Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza wajumbe watakaoshiriki mchakato wa kuwapigia kura watia nia wa ubunge na udiwani wa viti maalumu kupitia jumuiya zake za vijana (UVCCM), wanawake (UWT) na Wazazi.
Hatua hiyo ni baada ya chama hicho, kufanya marekebisho ya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, uliohusisha upanuzi wa wigo wa idadi ya wajumbe wa vikao vya chama na jumuiya zake watakaopiga kura za maoni.
Uamuzi huo kupanua wigo huo kwa mujibu wa chama hicho, umelenga kuimarisha demokrasia, uwazi na kupanua uwakilishi wa wanachama wa CCM katika kuwapata wagombea wa nafasi za uongozi katika chaguzi za vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumanne Machi 11, 2025 na Katibu wa NEC ya CCM, Oganaizesheni, Issa Gavu, wabunge wa UWT ngazi ya mikoa, kwa upande wa Tanzania Bara watapigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu.
Mkutano huo, utakuwa na wajumbe wote wa mkutano mkuu wa UWT wa mkoa, wajumbe wote wa kamati za utekelezaji wa jumuiya hiyo wilaya na kata.
Kwa upande wa Zanzibar, mkutano mkuu maalumu wa UWT wa Mkoa, utahusisha wajumbe wote wa mkutano huo ngazi ya mkoa, wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa jumuiya hiyo wilaya, jimbo, wadi/kata na matawi.
“Kwa upande wa UVCCM na Wazazi, kura za maoni kwa waombaji ubunge/uwakilishi wa viti maalumu wanawake zitapigwa na wajumbe wa mikutano mikuu maalumu ya taifa,” amesema.
Taarifa hiyo ya Gavu inaeleza kuwa utaratibu wa mkutano huo, utahusisha wajumbe wanawake tu, ambao ni wa mkutano mkuu wa taifa wa UVCCM/wazazi.
Pia, amesema wajumbe wote wanawake wa kamati za utekelezaji za UVCCM/wazazi za mikoa na wilaya.
Crédito: Link de origem