Dar es Salaam. Wakati mauzo ya zao la mwani nje ya Tanzania yakipanda na kushuka, wakulima kutoka Tanga, Kilwa na Zanzibar wamepelekwa nchini Ufilipino kujifunza namna ya kuongeza uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika shughuli zao za kila siku.
Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za hali ya uchumi kila mwezi zinaonyesha katika mwaka ulioishia Aprili 2024 mauzo ya mwani yalikuwa Sh18.73 trilioni ambayo yalishuka hadi Sh9.9 trilioni kipindi kama hicho mwaka huu.
Licha ya kuwapo kwa sababu mbalimbali zinazochangia kupanda na kushuka kwa mauzo hayo ikiwemo mabadiliko ya bei katika soko la dunia na msimu, lakini kupewa mafunzo hayo kunatajwa kuwa moja ya njia itakayoongeza mauzo ya mwani wa Tanzania katika masoko ya nje.
Mwakilishi wa kampuni ya C- Weed Mwani, Rogger Morre ambao ndiyo wanawapeleka wakulima hao amesema wanaamini kufanya hivyo kutachochea kukua kwa uzalishaji.
“Wakirudi watatumika kama walimu kwa wenzao na hii itasaidia kuongeza uzalishaji wa mwani. Hii pia itaisaidia Tanzania kuongeza kiwango cha mwani kinachouzwa katika soko la kimataifa,” amesema.
Amesema wakulima hao watajifunza mbinu mpya za kilimo kwa sababu nchi ya Ufilipino inatumia mbinu za kisasa katika uzalishaji wa zao hilo.
“Pia watajifunza mbinu mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakati wakifanya shughuli zao ili uzalishaji wao usiathirike,” amesema.
Kuhusu uzalishaji, ripoti hii inaonyesha tani 98,000 za mwani ziliuzwa nje katika mwaka ulioishi Aprili 2014 huku zikishuka hadi kufikia tani 65,000 Aprili mwaka huu.
Wakulima hao wameagwa leo Jumatano, Juni 11, 2025 huku wakiwa na matumaini ya kuongeza uzalishaji pindi watakaporejea kutoka katika safari hiyo ya kimasomo.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Halima Abdallah Hassan kutoka Mafia amesema anatarajia kujifunza zaidi katika safari hiyo ikiwemo kujua namna bora ya kupanda zao hilo.
“Kwa sasa tunapanda tu bila kuwa na teknolojia yoyote hivyo nadhani nikisoma naweza kupata mazao mengi tofauti na sasa ninapopata kilo 200 pekee,” amesema Halima.
Kassim Juma Hassan ambaye pia ni mkulima kutoka Pemba amesema anatarajia kujifunza mbinu mpya za uzalishaji zao hilo badala ya kulima kwa mazoea.
“Pia nitajifunza namna ya kutunza bahari wakati nikifanya shughuli hizi, kwani hii ndiyo sehemu pekee ambayo ikiathiriwa kilimo changu kitakuwa kimekwisha,” amesema Hassan.
Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Winfrida Shonde amesema kilichofanyika ni jitihada katika kuendeleza kuinua uchumi wa buluu.
Mkurugenzi wa C-WEED MWANI, Bwana Hamil amesema kwa zaidi ya miaka 30 imekuwa ikiwasaidia wakulima vifaa, mafunzo ya utendaji kazi na shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira, hadi kupata nafasi ya kuwa mabalozi wa mazingira.
“Tutaendelea kutoa kipaumbele kwa wakulima wa mwani Tanzania na kuhakikisha wananufaika na kilimo hicho, huku wakiwasaidia kuanzia upande wa zana bora za kilimo hicho, elimu na utunzaji wa mazingira lengo ni kuhakikisha wanaongeza kipato na kuinua Taifa kwa ujumla kupitia kilimo cha mwani,” amesema.
Crédito: Link de origem