top-news-1350×250-leaderboard-1

Watanzania wahamasishwa kushiriki siku ya haki za mtumiaji

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani ili kujifunza kuhusu haki za mtumiaji na jinsi ya kutumia huduma salama.

Wito huo umetolewa leo Machi 10,2025 na Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF), Daudi Daudi, alipokuwa akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani inayoadhimishwa Machi 15.

Amesema maadhimisho hayo yanakusudia kuhamasisha matumizi salama na endelevu ya rasilimali huku yakitoa jukwaa la majadiliano kati ya watumiaji, watoa huduma na wadau wa maendeleo.

Aidha amesema maadhimisho ya kitaifa yatafanyika mkoani Morogoro yakibebwa na kaulimbiu ya ‘Haki na Maisha Endelevu kwa Mtumiaji” ambayo inahimiza matumizi endelevu ya rasilimali, ambayo ni masuala ya msingi kwa maendeleo ya taifa.

Amesema maadhimisho hayo yanaadhimishwa kimataifa kwa lengo la kulinda haki za watumiaji na kuhimiza matumizi salama na endelevu ya huduma.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi kupata elimu kuhusu haki zao, huku Serikali na wadau wa sekta husika wakihimizwa kuhakikisha huduma bora na za haki zinapatikana kwa wote.

“Mtumiaji anapaswa kuwa na nguvu ya kufanya maamuzi sahihi kwa kupata huduma salama, nafuu, na endelevu. Kila mtu ana haki ya kuishi katika jamii inayowajibika kulinda mazingira na rasilimali kwa vizazi vijavyo,” amesema Daudi.

Mwenyekiti huyo amesema katika maadhimisho hayo wanatilia mkazo matumizi salama ya huduma katika sekta za nishati, mawasiliano na usafiri wa anga na nchi kavu.

Serikali inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Tusibaki nyuma katika mabadiliko haya, kutumia nishati safi si tu kwa faida ya leo, bali kwa afya na ustawi wa kesho,” amesema.

Kwa upande wa mawasiliano, usalama wa mtumiaji mtandaoni ni ajenda muhimu mwaka huu ambapo TCF itahimiza ulinzi wa faragha na matumizi salama ya huduma za kidijitali.

Vilevile usalama katika sekta ya usafiri wa anga na nchi kavu utaangaziwa ili kuhakikisha huduma bora kwa watumiaji.

“Dunia ya kidijitali inazidi kukua, lakini hakuna maendeleo bila usalama. Mtumiaji anapaswa kuwa na hakikisho kuwa taarifa zake zinalindwa,” amesema.

Maadhimisho hayo yanaandaliwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) linalojumuisha mabaraza ya kutetea watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa ambayo ni LATRA-CCC, TCAA-CCC, EWURA-CCC, na TCRA-CCC pamoja na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la The Foundation for Civil Society (FCS).

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.