Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasaidia wajasiriamali kukua na kuendelea kuwa shindani ili waweze kuzalisha kwa tija wauze kwenye masoko ya ndani na nje.
Akizungumza leo Machi 3,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya wanawake na vijana yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema taasisi hizo zikiwawezesha wajasiriamali wakazalisha kwa tija watauza katika masoko ya ndani na nje.
Amesema hatua hiyo pia itaongeza ajira kwa vijana na kinamama na kupata fedha za kigeni pamoja na kupunguza uingizwaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.
“Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kwamba tuhakikishe sekta binafsi inakuwa ndiyo sekta kiongozi katika kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati, daraja la juu, jumuishi na viwanda. Kote duniani wajasiriamali ndio ambao wanazalisha kwa wingi bidhaa mbalimbali ambazo nyingine ni za mwisho kwa sababu zinakwenda kwa walaji lakini nyingine ni za kati ambazo zinakwenda kwenye viwanda vya juu.

“Ombi langu kwa wajasiriamali tuendelee kutumia fursa nzuri ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara hapa nchini, taasisi zetu ambazo ziko chini ya wizara na zingine za serikali ziwasaidie wajasiriamali kukua, wafanyabiashara kufanikiwa, kuendelea na kuwa shindani ili waweze kuzalisha kwa tija na kwa ubora waweze kuuza kwenye masoko ya ndani na washindane kwenye masoko ya kikanda, Sadc na eneo huru la biashara,” amesema Kigahe.
Ametoa mfano wa baadhi ya bidhaa kama vile mafuta ya kula, mafuta ya kupakaa, sabuni na nyingine ambazo kipindi cha nyuma zilikuwa zinaingizwa kwa wingi kutoka nje hatua iliyolazimu kutumia fedha nyingi za kigeni lakini kwa sasa nyingi zinazalishwa hapa nchini.

“Tunataka tuone fedha zetu za kigeni zikitumika katika kununua bidhaa nyingine ambazo sisi hatuwezi kuzalisha, lengo tuzalishe kwa ubora…mtu mwingine ambaye anaweza kufikiri cha nje ni kizuri zaidi aseme hapana, cha Tanzania kizuri zaidi.
“Tupende bidhaa zetu za ndani, tutakuza uchumi wetu, tutakuza wajasiriamali, tutaondokana na dhana kwamba vijana wanakosa ajira. Ukinunua unawapa ajira na tutawawezesha kuzalisha kwa tija zaidi wawe shindani,” amesema.
Naibu Waziri huyo amewahakikishia wajasiriamali wanawake, vijana na Watanzania wote kwamba Serikali ipo nao bega kwa bega na itahakikisha wanatimiza malengo yao na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.
Aidha ameipongeza TWCC kwa kuandaa maonesho hayo na kuahidi kuwa kama wizara yenye dhamana hawatawaacha nyuma kwa kuwa wanawajali wajasiriamali.
“Tunawathamini sana na tutahakiksha tunawasaidia ili mfanikiwe mzalishe kwa tija zaidi,” amesema Kigahe.
Naye Rais wa TWCC, Mercy Sila, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
“Sisi ni wanawake lakini tuko na vijana, tumefungua dirisha la vijana wavulana wako ili wote kwa pamoja tujenge nchi yetu,” amesema Silla.
Amesema maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo wanatarajia pia kwenda jijini Arusha kushiriki sherehe za kitaifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema maonesho hayo yameshirikisha wajasiriamali 300 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema wajasiriamali wanachangia katika Pato la Taifa, wanachangia kuzalisha ajira na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Crédito: Link de origem