top-news-1350×250-leaderboard-1

Wasomi wajitosa sakata la ugawaji wa majimbo

Dodoma. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikihitimisha upokeaji wa mapendekezo ya kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi, wasomi wameonya kwamba uongezaji wa majimbo ni kuwaongezea wananchi mzigo wa gharama.

INEC ilianza kupokea maoni hayo Februari 26, 2025, na leo Machi 26, 2025, mchakato huo umehitimishwa, ambapo tayari jumla ya majimbo tisa yameomba kugawanywa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ukubwa wake na idadi kubwa ya watu.

Majimbo yaliyopendekezwa kugawanywa na wabunge wake kwenye mabano ni Dodoma (Anthony Mavunde), Mbeya Mjini (Dk Tulia Ackson), Ukonga (Jerry Silaa), Kigoma Vijijini (Vuma Augustine) na Kilindi (Omari Kigua).

Majimbo mengine ni Handeni Vijijini (John Salu), Muheza (Hamis Mwinjuma), Mbeya Vijijini (Oran Njeza) na Mbarali, ambalo kwa sasa linaongozwa na Bahati Ndingo.

Sheria inaelekeza ugawaji wa majimbo kufanyika kila baada ya miaka 10 kama itaonekana kuwa na haja ya kufanya hivyo. Mara ya mwisho, tume iligawa majimbo mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yaliongezwa.

Hadi sasa, Tanzania ina majimbo ya uchaguzi 264, ambapo Tanzania Bara yapo 214 na Zanzibar 50. Hata hivyo, Bunge lina jumla ya wabunge 393, ambapo wa majimbo ni 264, wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais, wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, wabunge 113 wa viti maalumu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akitangaza kuanza kupokea mapendekezo Februari 26, 2025, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alisema vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini ni kuanzia watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia watu 400,000.

Aliongeza kuwa idadi ya watu itakayotumika ni ile iliyotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Jaji Mwambegele alivitaja vigezo vingine kuwa ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Machi 26, 2025 kuhusu mchakato wa ugawaji wa majimbo, wadau wametaka sasa kuwe na ukomo wa idadi ya wabunge na iwekwe kisheria kwa sababu watu wanaongezeka, lakini ardhi iko vilevile, hivyo kuruhusu ugawaji wa majimbo kunaweza kuwa mzigo mzito kwa taifa.

Gharama zinazotajwa kuongeza mzigo kwa wananchi ni pamoja na mishahara na marupurupu ya wabunge watakaoongezeka, ofisi za wabunge hao, fedha za mwa jimbo na gharama nyingine za vifaa vya uchaguzi wakati wa uchaguzi.

Machi 22, 2024, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliibua mjadala aliposema hadi mwaka 2020, mishahara ya wabunge ilikuwa imepanda kutoka Sh13 milioni hadi Sh18 milioni kwa mwezi.

Hata hivyo, Bunge, kupitia Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, lilikanusha taarifa hiyo, likieleza kuwa hakukuwa na nyongeza ya mishahara kwa wabunge. Pia, taarifa hiyo haikuweka wazi kiwango wanacholipwa kama mishahara au marupurupu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda, amesema ugawaji wa majimbo ni mzigo kwa wananchi na hauna sababu ya msingi, badala yake, amependekeza kutungwa kwa sheria ya kuzuia ongezeko la majimbo.

Dk Mbunda amesema kazi za mbunge si za kila siku kama inavyodaiwa, kwani mambo mengi yanafanywa na manispaa au halmashauri. Kwa mujibu wake, muundo wa majimbo unatoa uwakilishi wa kutunga sheria, na si lazima majimbo yaongezwe.

“Hivyo, tunakwenda kuongeza jengo au kulipanua. Nasema, hakuna maana kwamba ndiyo tunakwenda kuongeza uwezo wa watu mle ndani; badala yake, watabaki hivyo, lakini fedha za walipakodi zinateketea bure,” amesema Dk Mbunda.

Mwanazuoni huyo amesema kuna gharama kubwa za kumtunza mbunge, na lazima zitabebwa na wananchi, ikiwemo mishahara na marupurupu.

“Ifike mahali tuseme hatuhitaji kuongeza idadi ya wabunge. Tuwe na ukomo, na hasa mijini, ndiyo maana hata mimi siyo mpenzi wa kuongeza hayo majimbo. Ni bora kuongeza halmashauri kuliko majimbo katika nchi changa kama yetu,” amesema.

Naye, Ezekiel Oluoch, Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), amesema nchi imekosa kipaumbele sahihi, hivyo inazalisha nafasi za ulaji kwa wanasiasa.

Oluoch amesema Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia maendeleo ya watu, lakini kinachofanyika ni kinyume chake.

“Hadi mwaka jana (2024), tulikuwa na walimu kama 270,000, kati ya zaidi ya 500,000 wanaotakiwa. Sasa kipaumbele cha kuongeza wabunge ni kipi? Ni kweli tunahitaji hilo?” amehoji Oluoch.

Oluoch, aliyewahi kuwa mbunge katika Bunge la Katiba, ameitaka Serikali kuiga mfano wa taifa la China, ambalo licha ya kuwa na idadi kubwa ya wananchi, lina wabunge wachache.

Amesema hakuna faida ya kugawa majimbo, kwa kuwa mbunge hana kazi za moja kwa moja zaidi bungeni, huku akihoji ni kwa nini wilaya na halmashauri, ambazo watendaji wake wanakuwa na majukumu mengi, haziongezwi au kuwekwa zaidi ya mkuu wa wilaya mmoja.

Akiwa na mtazamo tofauti, mtaalamu wa uchumi, Dk Nasibu Mramba amesema kiuchumi, ugawaji wa majimbo hauna maana kubwa, lakini inaweza kuwa na umuhimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Ni kweli baadhi ya majimbo ni makubwa na yanaweza kuwa tatizo kwenye utoaji wa huduma. Kilio cha gharama kinaweza kuwa na ukweli, lakini pia tunapaswa kuzingatia uwiano wa maendeleo kwa wananchi.

““Nadhani ugawaji huo hauko kichumi zaidi, bali ni kisiasa katika utoaji wa huduma kwa wananchi, maana kweli kuna majimbo makubwa zaidi, na ukisema yabaki hivyo siyo sawa. Mfano, Jimbo la Dodoma lina madiwani zaidi ya 50, wakati mengine yana madiwani 10,” amesema.

Wakati wanazuoni wakipinga ugawaji wa majimbo, baadhi ya wanasiasa wameunga mkono mchakato huo.

Katibu wa TLP Mkoa wa Dodoma, Damaly Richard, amesema kuna faida ya kugawa majimbo, kwani yanapokuwa mengi, yanasaidia hata vyama vidogo kupata nafasi.

Damaly amesema ugawaji ulisubiriwa kwa muda mrefu, hivyo kwao wameupokea kwa mikono miwili na wanajiandaa kushinda angalau jimbo mojawapo kati ya yale ya Dodoma, akisema mambo yatakuwa mazuri.

“Napinga hoja ya kuongezeka kwa gharama kwa sababu hata mume mwenye wake zaidi ya mmoja hawezi kuhesabiwa mzigo kama anaweza kuwamudu vema wake zake,” amesema Richard.

Mmoja wa makada maarufu wa CCM, ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema ugawaji wa majimbo unapaswa kufanyika kila inapobidi na siyo dhambi wala kosa.

“Majimbo yanapokuwa mengi, yanatoa fursa kwa watu tofauti wenye uwezo mkubwa kuingia bungeni na kusaidia kuondoa siasa za ‘ndiyo kila jambo,’” amesema kada huyo aliyewahi kugombea ubunge jimbo la Manyoni Magharibi

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.