Dar es Salaam. Wafanyabiashara waliokwama China na kufanikiwa kurejea nchini wameeleza hekaheka walizopitia katika kadhia hiyo.
Mei 4,2025 Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo Severine Mushi, alieleza kukwama kwa wafanyabiashara zaidi ya 70 nchini China.
Hii ilikuwa ni baada ya tiketi zao za kurudi Tanzania walizokatiwa na wakala iliyefahamika kwa jina la Jasmini kuonekana hazipo kwenye mfumo wa usafiri wa ndege kupitia shirika la ndege la Tanzania, Air Tanzania.
Mwenyekiti huyo alidai kuwa wakala alichukua pesa za watu zaidi ya Sh300 milioni kwa watu zaidi ya 70 wengine wakiwa wamekata ndege za kampuni nyingine.
Moja ya jitihada walizochukua akiwa nchini humo, Mushi amesema kwa waliowakuta uwanja wa ndege waliwasiliana na ATCL wawakatie tiketi hata kwa bei pungufu licha ya kukutana na changamoto ya nafasi kujaa ambapo wachache tu ndio waliofanikiwa.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio nchini China (DITAG), Alawi Abdallah amesema kwao walipata malalamiko ya wafanyabiashara 14 na tayari wote wameshawasaidia kurejea nyumbani.
Walichoeleza wafanyabiashara
Wakielezea madhila waliyopitia wakati wakiwa China , Chris Kabenga amesema aliingia nchini humo Aprili 15 na alitakiwa kurejea nchini Aprili 27.
Kabenga amesema kwa kuwa amekuwa akijitahidi kuwahi uwanja wa ndege anapokuwa na safari, ilimsaidia kujua kuwepo kwa tatizo hilo mapema na kutafuta namna ya kuondoka kwa kuwa muda wake wa kukaa huko ulikuwa umeshaisha.
“Ndege ilikuwa iondoke Mei 27,2025 saa 6:15 usiku, ila mimi nilifika Mei 26,2025 saa 2:00 usiku na nikawa wa pili katika mstari wa kukaguliwa.
“Baada ya kufika dirishani ndipo nikaambiwa tiketi yangu ilikuwa ya kwenda tu na sio na kurudi hivyo haifai, hii kitu ilinishtua sana kwa kuwa sio kawaida, kwani unaposafiri nchi za kimataifa kisheria lazima uwe na tiketi ya kwenda na kurudi,”amesema mfanyabiashara huyo.
Kutokana na alichoambiwa, Kabenga amesema kwa kuwa alikuwa hana tena hela ya kwenda kulala hoteli wala ya kumuwezesha kupata mahitaji mengine nchini humo, ilibidi amuombe rafiki yake aliyopo Tanzania amkopeshe pesa ili aweze kurejea ambapo ni kati ya waliopata nafasi kwenye ndege ya ATCL japo kwa shida.
Amesema wakati anakwenda kukata tiketi gharama ilikuwa imeshapanda na kufika Sh2.2 milioni wakati kwa Jasmini tiketi ya kwenda na kurudi alishalipia Sh2.6 milioni.
“Hii kwangu ilikuwa ni gharama kubwa kwa kuwa nimejikuta nasafiri kwa takribani Sh6 milioni safari moja fedha ambayo ningeweza kuiingiza kwenye biashara yangu.
“Lakini nilifanya hivyo kuwa kuhofia China kunifungia nisiweze kuingia tena nchini kwao kwa makosa hayo na mimi maisha yangu yanategemea nchi hiyo kwa biashara ninazozifanya,”amesema.
Anita Peter, amesema mume wake aliondoka nchini Aprili 20, na alitarajia kurejea Mei 6,2025 lakini sasa kutokana na tatizo hilo atarejea leo.
Anita amesema baada ya tatizo hilo, mume wake alitaka wachukue fedha dukani kwao wamtumia ili aweze kukata tiketi ya shirika jingine la ndege kwa kuwa ya ATCL waliambiwa imejaa.
Wito wake alitaka watumishi wa ATCL kuwa makini na watu wanaofanya nao kazi, kwa kuwa wafanyabiashara wengi wanapenda kutumia ndege hiyo kwa kujivunia ni ya nchi yao.
“Hata ukiwauliza leo nani wateja wao wakubwa wa ndege yao, watakuambia ni wafanyabiashara wa Kariakoo, hivyo tunaomba wafanyie kazi changamoto zilizojitokeza ili kutoharibu sifa ya shirika,”amesema Anita.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, wakala aliyewakatia tiketi hawakuwa na wasiwasi naye kwa kuwa anajulikana kwa kazi hiyo na wafanyabiashara sokoni hapo, huku akiwa ameanza kukata tiketi kwake tangu mwaka 2015.
Caroline Haule, amesema alipata taarifa ya kuwepo kwa tatizo hilo la tiketi baada ya kukabidhi chumba hotelini alikofikia, na kuwakuta Watanzania wengine wakiwa mapokezi wakijadiliana kuhusu hilo.
Amesema baada ya kusikia taarifa hizo ilibidi ampigie wakala kumwambia itakuwaje na hela hana za kuendelea kuishi huko, ambapo aliahidi kwamba angemtumia hela za matumizi kwa siku ile halafu kesho yake ndipo atamkatia tiketi ya ndege nyingine.
Wakati akimweleza hayo , amesema alikuwa ameenda na rafiki yake ambaye ndio mara ya kwanza kwenda nchini humo, na kumwambia kama anashughulikia hilo ahakikishe anafanya kwa wote kwa kuwa asingeweza kumwacha mwenzake.
“Nashukuru wakala huyo alifanya kama alivyoahidi, alitutumia hela za kutumia, na kesho yake akatutumia tiketi ya ndege ya shirika lingine tukaondoka,”ameelezea Caroline.
Taarifa iliyotolewa Mei 04, 2025 na ATCL ilieleza kuwa abiria hao waliwasilisha malalamiko yao kwao wakieleza wasiwasi juu ya tiketi zao za kurejea kutoka Guangzhou, China.
Hata hivyo baada ya kuarifiwa na wakala huyo kuwa ndege za ATCL hazikuwa na nafasi kwa tarehe walizopanga kurudi, ATCL ilichukua hatua za haraka kufanya uhakiki wa tiketi husika katika mfumo wake na kubaini kuwa majina ya abiria hao hayakuwepo kwenye orodha ya waliopaswa kusafiri kwa tarehe walizotaja.
Aidha ATCL imeeleza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuwa abiria walikatiwa tiketi halali za kwenda Guangzhou na kampuni ya Space Travel, ambayo ilitumia huduma za wakala aliyesajiliwa kwenye mfumo wa “Global Distribution System” (GDS), yaani Satguru Travel & Tour Services (JMD) ambapo iligundulika kuwa Space Travel alihusika kutengeneza tiketi bandia za kurudi.
Kufuatia udanganyifu huo, ATCL imeelekeza kusitisha mara moja uuzaji wa tiketi kupitia wakala huyo kuanzia Aprili 28, 2025 kwa kuwa si miongoni mwa mawakala waliomthibitisha kuuza tiketi zao.
Hatua hiyo inayolenga kulinda usalama na masilahi ya watumiaji wa huduma za usafiri wa anga, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kuchukuliwa.
Crédito: Link de origem