top-news-1350×250-leaderboard-1

Wadau watahadharisha ugawaji majimbo | Mwananchi

Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu mapendekezo ya kugawa majimbo, baadhi wakionya hilo lisifanyike kwa ajili ya masilahi binafsi ya wanasiasa. 

Kwa nyakati tofauti wamesema hayo leo Machi 26, 2025 katika mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukijadili mada isemayo: “Mapendekezo ya ugawaji majimbo ya uchaguzi yana faida au hasara?”

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo amesema ugawaji majimbo unapaswa kuungwa mkono kama unafuata vigezo na sifa zinazotakiwa, lakini upingwe ikiwa unafanyika kwa sababu ya kunufaisha kundi fulani la watu.

Amesema ugawaji majimbo una faida kwa sababu kuna baadhi ya maeneo wananchi hawafikiwi kabisa na huduma yoyote.

“Wanaopinga ugawaji wanapaswa kubadilika na kupaza sauti kwa pamoja ili kuhakikisha gharama zinazotumika kumlipa mbunge zinapunguzwa ili zisaidie kulipa wabunge wapya,” amesema.

Mchambuzi wa siasa, Dk Conrad Masabo amesema ugawaji majimbo ni jambo la kawaida lililoanza tangu mwaka 1961, lakini changamoto ni kama yanagawanywa ili kumfaidisha mtu fulani.

Amesema kuna changamoto, akihoji iwapo Kamati za Ushauri za Mkoa (RCC) zimefikiria gharama za uendeshaji wa majimbo yatakayoongezeka.

Dk Masabo amesema jambo la kujiuliza ni iwapo tupo tayari kugharimia majimbo yatakayoongezeka au ni mahitaji ya wananchi?

Mfanyabiashara Tumaini Patrick, amesema ni wakati wa nchi kuwa na wawakilishi wanaoendana na pato la Taifa, kwa kuangalia namna uzalishaji unavyofanyika na uwakilishi unaowekwa.

Amesema hakuna haja ya kuendelea kuongeza majimbo zaidi, badala yake iangaliwe namna waliopo wanavyoweza kuleta ufanisi.

Amesema ni ngumu kujenga nchi kwa kutumia zaidi ya pato la Taifa linavyokua, huku katika maeneo mengine bado wanafunzi hawana madawati.

Kwa mtazamo wake, mchangiaji wa mjadala huo, Yohana Elirwashinga, kuongeza majimbo kwa ama ongezeko la nafasi za utawala au huduma kwa wananchi, hakuna uhalisia kwa sasa kwani zipo halmashauri hazina watendaji wa kata wala wataalamu wa ugani wa kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema ni muda muafaka wa kuajiri wataalamu wa kada hiyo katika halmashauri ili kuwafikia watu kwenye kata zinazoonekana kuwa kubwa ili kusaidia ukuaji wa uchumi.

“Kata tunaweza kuzigawanya ili kupata watumishi huko, wakiwemo madiwani kwani gharama zao ni ndogo na uwakilishi wao unaanzia chini kuanzia kwenye vikao vya mtaa hadi baraza la madiwani,” amesema.

Mchangiaji mwingine amependekeza majimbo yapunguzwe hadi kufikia 150 ili kuongeza uwajibikaji wa wabunge katika maeneo yao na kuwapa nguvu ya kufanya kazi zaidi.

Hadi sasa, Tanzania ina majimbo ya uchaguzi 264, ambayo Tanzania Bara yapo 214 na Zanzibar 50. Hata hivyo, Bunge lina jumla ya wabunge 393, ambao wa majimbo ni 264, wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais, wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, wabunge 113 wa viti maalumu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

David Kindikwa amependekeza hayo na kueleza: “Ikibidi kama bajeti inahitajika iongezwe ili wabunge waweze kufikia wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuziwasilisha bungeni ili Serikali isikie kero za wananchi na kupeleka utatuzi unaohitajika.”

Mwanahabari, Selemani Msuya amesema kugawa majimbo si suluhisho, bali inapaswa kuangalia waliochaguliwa kama wanajua majukumu yao.

Amesema yapo majimbo mkoani Dar es Salaam yanafikika hata kwa miguu lakini hayana maendeleo.

Msuya amesema kumekuwa na ofisi za serikali za mitaa na kata lakini mambo yameendelea kudumaa, hivyo hakuna haja ya kukimbilia kugawa majimbo.

Amesema ugawaji majimbo umeibua mjadala ndani ya jamii, wananchi wanalalamika kutoshirikishwa hivyo wangepewa nafasi ya kutoa maoni kama kuna haja ya kuyagawa au yabaki vivyo hivyo.

Mwandishi mwandamizi wa siasa wa Mwananchi, Peter Elias, amesema ugawaji wa majimbo unakwenda kuongeza gharama za uendeshaji kwa sababu idadi ya wabunge itaongezeka na kila mmoja anatakiwa kulipwa stahiki zake, ikiwamo posho, marupurupu na kiinua mgongo atakapostaafu.

“Gharama zote hizi zinazoongezeka zinakwenda kwa mlipakodi, zinaongeza mzigo ambao kwa busara za kawaida unaweza kutafuta namna ya kuziepuka,” amesema.

Amesema katika maeneo mbalimbali nchini zipo halmashauri zinazohusika na usimamizi wa maendeleo ya eneo husika na kuhakikisha wananchi wanapewa huduma wanazopaswa kupata.

“Suala la kusema kugawanya majimbo lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi napata ukakasi kwa sababu zipo halmashauri, fedha ambazo zinakwenda kutumika kulipa stahiki za wabunge zingetumika kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia halmashauri zilizopo,” amesema.

Kwa mtazamo wake, ugawaji majimbo umezingatia zaidi masilahi ya wanasiasa kuliko ya wananchi, jambo ambalo linapaswa kubadilika na kuhakikisha mwananchi anapewa namna rahisi ya kuendesha maisha yake.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imehitimisha upokeaji wa mapendekezo ya kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi leo Machi 26, 2025. Ilianza kupokea maoni hayo Februari 26, 2025.

Tayari majimbo tisa yameomba kugawanywa kwa kinachodaiwa kuwa ni ukubwa wake na idadi kubwa ya watu.

Majimbo yaliyopendekezwa kugawanywa na wabunge wake kwenye mabano ni Dodoma (Anthony Mavunde), Mbeya Mjini (Dk Tulia Ackson), Ukonga (Jerry Silaa), Kigoma Vijijini (Vuma Augustine) na Kilindi (Omari Kigua).

Majimbo mengine ni Handeni Vijijini (John Salu), Muheza (Hamis Mwinjuma), Mbeya Vijijini (Oran Njeza) na Mbarali, ambalo kwa sasa linaongozwa na Bahati Ndingo.

Sheria inaelekeza ugawaji wa majimbo kufanyika kila baada ya miaka 10 kama itaonekana kuwa na haja ya kufanya hivyo. Mara ya mwisho, Tume iligawa majimbo mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yaliongezwa.

Akitangaza kuanza kupokea mapendekezo Februari 26, 2025, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alisema vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu, ambao kwa majimbo ya mjini ni kuanzia 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia watu 400,000.

Alisema idadi ya watu itakayotumika ni ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Jaji Mwambegele alivitaja vigezo vingine kuwa ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.