Unguja. Tanzania ikiwa nchi inayohusika na mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na wanawake, imesema kutoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo kunajenga uwazi, uwajibikaji na imani ya kimataifa juu ya kulinda haki za binadamu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema, hatua hiyo itasaidia kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Alisema hayo Machi 28, 2025 katika kikao kazi cha siku tatu cha kupitia rasimu ya taarifa ya nchi ya utekelezaji wa mkataba wa haki za binadamu.
“Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi iliyoridhia mikataba ya haki za binadamu inapaswa kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wake kwa wakati, kwani hatua hiyo itasaidia kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kusaidia waathirika wa ukiukwaji wa haki na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,” amesema.
Amesema endapo wataandaa taarifa yenye kukidhi viwango italeta taswira nzuri hasa katika jumuiya za kimataifa kwani itaonyesha dhamira ya nchi kulinda na kutetea haki za binadamu.
“Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kulinda, kuhifadhi na kukuza haki za binadamu kama zilivyoanzishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo imetaja haki za binadamu kuanzia ibara ya 12 hadi 24 na Katiba ya Zanzibar imeainisha haki hizo kuanzia kifungu cha 11 hadi 25,” amesema.
Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia masuala ya taarifa ya haki za binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Beatrice Mpembo amesema lengo la kikao hicho ni kupitia na kujadili rasimu ya taarifa za nchi juu ya utekelezaji wa mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na itifaki ya haki za wanawake Afrika.
Amesema ushirikiano wa wadau utasaidia kubaini hatua za utekelezaji wa mikataba hiyo, changamoto na kutoa njia bora za kuboresha utekelezaji huo.
Amesema kikao hicho ni muhimu kwani kitatoa fursa ya kupitia na kujadili hatua zilizochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa mkataba huo.
“Utekelezaji wa mkataba huu ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda na kukuza haki za binadamu na haki za wanawake,” amesema.
Amesema mkataba huo unatoa miongozo kwa nchi wanachama kuhakikisha sheria, sera na mikakati inayolenga kulinda na kutetea haki za binadamu.
Pamoja na hayo, amesema kikao kitazingatia maeneo muhimu yakiwemo ya haki za wanawake, usawa wa kijinsia, haki za watoto na haki za makundi maalumu katika kuhakikisha zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa kiwango kinachohitajika.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (Juwauza), Salma Haji Saadati amesema mkataba huo unazungumzia masuala mengi ikiwemo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo wangependa kuona hatua za utekelezaji katika taarifa hiyo.
Amesema upo umuhimu wa kuendelea kusimamia na kutekeleza mkataba huo ili kufikia usawa wa kijinsia unaowalinda wanawake dhidi ya ubaguzi, vurugu na vitendo vya ukatili.
Crédito: Link de origem