Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wateja wa Benki ya CRDB sasa watakuwa na uwezo wa kukopa hadi Sh milioni moja bila kuweka dhamana kupitia huduma mpya ya mkopo wa kidigitali ijulikanayo kama Jinasue.
Akizungumza leo Machi 25,2025 wakati wa kuzindua huduma hiyo Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi CRDB, Stephen Adili, amesema lengo ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora na nafuu.
Amesema huduma hiyo inawalenga wateja wote wa CRDB ambao ni zaidi ya milioni sita na ambao si wateja watatakiwa kufungua akaunti ya CRDB na kufanya miamala.
“Unapokwama kwenye suala la kifedha unafikiria unatokaje lakini kwa kutumia simu ya mkononi kupitia Applikesheni ya Simbanking unajinasua mwenyewe.

“Mkopo huu hauna dhamana na riba yake ni asilimia nane tu, mdhamini ni akaunti yako na miamala yako…tunawashauri watu waachane na mikopo umiza waje kwenye mikopo ambayo ni rasmi,” amesema Adili.
Mkurugenzi wa Creditinfo Tanzania, Edwin Urasa, amesema huduma hiyo itasaidia kuongeza wigo wa Watanzania wenye akaunti CRDB kupata unafuu wa kukopeshwa bila dhamana.
Naye Mchekeshaji Eliud Samwel, ameipongeza benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma hiyo na kushauri Watanzania ambao hawana akaunti katika benki hiyo kufungua ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
Crédito: Link de origem