Hai. Mamia ya wananchi wakiwamo wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Uduru Makoa, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wameandamana leo Jumatatu Juni 2, 2025 wakishinikiza kuondolewa kwa mwekezaji wa shamba la chama hicho, Elizabeth Stegmaier, kwa madai ya kutonufaika na uwepo wake kwa zaidi ya miaka 26.
Shamba hilo linalomilikiwa na chama hicho cha ushirika limeingia katika mgogoro na mwekezaji huyo kwa madai hawanufaiki na shamba hilo tangu mwaka 2019, alipokodishwa.
Katika kutuliza hali hiyo, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Bomboko alilazimika kutumia lugha ya Kimachame (kichaga) kuwaomba wananchi hao kuwa watulivu, huku akisema suala lao lipo kwenye vyombo vya sheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wananchi hao ambao ni wanachama wa chama hicho, wamesema tangu mwekezaji huyo aingie katika shamba hilo halijawahi kuwanufaisha zaidi ya migogoro ya mara kwa mara.
Judika Massawe, ambaye ni mwanachama wa chama hicho amesema mwekezaji huyo amekuwa akiwasumbua kwa muda mrefu na walitegemea angezalisha ajira nyingi kwa vijana, jambo ambalo halikufanyika.

Baadhi ya wananchi na wanachama wa chama cha Ushirika cha Uduru Makoa, Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali wakishinikiza mwekezaji wa shamba la Ushirika kuondoka. Picha na Janeth Joseph
“Turudishiwe shamba letu, tumepata sana shida hapa na huyu mwekezaji tunataka turudishiwe shamba letu kwa sababu hatuna manufaa nalo na hili shamba lingetupatia ajira nyingi kwa vijana wetu,” amesema Massawe.
Ameongeza; “Tunaomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie aone jinsi tunavyoteseka maana tulitegemea shamba hili litupe ajira kwa vijana wetu, na chama chetu cha msingi cha Makoa kipate fedha, lakini mpaka sasa hatuoni manufaa yake.”
Aidha, amemshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa namna anavyowapambania usiku na mchana kuhakikisha shamba hilo linarudi kwenye ushirika.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Mwenyekiti wa Kijiji cha Uduru, Anzam Mbowe amesema wameamua kuandamana kwa kuwa hawaoni manufaa ya kuwepo kwa mwekezaji huyo.
“Hili shamba limekaa kwa muda mrefu hapa bila mafanikio yoyote kwa wananchi wa eneo hili, likirudi kwa Ushirika ajira zitapatikana kwa wananchi,” amesema Mbowe.
Amesema ni miaka 26 hawajaona chochote kwenye shamba hilo lenye ekari 356 kwa muda mrefu, hawajaona faida ya mwekezaji huo.
Akizungumza na wananchi hao, Mbunge Mafuwe aliwatuliza wananchi hao na kuwaomba wawe watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa kwenye vyombo vya sheria.
Licha ya Mafuwe kuomba utulivu kwa wananchi hao, alilazimika kutumia lugha ya nyumbani (Kimachame) kuwatuliza wakati wakiandamana kwa hasira.
“Tumefika hapa, niwahakikishie hili shamba litarudi mikononi mwenu endeleeni kuwa wapole, tusifanye vurugu yoyote, nawashukuru sana mimi mnikubalie niendelee na hizo hatua nyingine,” amesema Mafuwe.
“Msichoke hapa kuna vita kubwa (Muleshe aghaa foo, yaankwifoo figha fininii, nlazima lukee andukumwi sha wana wa nka, mulesheishigha yenmmuni foo, Mwashimanya roo? ) msichoke, ni lazima tukae pamoja kama watoto wa mwanamke mmoja, mmenielewa ?
Akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko amesema mgogoro huo umefikia katika hatua mbalimbali za utatuzi na sasa uko mbioni kumalizika baada ya hatua za kisheria kukamilika.

Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe akiwatuliza wananchi waliokuwa wanaandamana kutaka mwekezaji wa shamba la Makoa kuondoka.
“Kwa kipindi hiki naomba muwe na utulivu kweli, nimeona wananchi mmekuja na hisia kali na mabango ndio sababu iliyonifanya nije baada ya kupata taarifa kwamba wananchi wamekusanyika wanataka shamba lao, kilichonileta hapa mimi na wenzangu ni taarifa tuliyoipata ya wananchi kutaka kwenda kuchukua shamba lao,” amesema Bomboko.
Alipotafutwa mwekezaji huyo hakutaka kuzungumza chochote kinachoendelea akidai suala hilo lipo kwenye vyombo vya Sheria.
Crédito: Link de origem