top-news-1350×250-leaderboard-1

Walimu wakuu, wapishi wafundwa kutumia nishati safi ya kupikia shuleni

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Walimu wakuu 60 na wapishi katika shule za msingi Halmashauri ya Manispaa Temeke wamejengewa uwezo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuboresha afya zao na wanafunzi pamoja na kulinda mazingira.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Shule ya Msingi Likwati yameandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Ubalozi wa Uingereza, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni Tanzania, Nishati Endelevu kwa Wote (SEforALL) na Serikali ya Tanzania.

Wakizungumza Machi 27,2025 baada ya mafunzo hayo baadhi ya walimu wakuu wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuhama kutoka kutumia kuni na mkaa na kutumia nishati iliyo bora na salama.

“Nishati safi inaokoa muda na inafanya jambo la upishi kuwa jepesi ukizingatia tuko shule tofauti kuna ambao wana watoto 200 wengine 800 kwahiyo, upikaji unakuwa mgumu. Vilevile inaokoa afya za wapishi kwahiyo tuna imani kubwa kupitia mafunzo haya tutaboresha upatikanaji wa lishe, tutaokoa muda, kupunguza utoro shuleni na kuboresha afya za wanafunzi,” amesema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Likwati, Innocent Balasi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umoja, Martina Daudi, amesema; “Tumeonyeshwa majiko ya umeme ambayo yanapika kwa muda mfupi, yanarahisisha kazi na yanalinda afya ya mpishi tofauti na anavyopikia kuni…tutatumia nishati safi na kufanya lishe iwe nzuri shuleni kwetu.

Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Kituye, amesema matumizi ya nishati safi shuleni bado si mazuri kwani kati ya shule 610 zinazotumia gesi ni 37, gesi na kuni ni 22, kuni na mkaa ni 127 na zinazotumia kuni pekee 113 na kuwataka walimu hao kuwa mabalozi wazuri kwa kueneza elimu waliyoipata.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa WFP nchini, Ronald Tran Ba Huy, amesisitiza umuhimu wa kubadili lishe bora shuleni inayotokana na matumizi ya nishati safi.

Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young, amesema moja ya malengo makubwa ya Jumuiya ya Madola ni kuhakikisha kuwa nchi zote wanachama wake zinatunza mazingira.

“Kutunza mazingira kunamaanisha kuweka shule katika hali ya usafi kwa kupanda miti, kutumia nishati safi ambayo husaidia kudumisha usalama wetu wa hewa, ardhi na maji.

“Nishati safi inamaanisha kutumia vifaa maalumu vya kielektroniki ambavyo havitengenezi moshi, vinaweka hewa safi na kutumia nishati kidogo,” amesema Balozi Young.

Mafunzo hayo pia yamehusisha maonesho ya teknolojia mbalimbali za nishati safi yakiwemo majiko ya umeme pamoja na ugawaji wa vitabu vya watoto vinavyozingatia hali ya hewa vilivyotolewa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola.

Mradi huo unalenga kuzifikia shule zaidi ya 500 za sekondari na chache za msingi na kuhakikisha zinatumia nishati safi ya kupikia huku malengo yakiwa kuzifikia shule zaidi ya 1,000 ndani ya miaka mitano.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.