Dar es Salaam. Wakati wimbi la mikopo kausha damu likiendelea kutawala nchini, wadau wa masuala ya uchumi wameshauri jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ikiwemo elimu ya mikopo ili kuwanusuru wananchi wanaoumizwa.
Wadau hao wanatoa ushauri huo kipindi ambacho Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekwishabainisha mwarobaini unaozuia mkopeshaji kuingia kwenye namba za simu za mteja.
Aidha, BoT imeelekeza kampuni zinazokopesha kwenye mtandao ziweke wazi masharti yake na si kuandika ‘vigezo na masharti kuzingatia’ pekee, badala yake kila sharti na kigezo lifahamike kwa mteja kabla ya kukopa.
Uamuzi wa BoT umetokana na agizo la Bunge la kuitaka Serikali kuhakikisha inawabana wakopeshaji wanaotuma ujumbe kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mtu waliyemkopesha kwa lengo la kumdhalilisha.
Suala hilo la mikopo limekuwa likisababisha adha kwa wakopaji wasiokuwa na uelewa hususan kuwa na riba kubwa wakijikuta matatizoni ama kwa kudhalilishwa mitandaoni, mali zao zikiwemo za ndani kuchukuliwa na wengine wakifikia hatua ya kujiua.
Leo Jumatano, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imewakutanisha wadau mbalimbali katika mjadala wa X Space ukiwa na mada inayosema ‘Utitiri wa mikopo umiza ya kidijitali, kausha damu lipi suluhisho la kudumu?
Mwenyekiti wa Mwananchi Saccos Limited, Ephrahim Bahemu amesema mikopo ya kidijitali ni miongoni mwa nguzo muhimu ya fedha na imenufaisha wengi kuliko kuwaumiza. Amesema shida ni mikopo ambayo haidhibitiwi na Serikali na riba zake hazipo sokoni.
Bahemu ambaye pia ni Mhariri wa habari za uchumi wa Mwananchi amesema mikopo isiyodhibitiwa, mtu anakukopesha Sh20,000 asubuhi jioni arudishiwe Sh22,000 hiyo ikiwa ni sawa na riba ya asilimia 10 kwa siku na kwa mwezi riba ya asilimia 300 ambayo haipo.
“Suluhu ya changamoto ya mikopo umiza ni wananchi kupewa elimu kufahamu, hakuna fedha inayopatikana kwa urahisi,” amesema na kuongeza:
“Watu wengi wanaoumizwa na mikopo umiza ni wasio na elimu ya fedha, wana kipato cha chini, sio rahisi kukuta mfanyabiashara mkubwa akiumizwa na mikopo umiza.”
Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema mikopo ya kidijitali imekuja kutatua matatizo japokuwa ilikuwepo toka enzi hata kabla ya kukopeshana fedha, kulikuwa na mikopo ya mifugo na vyakula hadi kufika mikopo ya kifedha.
Amesema uumizaji huo haupo kwenye gharama peke yake ambapo siku hizi watu wengi hawasomi maelezo juu ya mkopo anaotaka kuchukua na imefikia hadi watu kupata ruhusa ya mawasiliano ya mkopaji na kupigiwa baadhi ya watu wake.
“Katika biashara hii kuna gharama inaingiwa ambayo ni hatarishi ambavyo mtu anavikubali hata kuingia kwenye hatari ambayo inaingizwa kwenye gharama ya ule mkopo ambayo kiuhalisia ndiyo inamuumiza mlaji,” amesema.
Adili amesema kwa upande wao wamekuwa wakitoa elimu kuhakikisha walaji wanapata uelewa wa kutosha na ndiyo maana wamepeleka huduma hizo kwenye simu za aina zote, na wanapohitaji mkopo wanafuata taratibu zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Amesema BoT imeweka sheria ya kumuangalia mlaji kuanzia uwekaji wa gharama za mikopo, utoaji wa huduma na hata wanapokwenda kumdai mteja.
Katika maelezo yake, Adili amesema taratibu za kibenki ni chanzo kilichowafanya watu wengi kutoingia kwenye mifumo rasmi ya kuchukua mikopo licha ya kuwa na riba nafuu, kufuata sheria na taratibu zinazomlinda mlaji.
“Watu wengi wanaofanya biashara wanashindwa kuzirasimisha biashara zao, mfano mtu anaweza kuwa na biashara inafanya vizuri iwe ya nguo, chakula au vipodozi lakini akifuatwa kuonyesha rekodi ya manunuzi na uuzaji na faida yake wanakuwa hawana.
“Kutokana na jambo hili inatupa wakati mgumu sisi taasisi za fedha kupata taarifa za kutusaidia ili tuweze kufanya maamuzi ya kifedha na kimahesabu, tunashindwa kumsaidia muhusika,” amesema Stephen.
Amesema njia ya kutatua hili tatizo kuna taasisi za kuwafundisha watu namna ya kurekodi mauzo na fedha zao na wao wamekuwa na taratibu kupitia mfuko wao wa kuwaelimisha watu, na wamekuwa wakijikita kwa wanawake na vijana ambao watakaa kwa muda mrefu katika kujenga uchumi wa nchi.
Mkuu huyo wa idara amesema wafanyabiashara wanatakiwa kutumia lipa namba ili kuhamasisha wateja wao kulipa, wakifanya hivyo baada ya mwaka mmoja hakuna mtu atakayeuliza kama ana kiwanja au nyumba la kuweka dhamani, bali kwa kuangalia hesabu zake watuja anaingiza kiasi gani na kuweza kurejesha na kuingizwa kwenye mfumo ulio rasmi.
Alichokisema Dk Kristomus
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema mikopo ya kidijitali na kausha damu ni tatizo nchini kwa muda mrefu.
Amesema tangu kuruhusiwa kwa huduma za fedha jumuishi na mifumo ya kidijitali kwenye miamala wajanja wengi wametumia fursa hiyo kuanzisha mikopo umiza.
“Sasa hivi utaona baadhi ya wajanja wanaamua kukopesha watu simu na kumekuwa na hamu ya vijana na akina mama kumiliki simu janja na ambazo zina bei kubwa kuliko za kawaida, kwa hiyo wajasirimali wameamua kutumia hiyo kama fursa kwao,” amesema.
“Suluhu la changamoto hiyo ni taasisi za kifedha kutambua mchango kwa kundi la vijana ambao wanaingia kwenye mikopo ya kidijitali. Taasisi hizi zipanue wigo kwa kutoa elimu kwa vijana ili baadaye waje kuwa wateja wao kuliko kuwaacha hivihivi, ni ombi langu kwa taasisi za fedha kuona hili ni tatizo,” amesema Dk Kristomus.
Jambo lingine alilopendekeza Dk Kristomus ni wananchi kutafuta usaidizi wa kisheria kabla ya kusaini mikataba ya mikopo ambayo baadaye huwaumiza.
Mhadhiri huyo amesema kuondokana na tatizo hilo ni viongozi wa serikali za mitaa wawe wanaratibu mafunzo au kuwasaidia wajasiriamali wadogo wanaohangaika ambao taasisi ya fedha kama benki hawawezi kuwakopesha kwa kuanzisha vikundi vya kuwasaidia kwa kutunza pesa baada ya muda waruhusiwe kukopa.
“Tukiwa na vikundi vidogo vikalelewa na serikali za mitaa, wajasiriamali wakatumbukiza pesa zao kama kibubu na panakuwa na mtendaji wa kata au mtaa na kikundi hicho kikafahamika hata baadaye kukiwa na shughuli za kukopeshana wanaweza kufanya hivyo,” amesema.
Amesema kuwepo kwa vikundi kunaweza kusaidia serikali za mtaa kuwasiliana na taasisi za fedha au benki, zikawa zinaandaa mafunzo ili kupanda ngazi kutoka kwenye mikopo midogo na kuwa na kumbukumbu za fedha zao na kuja kuwa na sifa za kukopeshwa na benki.
Pia kwa wananchi ambao wanawaza kukopa simu kuna haja ya kufikiria kudunduliza ili kupata pesa ya halali, kuliko kukopa simu ya Sh150,000 na kudaiwa Sh350,000 ambayo anakwenda kunufaika mkopeshaji Sh200,000, hivyo kuna haja ya kupatiwa elimu ya uanzishaji wa kibubu cha kuweka kidogokidogo.
‘Miezi mitatu kesi 40’
Miongoni mwa washiriki wa mjadala huo alikuwapo mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Tabata Kimanga Darajani jijini Dar es Salaam, Marius Alphonce ambaye amesema wamekuwa wakikemea mikopo ya kausha damu kwa sababu sio rafiki kwa wananchi.
Amesema kwa kipindi cha miezi takriban mitatu alichoingia madarakani Novemba 2024 tayari amesuluhisha kesi zisizopungua 40 baada ya kushindwa masharti ya mikopo waliochukua huku wengine wakifilisiwa na kudaiwa kwa kero.
“Mikopo hii imekuwa rahisi kwa sababu ya upatikanaji wake ndiyo maana wananchi wanaikimbilia, japokuwa kwa uhalisia kampuni au taasisi zinazoitoa masharti yao ni magumu na riba yake ni kubwa na inatakiwa kuanza kulipwa kwa muda mfupi baada ya kukopeshwa,” amesema Alphonce.
Amesema amekaa kikao na wakopeshaji wa mtaani kwake ili kupata suluhisho la kukabiliana na changamoto inayowakuta wakopaji, lakini hawakuweza kufikia muafaka kwa sababu watu hao hawana leseni wala vibali vya kufanya biashara hiyo.
Naye Mdau wa Masuala ya fedha, Jacinta Ngororo amesema Watanzania hawana elimu sahihi ya fedha hivyo wanapopata haraka watu wa kuwakopesha hawafikiri riba wala muda wa rejesho.
Kutokana na hayo, amesema jambo linalohitajika ni elimu watu wafahamu wanachokifanya.
“Suluhu ni nidhamu ya mtu binafsi unapokuwa umeshika fedha unaiwekaje, watu wengi tunaitumia kwanza halafu tunaiweka baadaye lakini ilipaswa kuiweka kwanza halafu ndio uitumie,” amesema.
Njia nyingine aliyoipendekeza kutatua tatizo ni kukaa na watu wenye uelewa wa masuala ya fedha kwani kukaa na wasiokuwa na uelewa kuhusu suala hilo ni kutengeneza nafasi ya kuwa miongoni mwao.
Mbobezi wa masuala ya uchumi, Deogratias Kalulu amesema changamoto za madeni ya kausha damu ni kutokana na watu kukosa njia sahihi ya kupata fedha za haraka.
Amesema taasisi za kifedha mfano benki, zina mlolongo mrefu wa kupata mikopo ikiwemo mkopaji kuambiwa sharti awe na mali isiyohamishika.
Amesema njia ya kutatua tatizo la mikopo kausha damu ni kampuni za simu kuwa na uwezo wa kopesha watu, japo kuna changamoto baadhi yao kutokuwa waaminifu.
“Kwanza wananchi wapewe elimu ya fedha na turahisishe namna ya kupata mikopo ili kuwawezesha kutekeleza shughuli za kiuchumi,” amesema.
‘Serikali iweke mazingira kupata mikopo taasisi rasmi suluhu kausha damu’
Anachokisema Kalulu kinafanana na kile kilichoelezwa na Mjasirimali, Erick Munisi ambaye amesema suluhu ya kudumu ya mikopo kausha damu ni Serikali, kutengeneza mazingira kwa wafanyabiashara na wafanyakazi kupata mikopo kwa urahisi katika taasisi rasmi.
Amesema masharti ya upatikanaji wa mikopo katika taasisi rasmi za kifedha ni magumu jambo linalosababisha wananchi kukimbilia ya kausha damu.
“Mtu anafanya uchaguzi anaona akienda taasisi rasmi hadi kupata mkopo njia ni ngumu sana, mtu akienda benki anaomba mkopo Sh4 milioni anaombwa hati kiwanja au nyumba,” amesema Munisi.
Amesema hata mikopo inayotolewa na Serikali kupita halmashauri ni migumu kwani lazima muhusika awe kwenye kikundi: “Sasa kwenye vikundi nako kuna changamoto, mimi nina wazo langu lakini namna ya kumtafuta mtu wa kuendana na wazo langu au hata akiwa na wazo lake ni mgumu.”
“Serikali itengeneze mazingira ya kuwezesha wajasiriamali, wafanyabiashara na wale walioajiriwa sekta binafsi wapate mikopo kwa njia rahisi,” amesema.
Crédito: Link de origem