Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani iliyoketi Mbeya imetengua hukumu ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya iliyofuta usajili wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu (Chakumwata).
Mahakama Kuu Mbeya katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Rose Ebrahim Novemba 11, 2023, ilifuta usajili wa Chakumwata, kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa na Msajili wa Jumuiya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mahakama Kuu ilifikia uamuzi huo ikieleza imeridhika na moja ya madai ya Msajili, kuwa aliweza kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa pesa za michango ya wanachama Sh421.49 milioni.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani imetengua uamuzi huo wa Mahakama Kuu, kufuatia rufaa ya Chakumwata, iliyoikata kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, baada ya kuridhika na moja ya sababu za rufaa hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 27, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Winfrida Korosso (kiongozi wa jopo), Panterine Kente na Leila Mgonya, waliosikiliza rufaa hiyo namba 170/2023.
Katika hukumu hiyo, iliyoandikwa na Jaji Korosso kwa niaba ya jopo hilo, baada ya kuridhika, kiapo kilichounga mkono shauri la msingi lililofunguliwa na Msajili na AG, dhidi ya chama hicho, kilikuwa na upungufu wa kisheria.
Katika rufaa hiyo, chama hicho kiliwakilishwa na makamu wa rais mstaafu wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Peter Kibatala, rais wa TLS wa sasa, Boniface Mwabukusi, Luka Ngogo na Isaya Mwanri, kiliwasilisha jumla ya sababu 12.
Hata hivyo, siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, Februari 10, 2025, wakili Kibatala aliomba na akaruhusiwa kuondoa sababu tano za rufaa na kubakiza sababu saba, lakini Mahakama ya Rufani katika hukumu yake imezingatia sababu moja tu.
Sababu hiyo ambayo imetosha kutengua hukumu ya Mahakama Kuu, kwamba Mahakama hiyo ilikosea kuendelea na usikilizwaji mpaka kutoa uamuzi wa shauri msingi licha ya kasoro za kisheria zisizorekebishika za hati ya kiapo kilichounga mkono maombi ya kukifuta chama hicho.
Wakili Kibatala ameieleza Mahakama aya namba 5, 10, 11, 12, 13, 15, 16 na 17 za kiapo hicho kilichoapwa na Msajili wa Jumuiya katika Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Pendo Berege, zina kasoro zinazokifanya kiapo hicho kuwa na upungufu.
Alibainisha kasoro hizo kwa kila aya, ambazo ni pamoja na kuwa na maneno yasiyostahili kuwamo katika kiapo, hoja zinazoibua mabishano na kuweka hitimisho
Hivyo, amedai ulikuwa ni wajibu wa Mahakama Kuu kupima kama shauri hilo lilikuwa linaungwa mkono na nyaraka stahiki na kwamba kwa hiyo haikustahili kuendelea kwa kuitumia kiapo hicho kufanya uamuzi bila kuzungumzia kasoro zilizokuwamo.
Alisema kwa kuzingatia ni msimamo wa kisheria kuwa kiapo kinapokuwa na aya zenye kasoro, aya hizo zinapaswa kuondolewa; na akaiomba Mahamama hiyo kuendelea katika msiamamo huo, kuziondoa aya hizo zenye kasoro alizozibainisha.
Alisema aya hizo zikiondolewa, aya zinazobakia kwenye kiapo hicho hazilisalimishi shauri hilo kwa kuwa zitaifanya hata taarifa ya ukaguzi maalumu iliyokuwa imeambatanishwa katika shauri, ambayo ndio ilikuwa msingi wa uamuzi wa Mahakama Kuu, nayo kuondolewa.
Hivyo, aliiomba Mahakama hiyo kukubali rai ya kutengua hukumu ya Mahakama Kuu na kutupilia mbali amri zake.
Akijibu hoja hizo, Wakili Mkuu wa Serikali, Jesca Shengena alidai shauri hilo linalotokana na masuala ya kikazi.
Alidai kuwa, uamuzi wake haiwezi hauongozwi na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC), kulingana na kanuni ya 24(3) Kanuni za Mahakama ya Kazi Tangazo la Serikali (GN) namba 106/2007.
Alidai kwa namna yoyote ile Mahakama hiyo (ya Rufani) siyo jukwaa sahihi kuibua hoja hiyo ya kasoro ya kiapo na kwamba malalamiko hayo yangeibuliwa na kujadiliwa.
Hata hivyo, Shengena alikiri aya hizo zilizoainishwa na Wakili Kibatala zina shida kwa mujibu wa matakwa ya kisheria kuwepo katika kiapo kinachounga mkono mashauri ya maombi.
Kwa upande wake, wakili wa Serikali Mjahidi Kamugisha alidai kuwa, licha ya dosari za aya hizo, Mahakama itakapoziondoa kwenye kiapo hicho bado kiapo hicho kingeweza kusimama kwa kuwa aya zinazosalia zinaweza kuunga mkono shauri la maombi hayo.
Kamugisha aliiomba Mahakama iione sababu hiyo ya rufaa kuwa haina mashiko.
Lakini Wakili Kibatala alidai kuwa kutokana na wajibu rufani kukubali kasoro hizo kinachobaki bila kupingwa ni kwamba aya zote isipokuwa aya ya tano, zina kasoro na zinazosababisha kiapo hicho kuwa na upungufu, akisisitiza kuwa zinazosalia haziwezi kujenga msingi wa maombi hayo.
Mahakama katika hukumu yake ilieleza kuwa, baada ya kupitia aya hizo ya 10, 11, 12, 13, 15, 16 and 17 za kiapo hicho inakubaliana na Wakili Kibatala maneno yaliyomo ni hoja zenye hitimisho na zinazoibua mjadala.
Ilisema licha ya kudurusu kiapo hicho haikuona maelezo yoyote ya hoja za kisheria, zinazotokana na masuala muhimu yaliyomo kama inavyotakiwa na kwa kiapo kinachounga mkomo maombi katika Mahakama ya Kazi chini ya kanuni ya 24(3) cha Kanuni za Mahakama ya Kazi.
“Katika mazingira hayo, hatutaelezea sana upungufu uliosisitizwa katika aya hizo, ambao kimsingi unamaanisha hapakuwa na ushahidi kuthibitisha tuhuma zilizomo,” inaeleza Rufani.
Ilieleza kuwa, tatizo kama ilivyobainika ni ukweli kwamba kiapo hicho hakistahili kwa kushindwa kutoa maelezo ya masuala ya kisheria yanayoibuka katika mambo muhimu ya kesi, hakikukidhi matakwa ya lazima chini ya kanuni ya 24(3) ya Kanuni za Mahakama ya Kazi.
“Kwa sababu hiyo, tunakubali rufaa na kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu na amri zilizotokana na uamuzi huo, kwa kuzingatia na mazingira ya rufaa hii, hatii amri yoyote kuhusiana na gharama,” inaeleza Mahakama ya Rufani ilihitimisha hukumu yake.
Katika shauri hilo la msingi, shauri la maombi ya kikazi namba 13/2022, waombaji waliiomba Mahakama hiyo kukifutia usajili wake chama hicho kama Chama cha Wafanyakazi.
Katika shauri hilo waombaji walidai kwamba chama hicho kilikuwa kimeshindwa kukidhi matakwa ya usajili kwa mujibu wa Sheria na Kanuni pamoja na Katiba yake na kanuni zake.
Walibainisha madai hayo ya ukiukwaji wa sheria kuwa ni pamoja na kushindwa kuunda na kusajili bodi ya wadhamini, kushindwa kuwa na kudumisha akaunti moja ya benki kwa mujibu wa kanuni za kifedha zinazosimamia Jumuiya kama hizo.
Vilevile walikituhumu chama hicho kwa ubadhirifu wa Sh421,491,532.00 zilizotokana na michango ya wanachama na kwamba chama hicho kina akaunti za benki 33 katika mikoa kadhaa kinyume na kanuni na Katiba yake.
Chama hicho kilikana tuhuma zote hizo, huku kikibainisha kuwa fedha zilizodaiwa kufujwa zilitumika kwa shughuli za kiofisi na wajibu kama vile malipo ya mishahara, posho, gharama za uendeshaji, ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kiofisi, shughuli za mawasiliano, elimu ya soko na bonasi.
Hata hivyo Mahakama Kuu ilikubaliana na waombaji na kukifuta ndipo kikakata rufaa hii.
Crédito: Link de origem
Comments are closed.