Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD) leo, bado inashuhudiwa katika ngazi za uamuzi kuna idadi ndogo ya wanawake, vyama vya siasa vikitajwa kuchangia hali hiyo.
Hata hivyo, wanawake vinara waliojikita mstari wa mbele kwenye masuala ya siasa, wamesema mwaka huu wamejipanga na kuhamasisha wengine kujitokeza kwa wingi kupambania nafasi za uongozi na kuingia kwenye ngazi za uamuzi.
Licha ya hatua iliyofikiwa kwa sasa, bado hali hii haiakisi utekelezaji wa Azimio la Beijing lililopitishwa katika mkutano wa nne wa dunia wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995 chini ya Umoja wa Mataifa, likilenga kukuza haki za wanawake na usawa wa kijinsia duniani.
Ili kutekeleza azimio hilo lililofikisha miaka 30 sasa, ajenda kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, Tanzania ilianzisha mfumo wa viti maalumu kwa wanawake katika Bunge na Serikali za Mitaa ili kuongeza ushiriki wao kwenye ngazi ya uamuzi.
Kwa takwimu zilizopo za mwaka 2020/2021 wabunge wanawake walikuwa asilimia 37 na kati ya hao asilimia 10 pekee ndio walishinda kwenye majimbo ya uchaguzi.
Katika ngazi ya baraza la madiwani wanawake ni asilimia 34.7, kati ya hao waliochaguliwa ni asilimia 6.5 na wanawake wenyeviti wa mabaraza ni asilimia 2.7. Kati ya vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, ni vitatu pekee vyenye wenyeviti wanawake ambavyo ni CCM, ACT-Wazalendo na Sauti ya Umma (SAU), huku vyama vinne vikiwa na makatibu wakuu wanawake ambavyo ni CCK, UDP, CUF na NCCR-Mageuzi.
Wanawake katika baraza la mawaziri mwaka 2020/2021 walikuwa asilimia 36, wanawake naibu mawaziri walikuwa asilimia 21, wakuu wa mikoa walikuwa asilimia 23.1 na wakuu wa wilaya asilimia 28.5.
Licha ya juhudi zinazofanyika, ushiriki wa wanawake katika siasa ili kushika nafasi za uamuzi unakabiliwa na changamoto kadhaa, mfumo dume ikitajwa kama moja ya sababu.
Tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani baadaye mwaka huu, baadhi ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake wamezungumzia kinachopaswa kufanyika ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uamuzi.
Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amesema vyama vya siasa ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kuwania majimbo, lakini bado haviamini kama kundi hilo linaweza kusimama.

Akizungumza Jumatano Machi 5, 2025 akichangia mjadala wa Mwananchi X Space uliojadili mada kuhusu ukomo wa ubunge na udiwani viti maalumu, ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Ruge aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Serengeti, mkoani Mara, mwaka 2020 alisema mwanamke anaweza kushinda katika kura za maoni, lakini anaambiwa ampishe mwanamume ili yeye apewe viti maalumu.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu alisema” “Hii maana yake nini, hakuna utashi wa kisiasa, siyo tu kwenye vyama vingine hata kwenye chama changu. Muda mwingine hakuna utashi wa kisiasa wa kweli wa kuwasaidia wanawake.
“Kwa hiyo hii 50 kwa 50 vyama vya siasa vikiamua inawezekana, lakini kuna ubinfasi wa hali ya juu hasa kwa wanaume wanaotamani wawe wao tu viongozi, lakini pia mtazamo wa jamii kwamba wanawake hawawezi,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema:
“Mwaka huu vyama vya siasa vihakikishe vinawapa fursa wanawake wenye uwezo. Vipo vyama vina idadi ndogo ya wanawake, madai yao ni kwamba vitawatoa wapi wanawake?
“Lakini ukiangalia Tanzania idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume, ila tukija kwenye vyombo vya uamuzi hawapo, ni kwa nini?” amehoji.
Ametoa mfano kwenye majimbo ya ubunge kati ya 264 wanawake wa kuchaguliwa ni wa majimbo 26.
“Hii tunazungumzia miaka 63 ya Uhuru, jambo ambalo si sahihi. Mwaka huu wanawake twende na kaulimbiu ya suala zima la usawa wa kijinsia,” amesema.
Ametoa rai kwa viongozi wa vyama pamoja na mfumo dume uliopo, wahakikishe wanawake wanapewa nafasi ya kugombea.
“Habari njema ni kwamba, sheria ya vyama vya siasa iliyofanyiwa marekebesho mwaka 2024 sura ya 256 inasema wazi kila chama cha siasa lazima kiwe na sera ya jinsia na ujumuishaji. Sera hii itaanza kufanya kazi kwenye uchaguzi huu,” amesema.
Amesema vijana na wanawake washiriki kwenye siasa, ndani ya vyama, kwenye vyombo vya uamuzi vya juu wanawake wapewe nafasi sawa na wanaume.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi, ajenda kuu iwe wanawake wanaweza wapewe nafasi, huwa mara nyingi naona inatokea wanaume wanazuia wanawake kupewa nafasi za majimbo wakidai kwamba wao wana nafasi zao za viti maalumu, hii si sahihi,” anasema.
Lyimo amesema wanaume na wanawake wote wana uwezo wa kugombea idadi sawa ya majimbo.
Akizungumzia katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni, mbobezi wa sayansi ya siasa Profesa Ruth Meena alisema kinachokwamisha wanawake wengi kupatana nafasi za uongozi hasa za kisiasa ni kukosekana utashi wa kisiasa wa vyama.

Profesa Meena alisema vyama vya siasa vinapaswa kubadilisha mfumo ulioko sasa wa uteuzi na kuweka ambao unataka kusimamisha wagombea wawili ambao ni mwanamke na mwanamume.
“Tusipobadilisha mfumo ndani ya vyama tutakuwa tunapoteza muda kuzungumza 50 kwa 50, hili suala linahitaji juhudi za pamoja.
“Hii hoja kwamba wanawake wanahitaji kujengewa uwezo sioni kama ina mashiko kwa sababu wapo wengi wenye uwezo na sifa za kuwa viongozi ila mifumo ndiyo haitaki,” alisema.
Mratibu wa Kitaifa wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Dk Ave-Maria Semakafu anasema kuna wanawake wengi wenye uwezo wa kushika nafasi za uongozi lakini wanakwamishwa na mifumo.
“Hili suala la wanawake wasubiri kujengewa uwezo linatuchelewesha, kwa sababu hakuna shule inayofundisha ubunge. Tuweke mfumo utakaoruhusu ushiriki sawa katika michakato ya demokrasia kwa wanawake na wanaume.
“Miaka 30 baada ya Beijing tulilia ushiriki wa wanawake katika ngazi za uamuzi na michakato ya kidemokrasia lakini bado tuko nyuma kwa sababu mifumo imebaki ileile,” anasema.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Sophia Simba, Februari 28, 2025 aliibua hoja ya ukomo wa viti maalumu katika maadhimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa Ulingo alisema ifike mahali uwepo ukomo wa viti maalumu ili wengine wakalie nafasi hizo.

Mwanasiasa huyu mkongwe akizungumza na Mwananchi amesema wakati wa wanawake kuogopa kuingia kwenye siasa haupo tena, akiwataka waingie kuchuana kwenye majimbo.
“Siyo kwenye ubunge tu, kuna udiwani wengine waanzie huko, haya mambo ya siasa si kuogopa, mwanamke ukiogopa kufanya siasa ndipo hapo tunawaachia wanaume nafasi. Tuingie kwenye uchaguzi tukiwa na ajenda ya usawa wa kijinsia, wanawake na wanaume tupo sawa,” amesema.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Anna Abdallah amewataka wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea majimbo na si kusubiri kuingia kwenye viti maalumu.
“Kina mama wakagombee wasingoje viti maalumu, tunao wanawake wengi wenye uwezo katika siasa, waingie kugombea.
“Wasisubiri vitu maalumu, wakiingia kugombea majimbo maana yake wanawapa vijana fursa ya kujifunza, viti maalumu ni shule, unakwenda kujifunza ukihitimu unaondoka kuwania jimbo,” amesema.

Anasema miaka ya nyuma wanawake hawakuweza kugombea kwa sababu ya utamaduni.
“Tulitafuta namna ya kuwaingiza kwenye vyombo vya uamuzi, lengo likiwa ukishajifunza unawaachia na wengine wanaingia, rai yangu tu kwenye uchaguzi wa Oktoba, wanawake wote wenye sifa wakagombee majimboni,” anasema.
Profesa Meena anasema licha ya kuwa viti maalumu vinasaidia kuongeza idadi ya wanawake viongozi, ikiwemo wabunge lakini uhalisia ni kwamba hawapati stahiki sawa na wale waliopigiwa kura.
“Hawa hawawezi kuteuliwa kushika nafasi ya waziri mkuu na wala hawapati fedha za majimbo zinazowezesha wabunge kuendelea kujinadi kwenye majimbo,” amesema.
Hoja ya wabunge wa viti maalumu kutokuwa na hadhi sawa wale wa majimbo pia imezungumzwa na Ruge aliyesema:
“Mimi siyo muumini wa viti maalumu, naamini katika kusimama kuwania jimbo, hii ni kwa sababu nimeshakuwa mbunge wa viti maalumu na nimeona namna tunavyochukuliwa, hupati ile heshima anayipewa mbunge wa jimbo ndiyo maana nasema vyama viweke mazingira wezeshi na uwanja sawa kwa mwanamke au mwanaume kusimama.”
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa 2025 anasema:
“Lazima tufanye kazi, tuwafuate wananchi kwa mipango bora, unapoingia kugombea uongozi maana yake unaingia kwenye eneo la kupimana nguvu, siyo kusubiri huruma wala kupewa uongozi kama zawadi kwa kuwa ni mwanamke, la hasha!”.
Anasema katika uchaguzi wa mwaka huu, wanawake wasirudi nyuma, wajitokeze wagombea.
“Tunataka kuona wanawake wakiwa kwenye meza ya uamuzi katika kila nyanja. Habari njema ni kwamba, wanawake viongozi huwa tunaamini zaidi katika maendeleo na familia, tukiwa katika uongozi hata rushwa zinapungua,” amesema.
Amewataka wanawake kubeba ajenda ya maendeleo na demokrasia ya kweli ili thamani ya kura ionekane na ulinzi wa demokrasia iliyopiganiwa na waasisi wa Taifa iendelezwe.
“Wanawake tusimame kidete kuleta maendeleo, kina mama ndio wanaozunguka na ndoo kichwani kutafuta maji, hao ndio elimu ikiwa mbaya wanahangaika na watoto, wao ndio watafutaji chakula.
“Ndani ya ajenda ya maendeleo hapo ndipo tunakutana na huduma bora za jamii kama afya, elimu, maji na mengine yote yatakayompunguzia mzigo mwanamke,” anasema.
Mwanaharakati na mtetezi wa haki za wanawake, Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema katika uchaguzi mkuu ujao, wanawake inabidi kuzingatia ajenda ya usawa.
“Katika hili kuna vitu tulishafanikiwa lakini kuna vingine ni kama tumeanza kurudi kinyume-nyume, hivi sasa kila saa anaongelewa mtoto wa kiume, lakini wanasahau kwamba wanawake tumetoka mbali.
“Tunahitaji kulinda sana vitu tulivyokwishavipata, hatutafuti kupambana na wanaume bali tunatafuta usawa,” anasema.
Anasema kwenye uchaguzi ujao, kila mwanamke mwenye uwezo wa kugombea asibaki nyuma, afuate mifumo na kugombea kuanzia udiwani, ubunge na urais.
Pia amewahimiza wanawake kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura ili siku ya kupiga kura wakachague viongozi wanaofaa.
Kiongozi wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Wananchi (CUF), Anna Rioba anasema uwepo wa wanawake wachache katika nafasi za uamuzi ni athari za kiutamaduni.
“Kusuasua huku ni matokeo ya athari za kiutamaduni kwa kuona wanawake kazi yao ni kulea familia na siasa ni kwa ajili ya wanaume. Kutokana na hilo katika moja ya mikakati yetu ni kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea udiwani, tukiamini huduma nyingi za kijamii zinatolewa huko zikiwemo za shule, afya, maji hivyo itakuwa rahisi kufuatilia utekelezaji wake,” anasema.
Anashauri kuwekwa mazingira rafiki kwa wanawake kugombea, zikiwemo kanuni za uchaguzi.
Crédito: Link de origem