top-news-1350×250-leaderboard-1

Wajumbe kamati tendaji waridhishwa utekelezaji mradi wa SLR mkoani Mbeya

Na Mwandishi Wetu,

KAMATI Tendaji ya Usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri za Wilaya ya Mbarali na Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili (Machi 16, 2025) Mkoani Mbeya wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo kukagua shughuli za utekelezaji wa mradi ikiwa ni juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuhamasisha kuhusu uhifadhi wa mazingira na urejeshwaji wa uoto wa asili nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji, Bi. Rosemary Rwebugisa amesema kamati hiyo imeridhishwa na ushirikiano na juhudi zinazoendelea kufanywa na Ofisi ya Makamu kupitia mradi katika kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kama mbinu mbadala za kuboresha ustawi wa maisha.

“Tumejionea miradi ya utunzaji wa vyanzo vya maji, upandaji miti na miradi ya kuboresha maisha ya jamii kama ufugaji, uchimbaji wa visima na ufugaji wa nyuki na miradi hii kimsingi inalenga kuinufaisha jamii na tumeona mwitikio chanya katika mapokeo yake” amesema Bi. Rwebugisa.

Aidha ameongeza kuwa hatua zilizochukuliwa na mradi kwa kuweka miradi ya kijamii na kiuchumi imejenga mwamko kwa wananchi kwa kuona kuwa mradi ni sehemu muhimu ya maisha yao hivyo kuwapa morali katika kutunza na kuhifandhi mazingira ikiwemo kupanda miti na kutunza uoto wa asili.

Ameongeza kuwa mafanikio ya mradi huo yatawezesha jamii ya wananchi wa Mbarali na Mbeya Vijijini kuwa ni sehemu muhimu ya kuchagiza ajenda ya uhifadhi wa mazingira kupitia fursa za miradi ya uzalishaji mali inayoibuliwa na jamii katika maeneo ya uhifadhi na kuwa kuchochea ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya.

“Wananchi wamehamasika kupitia miradi hii….tumeshuhudia uchimbaji wa visima na ujenzi wa majosho kwa ajili ya mifugo, shughuli ambazo ndio msingi mkuu wa maisha ya kiuchumi kwa wananchi wa vijijini…Tunahimiza miradi hii iendelee kutunzwa ili inufaishe kizazi cha sasa na kijacho” amesema Bi. Rwebugisa.

Aidha ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuziunganisha Wizara za kisekta katika kuunda kamati ya kitaifa ya usimamizi wa mradi huo na kuahidi kuwa Wizara ya Maji itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha malengo ya mradi huo yatafikiwa katika kuimarisha hifadhi endelevu ya mazingira na urejeshwaji wa uoto wa asili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius amesema kupitia mradi huo Ofisi hiyo itaendelea kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wanawake na vijana kuweza kuendesha shughuli endelevu za uhifadhi wa mazingira katika kujiongezea kipato.

“Ziara hiii imeweza kutoa tafsiri ya hali ya uhifadhi wa mazingira ilivyokuwa hapo awali katika jamii za wananchi wa Mbarali na Mbeya Vijijini na sasa tunaona jinsi wanavyoweza kunufaika kupitia fursa mbalimbali ikiwemo uvunaji wa asali ambao umewawezesha kuwaongezea kipato” amesema Dkt. Paul.

Kamati hiyo hiyo ya kitaifa ya Mradi wa SLR ilitembelea jumla ya miradi nane ya uhifadhi wa mazingira ambayo ni mradi wa chanzo cha maji, mradi wa bustani ya miche, mradi wa josho la mifugo, mradi wa maji, mradi wa banio la mifugo, mradi wa uhifadhi wa misitu.

Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji.

Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na unatarajia kukamilika mwaka 2025 na ambapo jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54 zinatarajia kunufaika. Halmashauri hizo ni Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga Vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.