top-news-1350×250-leaderboard-1

Waliosoma Veta wahamasishwa kuongeza ujuzi fani za baharini DMI

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Ili kupanua wigo wa ajira na kufanya kazi nchi kavu na baharini wahitimu kutoka vyuo vya Veta wamehamasishwa kujiunga na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).

Wahitimu hao wa Veta ni wale wanaomaliza katika ngazi ya Level Three na ambao wana ufaulu wa kuanzia masomo mawili (D 2) katika mtihani wa kidato cha nne.

Akizungumza Machi 20,2025 kwenye maonesho ya miaka 30 ya Veta yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Mkufunzi kutoka DMI, Kapteni Emmanuel Nanyaro, amesema sekta ya bahari inakua kwa kasi na wanaopita katika chuo hicho wanaweza kufanya kazi duniani kote.

Chuo hicho kinashiriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa umma kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa pamoja na uhusiano uliopo kati ya DMI na Veta.

“Uhusiano uliopo kati ya DMI na Veta ni kwamba watu wa Veta wanaweza kuja kujiunga DMI kwa lengo la kupanua wigo wa ajira, mtu mwenye ‘level three’ ya Veta akija kwetu anaweza kujifunza umeme wa kwenye meli au kuchomelea melini kwa sababu kuchomelea nchi kavu ni tofauti na baharini hivyo, akija kwetu atajifunza kuchomelea melini na umeme wa kwenye meli.

“Atapanua wigo wa ajira kwa sababu atakuwa na uwezo wa kufanya kazi nchi kavu na baharini na atapata kipato kizuri,” amesema Kapteni Nanyaro.

Mkufunzi huyo amesema wapo baadhi ya wanafunzi waliosoma Veta kisha kwenda DMI kusoma elimu ya ubaharia ambapo wengine wanafanya kazi nje ya nchi kama wachomeleaji na mafundi umeme kwenye meli.

“Tunatoa wito kwa vijana wanaosoma Veta wakimaliza wasiishie tu kule waje Chuo cha Bahari wapate elimu ya baharini, wajifunze ufundi mitambo wa baharini wajue injini za meli namna ambavyo zinafanya kazi na kozi nyinginezo,” amesema.

Chuo cha Bahari kilianzishwa kwa Sheria Namba 22 ya Bunge mwaka 1991 kwa lengo la kutoa Elimu na mafunzo ya bahari, kufanya tafiti na ushauri elekezi kwa taasisi za Umma na binafsi.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.