top-news-1350×250-leaderboard-1

Wanawake wakumbushwa kutafakari suluhisho la ukatili nchini

Arusha. Wanawake nchini wamekumbushwa kutafakari kwa kina kuhusu matukio ya ukatili yanayoendelea nchini, wakati wakisherehekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, athari zake katika jamii na kutoa maazimio ya mapendekezo ya nini kifanyike kukabiliana nayo.

Wito huo umetolewa leo, Machi 6, 2025, jijini Arusha na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax, wakati wa kongamano la wanawake kanda ya kaskazini kuelekea maadhimisho ya kilele cha siku hiyo inayotarajiwa kufanyika Machi 8, 2025 mkoani Arusha.

Dk Tax amesema nchi kwa sasa imekumbwa na matukio ya ukatili yanayoendelea kushamiri siku hadi siku, hasa ya ukatili wa kingono, ubakaji na ulawiti, ambayo yamekuwa yakiacha makovu kwa wanawake na watoto bila kujali jinsia, hali inayohatarisha usalama wa Taifa kwa baadaye.

Amesema ripoti ya sasa ya Benki ya Dunia (WB) inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 45 wamefanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 17 wakikumbwa na ukatili wa kingono.

“Zaidi ya hayo, takwimu zinaonyesha kuwa karibu asilimia 30 ya wasichana wanakutana na ukatili wa kingono kabla ya kufikisha umri wa miaka 18,”

“Hii ni hatari ndugu zangu, na bahati mbaya hali hii imeingia kwa watoto wetu wa kiume, hivyo niombe tunapoadhimisha siku hii, tutumie kongamano hili kuhakikisha tunakuja na majibu ya nini kifanyike ili tuendelee kuona Taifa letu likiwa salama katika uongozi wa kizazi cha baadaye,” amesema Dk Tax.

Akigusia maazimio ya mkutano wa Beijing nchini China mwaka 1995 na tamko la Umoja wa Mataifa, Dk Tax amewataka wanawake wanaopata nafasi mbalimbali kutokana na harakati hizo za utetezi wa wanawake katika nyanja mbalimbali kuzitumia vema.

“Wakati maadhimisho haya yanaendelea kujenga misingi imara ya kutambua nafasi ya mwanamke katika kudai na kutetea haki za msingi kwa lengo la kukuza usawa wa jinsia katika jamii, Tanzania tumepiga hatua kwa kuwainua wanawake na wasichana kushiriki katika masuala ya kiuchumi, kijamii, elimu, mafunzo, afya, mifumo ya uongozi na uamuzi.

“Katika juhudi hizi, niwaombe sana kina mama, tunapopewa nafasi hizi, tuzitendee haki kama ambavyo mmemuona Rais wetu, ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais anavyochapa kazi na anavyoitendea haki nafasi hiyo. Na sisi ametupa nafasi nyingi tukachape kazi ili kuondoa ile tabia ya kuona mwanamke hawezi eti kisa jinsia yake,” amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis, amesema kuwa maadhimisho hayo yanatenga nafasi kwa wanawake kutafakari mambo yao, fursa na changamoto wanazopitia katika kuzitafutia ufumbuzi.

Katika hilo, amewataka wanawake kutafakari mapema nafasi za uongozi zinazowafaa na kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanagombea kuliko kusubiri viti maalumu.

“Mwaka huu wa uchaguzi, tumekubaliana wanawake unyonge haupo, tujitokeze kwa wingi kuhakikisha nafasi za ubunge na udiwani nyingi zinakuwa zetu na kumuunga mkono mgombea mwenzetu mwanamke, sio kusubiri wanaume wakagombee tuje kutoleana macho kwenye viti maalumu,” amesema.

Naye Dk Bakari George, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), amesema wameandaa kongamano hilo lililokutanisha zaidi ya wanawake 100 kutoka nyanja mbalimbali ili kuendelea kupata maoni yao namna ya kukabiliana na mambo yanayowakabili na kukwamisha juhudi zao.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.