top-news-1350×250-leaderboard-1

Wanandoa wanaodaiwa kuuawa na mtoto wao, kuzikwa kesho Moshi

Moshi. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro likimsaka kijana anayedaiwa kuhusika na mauaji ya wazazi wake (jina linahifadhiwa), familia imeamua kuzika miili hiyo kesho Jumatano, Juni 4, 2025 katika Mtaa wa Kariwa Chini, kata ya Rau, Wilaya ya Moshi.

Wanandoa hao Godfrey Mota (60) na Blandina Ngowi (53), wakazi wa Msufuni, Msaranga wilayani hapa, wanadaiwa kuuawa kikatili usiku wa Mei 29, 2025 na mtoto wao wa kumzaa ambapo baada ya kutekeleza mauaji hayo alitokomea kusikojulikana.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo alisema mauaji ya wanandoa hao yalitokea Mei 29, 2025 ndani ya nyumba ya kupanga waliyokuwa wanaishi familia hiyo eneo la Msufuni.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawasaka waliohusika katika mauaji ya watu wawili ambao ni mke na mume waitwao Godfrey Mota (60), aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye makali shingoni pamoja na mkewe Blandina Ngowi (53) ambaye mwili wake haujakutwa na majeraha, wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Msufini, Kata ya Msaranga, Mei 29, 2025 saa moja na nusu usiku,” alisema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha mauaji hayo na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria na miili ya marehemu ilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi zaidi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Juni 3, 2025 mtoto wa marehemu, Abraham Godfrey amesema familia imepanga kuwazika wazazi wake kesho Juni 4, katika mtaa wa Kariwa Chini uliopo kata ya Rau, Manispaa ya Moshi.

Aidha, amesema miili hiyo itaagwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msaranga Mandaka na baadaye itakwenda kuzikwa katika eneo la Kariwa chini.

Pamoja na mambo mengine, amesema kuhusu ndugu yao huyo ambaye anatuhumiwa na mauaji ya wazazi wao bado wanaendelea kumtafuta ingawa mpaka sasa hawajafanikiwa kumpata.

“Kutokana na kwamba ndugu yetu haonekani kama yupo hai au amekufa au alihusika na tukio tunaomba uchunguzi uendelee kufanyika kwa kina ili tujue ukweli wa tukio hili,” amesema mtoto huyo wa marehemu.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.