Dodoma. Vuguvugu la uchaguzi mkuu nchini linaendelea kupamba moto, ambapo vyama 14 vya siasa vya upinzani vimeungana na kuunda jukwaa maalumu kwa lengo la kuwasisitizia Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuwataarifu na kutangaza wagombea watakaoshinda katika Uchaguzi Mkuu unaokuja.
Mbali na hayo, vyama hivyo vimesema kuwa vinaendelea na majadiliano ndani ya vyama vyao kuhusu uwezekano wa kuungana katika uchaguzi huo.
Iwapo vitafikia muafaka itakuwa si mara ya kwanza kwa vyama vya siasa nchini kuunda umoja wakati wa uchaguzi, ambapo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 vyama vinne vya NLD, Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF vilishiriki uchaguzi huo kupitia Ukawa.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, vyama hivyo vilimsimamisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais huku vikigawana majimbo ya kusimamisha wagombea.
Vyama vilivyoko katika jukwaa hilo jipya ni 14 kati ya 18 vilivyosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Vyama hivyo ni ADA-TADEA, DP, NRA, NCCR-Mageuzi, UDP, AAFP, UMD, MAKINI, CUF, NLD, CCK, UPDP, TLP na SAU. Baadhi ya vyama hivyo tayari vimeteua wagombea urais.
Akizungumza leo, Juni 1, 2025, Katibu wa Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir, ameitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutokuwa na hofu wala kusitasita kuwatangaza washindi halali, endapo wataibuka na ushindi katika uchaguzi huo.
“Pamoja na kwamba wananchi ndio wenye ‘mandate’ (mamlaka) ya kumchagua wanayemtaka, niwaombe sana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ZEC sisi kama vyama tumejipanga tukashiriki katika uchaguzi na tutakaposhinda watutangaze katika nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani,” amesema.
Amewataka CCM nao kuridhika matokeo endapo watashinda katika uchaguzi huo na kuwaunga mkono, kama walivyofanya wakati wa uongozi wao.
Naye Katibu Mkuu wa chama cha NRA ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho, Hassan Almasi amewataka Watanzania kutambua kuwa vyama vya siasa hivyo vitamuunga mkono yoyote atakayeshinda katika uchaguzi mkuu kihalali.
“Sisi tutakuwa wa kwanza kupokea matokeo yote yatakayotufanya kuwa washindi ama yoyote atakayetangazwa, hii yote ni kuhakikisha tunabakiza Taifa letu moja baada uchaguzi kwa sababu maisha bado yanaendelea hatuwezi kuwa tatizo katika nchi hii.
“Tutakwenda kuomba ridhaa kwa wananchi kama wanavyoomba wengine na tutagemea kura ya wananchi kwa mujibu wa Katiba. Sisi kwa niaba ya Watanzania wote watulie, wajue kura ina nguvu kubwa zaidi ya risasi,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Abdul Mulya amesema vyama bado vinaendelea na mikutano mikuu ambako pia ajenda ya kuwa na utayari wa kuungana zinajadiliwa.
“Bado tunajadiliana huku ndani, muda bado tunao mrefu baadaye tutakuwa na mkutano wa vyama vyote kujadiliana, na kupokea mawazo ya kila chama ili kuona tunaendaje katika uchaguzi,”amesema Mulya ambaye pia ni Katibu Mkuu wa DP.
Amesema muungano uko wa namna mbili wa siri na ule wa hiari na kuwa zote mbinu za vita watakazotumia kuhakikisha kuwa CCM mara hii kinaondoka madarakani.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo amesema kinachowasukuma kuona kuwa wanaenda kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu na kushinda, ni marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambazo zilikuwa zikilalamikiwa na watu wengi.
“Marekebisho ya sheria za uchaguzi yanatupelekea kwenda kuamini kuwa tunashinda uchaguzi wa mwaka 2025, watu wanajiuliza kuwa chaguzi zilizopita zilikuwa na dosari nyingi za kisheria lakini nataka niwafahamishe Watanzania zimebadilika,”amesema Doyo ambaye chama chake kimemteua kuwa mgombea urais.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Evelyn Munisi amesema wamejipanga na wana nia, dhamira madhubuti ya kuchukua dola na hivyo kubadilisha historia ya Tanzania kwa kuongozwa na chama cha upinzani.
“Tunawaomba Watanzania huko mliko mtupokee, mtusikilize, malalamiko tumeyasikia, mambo yote yanayoendelea tumeyasikia ili kunyamazisha kelele zenu na kuondoa sintofahamu shirikianeni na vyama vya upinzani tuiondoe Serikali madarakani,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha CUF Tanzania Bara, Othaman Dunga amesema kwa wao kushiriki katika uchaguzi ni kuwatendea haki Watanzania na Katiba kwa sababu mamlaka inawekwa na wananchi.
“Tutashindana kwa hoja bila kutukanana, bila kupigana, bila kukashifiana Watanzania watafanya uchaguzi na uwanja wa kuwaweka madarakani ni wao pia,” amesema.
Dunga amesema wanashiriki katika uchaguzi vyama vyote vikiwa sawa bila kuwa na kidogo wala kikubwa na kuwataka kutolinganisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu na ule wa serikali za mitaa wa mwaka jana.
Naye Katibu Mkuu wa chama cha UDP, Saumu Rashid ametaka vyama vya siasa kutoa fursa kwa wagombea wanawake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa wana sifa na vigezo sawa na wale wa kiume.
“Tunawaasa wenzetu kudumisha mazingira ya amani na utulivu kwani yanapotokea machafuko yoyote waathirika wakubwa ni wanawake na watoto. Uchaguzi huu ni wa kihistoria kuna mambo mengi yanaonyesha mwaka huu tutakuwa na mabadiliko,”amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha AAFP, Rashid Rai amesema kuna ujinga mkubwa katika kutafsiri vyama vya siasa vya upinzani ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakisema ni vyama vya mfukoni.
“Kuna kauli kuwa vyama hivi ni chawa, mamluki, mapandikizi, haya ni maneno yaliyozungumzwa kwa miaka mingi lakini nataka kuwaambia kuwa kwa mara ya kwanza kinakwenda kutokea kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2025.
“Hakuna pandikizi, hakuna chawa, hakuna kunguni, kwanza pandikizi maana yake nini sisi tumekuwa mpunga katika majaluba, ama vipande vya mihogo. Kama ni chawa, chawa wa nani maana ni mchafu. Tunaomba mtuamini tunakuja, tunaomba mtuamini,” amesema.
Amesema wamekuwa wakidharauliwa wakifika kwa wananchi na wanaposhindwa katika uchaguzi wanaambiwa kuwa walioshindwa ni mapandikizi.
“Safari hii hakuna pandikizi, chawa, kunguni wala kiroboto tunakwenda kufanya kazi kuhakikisha tunaleta mabadiliko kwenye nchi hii. Watanzania watarajie mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuongozi, kijamii na maendeleo,” amesema.
Amesema kwa mara ya kwanza katika mkutano mkuu wa CCM, uliomalizika hivi karibuni walitaja vyama rafiki ni vya kutoka nje ya nchi na wao walitajwa na Rais Samia Suluhu Hassan kama vyama dada na kaka.
“Tunakubaliana kwamba kwa CCM ni chama kubwa, kaka yetu na dada yetu ni yeye, lakini kwa mara ya kwanza wajiandae na wao kuwa vyama vya upinzani,” amesema.
Crédito: Link de origem