top-news-1350×250-leaderboard-1

Wafugaji wapigia chapuo hati miliki maeneo ya malisho

Simiyu. Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimeiomba Serikali kupanga, kupima na kurasimisha maeneo rasmi ya malisho.

Kimesema kwa kufanya hivyo, kutasaidia kumaliza migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji ambayo mara nyingi husababisha madhara ikiwamo vifo, majeraha na uharibifu wa mali.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Juni 15, 2025 na Katibu wa CCWT, Mathayo Daniel wakati wa kongamano la kitaifa la wafugaji lililofanyika kwenye viwanja vya Nanenane, Nyakabindi wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Katibu Mkuu CCM,Dkt Emanuel Nchimbi akizungumza katika kongamano la wafugaji katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.Picha na Samwel Mwanga



Mathayo amesema licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha sekta ya mifugo, bado upungufu wa maeneo ya malisho na vyanzo vya maji unawalazimu wafugaji kuhama mara kwa mara, jambo linalochochea migogoro isiyokwisha baina ya wakulima na wafugaji.

“Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo Serikali yetu imefanya kwa wafugaji, tunaomba sasa maeneo ya malisho yapimwe na yamilikishwe rasmi kwa wafugaji, pia tuhakikishiwe upatikanaji wa maji ya mifugo. Bila hatua hizo, migogoro itaendelea,” amesema Mathayo.

Amepongeza hatua zilizokwisha kuchukuliwa za ujenzi wa majosho 750 na uchimbaji wa visima vya maji katika baadhi ya maeneo, lakini akasisitiza kuwa, juhudi hizo bado hazitoshelezi mahitaji ya wafugaji wengi nchini.

Kwa upande wake, Maligigwa Maganga, mfugaji kutoka Meatu mkoani Simiyu, amesema umiliki wa maeneo ya malisho utasaidia kuboresha uzalishaji wa bidhaa bora kama nyama na maziwa, hivyo kuimarisha kipato cha wafugaji na kuchangia pato la Taifa.

“Tukipata maeneo ya malisho yenye hati miliki, tutaimarisha ubora wa mazao ya mifugo na kushindana katika soko la ndani na kimataifa,” amesema.

Baadhi ya wafugaji waliohudhuri kongamano la kitaifa la wafugaji katika viwanj vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu.Picha na Samwel Mwanga



Naila ole Nashaki, mfugaji kutoka Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, amesema ni muhimu kwa Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kufanikisha upangaji wa maeneo ya malisho kwa kuzingatia Mpango Kabambe wa Matumizi ya Ardhi wa Taifa (NLUP).

“Maeneo haya yakirasimishwa na kutolewa hati miliki, itasaidia kututambua kisheria na kutuwezesha kupata mikopo kupitia taasisi za fedha,” amesema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashati Kijaji amesema jitihada za kumilikisha maeneo ya malisho ni muhimu kwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeathiri upatikanaji wa malisho na maji, hivyo kusababisha uhamaji wa mara kwa mara wa wafugaji.

Ameeleza kuwa, migogoro hiyo huibuka hasa pale wafugaji wanapolazimika kuingia kwenye mashamba ya wakulima kutafuta malisho au maji kwa mifugo yao, hali inayochochea uhasama mkubwa.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emanuel Nchimbi amesema chama hicho katika Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030, kimeelekeza Serikali kuhakikisha inatenga na kumilikisha maeneo ya malisho kwa wafugaji.

Amesema ilani hiyo inasisitiza mikakati ya kudhibiti migogoro ya ardhi kupitia utayarishaji wa mipaka ya maeneo ya malisho, uwekezaji katika vyanzo vya maji na ununuzi wa mifugo kwa mujibu wa mahitaji.

Waziri wa mifugo na uvuvi,Ashatu Kijaji akizungumza katika kongamano la Wafugaji Kitaifa lililofanyika viwanja vya Nyakabindi mkoa  wa Simiyu.Picha na Samwel Mwanga



Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji imeendelea kushika kasi katika mikoa mbalimbali ikiwamo Simiyu, Tabora, Morogoro na Manyara, hali inayohitaji suluhisho la kudumu.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.