia Juni 3, 2025, kufuatia mvutano uliotokea kati yao na Polisi, lililotinga makao makuu ya kanisa hilo Ubungo, jijini Dar es Salaam kuwatawanya waumini.

Chanzo cha kadhia hiyo ni hatua Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kutangaza kulifuta kanisa hilo, kile alichoeleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 “kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”

Kihampa alitangaza hatua hiyo Juni 2, 2025 siku chache baada ya Askofu Gwajima kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia matukio ya watu kutoweka na kutekwa, huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje ikiwa matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi mbalimbali, akiwemo yeye mwenyewe.

Kauli zake ziliwaibua baadhi ya watu wakiwemo wabunge wakimshutumu, naye akatumia mimbari ya kanisa hilo kuwajibu, kama ambavyo amekuwa akifanya kwenye baadhi ya matukio.

Baada ya kanisa kufungiwa askari polisi walifika kanisani hapo usiku na kuwatawanya waumini waliokuwa kwenye maombi, kisha kuwakamata makumi miongoni mwao.

Peter Kibatala, wakili wa Askofu Gwajima amesema mapema leo Alhamisi Juni 4, kuwa jumla ya waumini 86 walikamatwa na miongoni mwao 84, waliachiwa kwa dhamana jioni ya Jumatano Juni 4, 2025.

“Waumini 86 walikamatwa, wameachiwa wote kwa dhamana isipokuwa wawili ambao taarifa zao tutazitoa baadaye,” amesema Wakili Kibatala ambaye pia jana alisema “Askofu Gwajima yuko eneo salama na hashikiliwi na mtu yeyote.”

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alipoulizwa na Mwananchi leo kuhusu kushikiliwa na kuachiwa kwa waumini hao, alijibu kwa kifupi kwamba kuna tofauti kati ya kukamatwa na kushikiliwa.

Juni 3 Muliro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema: “Kuna watu ilibidi tuwachukue ili kuzungumza nao, watueleze kwa undani kama walikuwa hawaelewi kilichokuwa kinatekelezwa na maofisa wa polisi au walikuwa wanafanya tu kukataa, ili kusasabisha fujo.”

Waumini hao walikuwa kwenye maombi ya siku saba yaliyoanza Juni 2, 2025, lakini hayakuweza kuendelea baada ya kanisa hilo kuwekewa utepe wa zuio na kuwa chini ya ulinzi wa polisi.

Hadi leo, Juni 5, 2025, askari wenye silaha pamoja na gari la maji ya kuwasha bado wanaendelea kuimarisha ulinzi kwenye kanisa hilo.

Hali hiyo ndiyo iliyowaibua wanasiasa na viongozi wa dini kulaani hatua hiyo, ambapo James Mbatia, mwanasiasa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, leo Alhamisi amekutana na waandishi wa habari na kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo hilo la kufungwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Mbatia amesema Askofu Gwajima kama alionekana ametetereka kulingana na usajili wake, alipaswa kupewa onyo kali kwa namna yoyote.

“Huwezi kwenda kuvamia watu wapo wanasali, sasa hivi malalamiko yaliyopo watu wanatoka nje ya Gwajima wanapaza mambo mengine, Gwajima siku za nyuma alipaza sauti juu ya matukio ya utekaji katika taifa na kueleza nini kifanyike.

“Gwajima sio askofu tu, ni mbunge na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, kwa hiyo hekima inahitajika kutatua mambo magumu kama yale, umefanya jambo lile unanyanyua hasira na kuibua mambo mengine ambayo yanavuka mipaka ya Gwajima na kuibua mambo makubwa zaidi,” amesema.

Mbatia ambaye ni mtaalamu wa majanga, amesema hakukuwa na haja ya kutumia mitutu ya bunduki kumtafuta askofu huyo, badala yake angeitwa kama alihitajika.

Mbatia amesema wenye dhamana wanapaswa kushirikiana lakini imekuwa bahati mbaya wenye dhamana wamekuwa wakitoa maneno ya kejeli, akitolea mfano kauli zilizotolewa bungeni juu ya yale yanayoendelea.

Amewaomba wenye mamlaka kuangalia wanachoongea, wanaongea na akina nani na kwa wakati gani, ili kuleta taifa pamoja na kuacha kukejeli watu.

Kutokana na hayo, mwanasiasa huyo amesema Serikali ina jukumu la kukaa meza moja na wadau mbalimbali, ili kuondokana na vuta nikuvute inayoendelea, ambayo inaweza kuleta shida nchini.

“Hofu tuliyonayo sasa inahifadhiwa katika historia kwa kutumia kalamu yenye kutumia damu ya waathirika wa migogoro. Kalamu ya udugu, umoja itumike kujenga historia ya mama Tanzania,” ameshauri.

Mbali na Mbatia, mwingine aliyezungumzia tukio hilo ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema – bara, John Heche aliyesema uamuzi wa Serikali kufuta kanisa hilo unakiuka uhuru wa kuabudu kama unavyolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Chadema tunapinga vikali kufutwa kwa kanisa la Ufufuo na Uzima. Huu ni mwendelezo wa juhudi za kimfumo kuziba midomo ya wale wanaoamua kusimama na kusema ukweli. Ni hatari kwa taifa na ni uvunjifu wa haki za msingi,” alisema Heche Jumatano wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Heche pia ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kusimama kidete kusema ukweli bila hofu,  akisisitiza dini ni mhimili muhimu wa maadili na haki katika jamii, hivyo viongozi hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea dhuluma bila kuchoka.

“Naomba viongozi wa dini wasikate tamaa. Waendelee kusema hadharani, waendelee kuwa sauti ya watu wasio na sauti. Taifa linawahitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote,” alisema.

Alichokisema Mzee wa upako

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) Tanzania, Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako ameiomba Serikali kuacha kufunga makanisa.

Mchungaji Lusekelo amesema kanisa ni taasisi na hivyo akihoji, watoto wanaosali Jumapili wana makosa gani na kwa nini kondoo watawanywe.

“Sitetei mambo ya Gwajima, yeye anajuana na CCM wenzake huko, lakini kufunga kanisa si jambo zuri, unafunga kanisa halafu watoto wakasali wapi Jumapili…? Wewe shughulika na Mzee wa Upako…nyie endeleeni kusali lakini Mzee wa Upako tunamhitaji, si kufunga kanisa,” amesema Lusekelo.

Kiongozi huyo amesema inahitajika hekima kumuua nyoka bila kuharibu mayai, akieleza masikitiko kuwekwa kwa utepe eneo la kanisa, akishauri Gwajima ndiye angetafutwa.

Amesema “Askofu Gwajima ana makosa na wale waliofunga kanisa wana makosa, lakini makosa ya askofu huyo hayahalalishi makosa yao.

“Sasa  mimi kinachoniumiza ni kufunga kanisa. Msifunge kanisa, mkamateni huyo huyo waacheni watoto Jumapili waende kanisani, tafuteni namna na huyo mtu wenu,” amesema na kuongeza:

“Mfukuzeni kwenye chama chenu cha CCM, mnyang’anyeni ubunge, mpigeni mikwara hadi anyooke lakini watu waendelee kusali.”

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.