top-news-1350×250-leaderboard-1

Wafugaji kuku wa nyama wafundwa kufuga bila kutumia dawa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wafugaji kuku wa nyama wametakiwa kuepuka matumizi ya dawa za antibayotiki ambayo kwa sasa yamekuwa tishio kwa kuongeza usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwilini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria watu milioni 1.2 hufariki kila mwaka kutokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa huku ikitabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 unaweza kusababisha vifo vya watu milioni 10 kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa mahafali ya wafugaji 30 wa Kata ya Chanika waliopata mafunzo ya ufugaji kuku wa nyama bila kutumia dawa, Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Gibons Kayuni, amesema lengo ni kuepusha usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

“Wafugaji wote wawatumie wataalam ili waweze kufuga ufugaji ulio bora na ambao unazuia matumizi ya dawa kwa mifugo, iwe kwa samaki, kuku au mifugo ya aina nyingine dawa zitumike tu pale inapobidi na ukiona mfugo unaumwa watafute wataalam,” amesema Dk. Kayuni.

Amesema mradi huo umejikita kupunguza matumizi ya dawa kwenye mifugo kwa kuhamasisha wafugaji kutumia chanjo na kuzingatia usafi wa mabanda na vyakula vya mifugo.

Aidha amesema mafunzo yamejikita katika kitoweo cha kuku kwa kuwa ndicho kinacholeta protini haraka kulinganisha na wanyama wengine kama vile ng’ombe na mbuzi ambao wanachelewa kuleta protini.

Amesema walifanya utafiti ambao unaonyesha kama hakutakuwa na jitihada zaidi kutakuwa na upungufu wa protini inayohitajika kwa siku zijazo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, watu wengi wanaoingia kwenye ufugaji hawana elimu hivyo wamekuwa hawazingatii utaalam na kulisha kuku dawa badala ya kuwapa chanjo hali ambayo inachangia kuongeza usugu wa vimelea.

“Mdudu akiota usugu akiwa kwa mnyama ana uwezo wa kuhamishwa kwenda kwa binadamu na ule usugu akauendeleza hivyo, binadamu atakapotibiwa kwa kutumia dawa hatoweza kufanikiwa,” amesema.

Naye Mratibu wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Dk. Elibariki Mwakapeje, amesema binadamu hupata usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa kula mazao ya wanyama au yale ya shambani ambayo yanakuwa na masalia ya dawa zilizotumika kwa mifugo au mazao mbalimbali.

Amesema changamoto ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa husababisha vifo vingi zaidi kulinganisha na magonjwa mengine na kupitia mradi huo wanahimiza ufugaji unaohusisha kinga zaidi kuepusha kuku kuambukizwa magonjwa kwa kuzingatia usafi na kutumia vifaa kinga.

Amesema mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye halmashauri sita nchini ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yalianza Juni 2024 hadi Februari 2025 yanalenga kuongeza uelewa kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa wafugaji kuku wa nyama.

“Tumekuwa tukitekeleza mradi huu wa ufugaji bora wa kuku wa nyama bila kutumia dawa kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa tatizo ambalo limekuwa kubwa hapa nchini na shida kubwa inajitokeza kwenye kuku wa nyama.

“Kuna imani kwamba kuku wa nyama ni lazima afugwe na dawa kwahiyo wafugaji wamekuwa wakiwapa dawa hata pale isipobidi na imeonekana kwamba kuku wa nyama ndio wanalishwa dawa nyingi ndio maana tukaja na mradi huu kuboresha ufugaji wa kuku kutumia mbinu bora za ufugaji ambazo zinamwezesha kuku kukua bila kupata magonjwa hivyo mfugaji anakuwa hawezi kushawishika kutumia dawa,” amesema Dk. Mwakipeje.

Amesema kuku aliyezalishwa kwa kutumia mfumo huo anakuwa na uzito mkubwa wa zaidi ya kilo mbili na kupitia mradi huo wameuzwa kwa zaidi ya Sh 10,000 kwa sababu mnyama asipoumwa anakuwa na nguvu ya kukua na nyama yake inakuwa na ladha nzuri.

Mmoja wa wafugaji wa kuku wa nyama kutoka Kata ya Chanika, Amina Kinyonga, amesema; “Mwanzoni tulikuwa tunafuga kwa kutumia madawa na gharama ilikuwa ni kubwa sana lakini baada ya kupata mafunzo ya kufuga bila kutumia dawa kwa kweli tunashukuru tumeanza kuona faida. Tuko tayari kuwaelimisha wenzetu kufuga bila dawa ili tuweze kupata faida nzuri na kuwa na afya bora.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.