Dodoma. Wadau na wabunge wamesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025/30, iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho, imejibu masuala mengi muhimu ambayo Watanzania walikuwa wakingojea kwa hamu, yakiwemo mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
Akizungumza leo, Ijumaa Mei 30, 2025, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kuwa wao kama asasi za kiraia wamekuwa na utaratibu wa kuandaa ajenda za wananchi kila kipindi cha uchaguzi kupitia Ilani ya Asasi za Kiraia na kuzikabidhi kwa vyama vya siasa kabla ya wao kuandaa ilani zao.
“Ilani yetu tuliizindua mwaka jana na tukapeleka wa vyama vya siasa kama ulivyosikia wamekiri (CCM) tangu mwaka jana tumewapelekea Ilani yetu. Lengo ni kwamba vyama vya siasa viende kutengeneza Ilaini zenye ajenda za wananchi na asasi za kiraia,” amesema.
Amesema wakati mwingine wananchi wanashindwa kuzieleza changamoto zao kwa viongozi wanapokuja kwenye kampeni kwa sababu ni muda.
Amesema zaidi ya asilimia 85 ya mapendekezo yao waliyopeleka katika vyama vya siasa yamechukuliwa kwa sehemu kubwa.
“Na kati ya mapendekezo ambayo kwa haraka haraka ni ya msingi na ni kiu ya Watanzania kwa muda mrefu ambayo yalikuwa kwenye ilani yetu namba moja ni Katiba Mpya. Tulieleza kabisa kwenye ilani yetu kwamba tuanzie pale tulipoishia.
“Tukae kama Taifa tujenge sheria mpya ya Katiba baada ya uchaguzi huu. Tukae kama Taifa tujadiliane tunamalizaje mchakato wa Katiba. Hili ni jambo la faraja sana kwamba walau chama ambacho kipo madarakani kimeweka,” amesema Ole Ngurumwa.
Ole Ngurumwa ametaja mambo mengine ni masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.
Amesema anaamini kuwa vyama vingine pia vitachukua Ilani hiyo na kujumuisha katika Ilani zao za uchaguzi ili endapo watashinda watazitekeleza.
Ole Ngurumwa ametaka uwakilishi wa wabunge wa makundi bungeni uongezwe ili yaweze kushirikishwa zaidi na kutoa mfano wa CCM ilivyoweka mwakilishi wa asasi za kiraia bungeni ambaye amekuwa ni kiunganishi kikubwa.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Neema Lugangira amesema asasi za kiraia zimenufaika sana na Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025 ina mambo mengi sana ambayo yanakwenda kutoa majawabu katika kukuza na kuharakisha ustawi na maendeleo ya nchi.
“Nikiwa kama mdau mkubwa wa masuala ya usawa wa kijinsia katika siasa, nimefarijika sana na sehemu ambayo inaongelea masuala ya usawa kijinsia, lakini ile inaongelea masuala ya kudumisha demokrasia,” amesema.
Amesema CCM kinaendelea kujidhihirisha namna ambavyo kitaimarisha mazingira ya ushiriki katika siasa na demokrasia kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Lugangira amesema pamoja na utekelezaji wa sheria ambazo zilipitishwa hivi karibuni bungeni, Sheria za Vyama vya Siasa na Sheria za Uchaguzi, CCM inakwenda kuwa na Sera ya Jinsia pamoja na dawati la jinsia.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema nchi inataka kutengeneza ajira kama ambavyo ilani ya uchaguzi imesema lakini ili kufikia hayo ni lazima kuongeza thamani kwa mazao na bidhaa zinazozalishwa.
“Miaka 7 na 8 iliyopita nikiwa Simiyu (Mkuu wa Mkoa wa Simiyu), tulianzisha kitu kinaitwa district product factory (uzalishaji wa bidhaa katika wilaya) yaani kila tunachokizalisha tulikiongezea thamani hii ni sawa ya hii ya kujenga viwanda kwenye kila maeneo ya uzalishaji,”amesema.
Amesema Ilani ya Uchaguzi kuja na wazo hilo la kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwenye wilaya inakwenda kujibu kila kitu kilichokuwa kikihitajika na watanzania.
“Katika mahala ambapo nchi yetu haitauza kitu ghafi kwenye uzalishaji, tutatengeneza ajira, tukiongeza thamani ajira zinaongezeka toka shambani kwenye viwanda vidogo kwenda sokoni,”amesema Mtaka.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Dk Hamisi Kigwangalla amesema bima ya afya kwa wote ndio baba na mama wa kila kitu kwenye sekta ya afya kwa kuwa inaanisha raslimali fedha za kugharamikia huduma za matibabu zitakapopatikana.
Amesema uwepo wa suala hilo kwenye Ilani ya Uchaguzi unaenda kutatua changamoto za utoaji wa huduma bora za afya kwa watu wote.
“Sasa unapokuwa na nchi ambayo inakua kwa kasi kama yetu ambapo mpaka sasa hivi inakadiriwa kuwa na takribani watu watu milioni 67 hadi milioni 70 hapo lazima uangalie suala la matibabu kwao na Ilani imefanya hivyo,”anasema.
Dk Kigwangalla amesema pia Ilani hiyo imeangalia uwekezaji kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa za kanda na hospitali za kitaifa.
“Na tunahitaji kuendelea kuwa na fedha za kutosha zaidi ili kuongeza idadi ya vituo vya afya na kuongeza idadi ya huduma ambazo zinatolewa na vituo vya afya ambavyo vipo sasa ili tuweze kufikia hilo,”anasema.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Rita Kabati alisema ilani hiyo imegusa mambo mengi ambayo yalikuwa yanakwaza wabunge na watekeleza ilani wote.
“Mimi ni balozi wa wachimbaji wanawake kuna mambo ambayo ambayo ameyazungumzia kwenye mambo ya madini kwanza kabisa wawekezaji ni lazima waingie ubia na wazawa hili ni jambo litakalokwenda kutuinua sana,”amesema.
Amesema kuwa jambo hilo litafanya sasa madini hayatasafirishwa nje ya nchi kama malighafi na hivyo kuongeza kipato kwa wachimbaji na Taifa kwa ujumla.
Mjumbe mwingine Ng’wasi Kamani amesema kwa upande vijana ilani hiyo inakwenda kujibu changamoto zao nyingi.
“Ilani hii ina vipaumbele tisa ambavyo vimeainishwa wazi na vipaumbele hivi vyote kwa umoja wake vinakwenda kuboresha maisha ya Mtanzania lakini kwa kijana kwa kumjengea mazingira bora zaidi ya kujiajiri mwenyewe,”amesema.
Amesema ilani hiyo itatengeneza mazingira bora zaidi ya kuajiriwa au kuwa mtumishi wa umma kwa vijana lakini pia kutengeneza mazingira bora sana kwa sekta binafsi.
Crédito: Link de origem