top-news-1350×250-leaderboard-1

Vyakula yenye virutubishi lishe kuukabili udumavu Simiyu

Simiyu. Jamii katika Mkoa wa Simiyu imeshauriwa kuondoa mitazamo potofu kuhusu matumizi ya vyakula na mafuta yenye virutubishi vilivyoongezwa, ili kukabiliana na changamoto za lishe duni.

Ushauri huo umetolewa kutokana na ongezeko kubwa la watoto wenye udumavu mkoani humo.

Pia, wataalamu wa lishe wamesisitiza kuwa matumizi ya vyakula vilivyoimarishwa kwa virutubishi kama vile vitamini na madini, ni njia muhimu ya kuboresha afya ya watoto na wanawake wajawazito, ambao ndiyo kundi lililo hatarini zaidi.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Juni 11,2025 na ofisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya kinga, sehemu ya huduma za lishe, Haliye Abubakary wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Sangamwampuya na Chugamita Wilaya ya Maswa kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kukabiliana na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.

Amesema ukubwa wa tatizo la udumavu katika mkoa huo umeelezwa kuongezeka huku taarifa mpya zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zikionesha kati ya watoto 100 wenye miaka chini ya mitano, 33 wana changamoto hiyo.

Afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya kinga, sehemu ya huduma za lishe, Haliye Abubakary (kulia) akizungumza na baadhi ya wakinamama wa Kijiji cha Sangamwampuya mara baada ya kunywa uji ulioongezwa virutubishi. Picha na Samwel Mwanga

 “Hali ya udumavu katika Mkoa wa Simiyu inazidi kuongezeka kwani takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2016 watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu walikuwa asilimia 32 na idadi imeongezeka kwa mwaka 2024 imefikia asilimia 33.4 na kuacha maswali mengi kwa kuzingatia kwamba mkoa huu ni moja ya mikoa inayozalisha kwa wingi vyakula vya aina mbalimbali,” amesema.

Amesema kuwa, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeanzisha kampeni maalumu kwa kushirikiana na sekta binafsi, hususan Kampuni ya Sancu inayojihusisha na uboreshaji wa lishe, ili kusaidia kufanikisha jitihada hizo.

Ofisa Lishe wa Mkoa wa Simiyu, Dk Chacha Magige, amesema kuwa kuna mitazamo tofauti miongoni mwa wanajamii kuhusu matumizi ya vyakula vilivyoongezewa virutubishi.

Amesema baadhi ya watu wanaelewa umuhimu wake na wanavitumia ipasavyo, lakini bado wapo ambao hawana uelewa wa kutosha na hupinga matumizi yake, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la udumavu kwa watoto.

Magige amesema kuwa mkoa huo umeweka mipango ili kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo ya kuongeza virutubishi kwenye vyakula na hasa katika unga wa mahindi ambao unatumika katika chakula kwenye familia na shule.

“Hali ya udumavu katika Mkoa wa Simiyu iko juu kwani kati ya watoto 100 wapo watoto 33 ambao wanakabiliwa na tatizo la udumavu, ni hali ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa nguvu kubwa ili kuwanusuru watoto hao.

“Na tunasisitiza chakula cha wanafunzi katika shule na familia ni lazima unga wake uongezwe virutubishi na sasa tuna mradi wa kufunga mashine ambazo zitasaidia kuchanganya unga wa mahindi na virutubishi,” amesema.

Amesema kuwa unga ambao umeongezewa virutubishi hauna changamoto zozote za kiafya kama baadhi ya watu wanavyoamini bali zina virutubishi vyote muhimu katika kukabiliana na utapiamlo na udumavu.

Eliamani Mmari, mwakilishi wa Kampuni ya Sancu, amesema kuwa kampuni hiyo imejikita katika kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi kwa lengo la kuimarisha afya ya walaji.

Hata hivyo, amesema kuwa kwa sasa wamebaini ongezeko la changamoto za kiafya kwa watoto wachanga, ikiwemo kuzaliwa wakiwa na matatizo kama mgongo wazi, vichwa vikubwa, na mgongo sungura.

Amesema tatizo hilo limehusishwa na lishe duni kwa akinamama wajawazito, hasa kutotumia vyakula vyenye virutubishi muhimu wakati wa ujauzito.

 Mayombi Emanuel, mkazi wa Kijiji cha Sangamwampuya, amesema kuwa bado kuna baadhi ya watu katika jamii wanaopinga matumizi ya unga wa mahindi ulioongezewa virutubishi, wakidai kuwa unga huo unapunguza nguvu za kiume.

 “Wale ambao hawana elimu wanapingana nayo wakidai watashindwa kuzaa au kupunguza watu lakini wakielimishwa wataelewa tu,” amesema.

Esther Bassu, mkazi wa Kijiji cha Mbugamita mkoani Simiyu, amesema kuwa umasikini wa kipato na ukosefu wa elimu kuhusu lishe bora kwa wazazi, hususan kina mama, ni miongoni mwa sababu zinazochangia udumavu kwa watoto katika maeneo ya vijijini.

Afisa lishe mkoa wa Simiyu, Dk Chacha Magige akieleza hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano katika mkoa huo.Picha na Samwel Mwanga

“Elimu ya lishe bado haijawafikia watu wengi vijijini. Wengi hawajui umuhimu wake, na ndiyo maana watoto wanadumaa kwa kula aina moja ya chakula kila siku. Ili tuweze kuondokana na hali hii, elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa nguvu zote,” amesema Bassu.

Agnes Azami, mkazi wa Kijiji cha Sangamwampuya, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika uzalishaji wa vyakula vyenye virutubishi ili kukabiliana na tatizo la udumavu.

“Kampeni dhidi ya udumavu haziwezi kufanikiwa bila mshikamano wa kweli kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi. Wao ndiyo wana uwezo wa kuzalisha vyakula vyenye virutubishi kwa wingi na kwa bei nafuu,” amesema Azami.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.