top-news-1350×250-leaderboard-1

Vita ulaji vyakula vya asili na vya kisasa janga jipya

Dar es Salaam. Katika miji yenye shughuli nyingi kama Dar es Salaam, Lagos  Nairobi na mingineyo barani Afrika, harufu ya vyakula vya haraka na vilivyosindikwa ( junk foods) inashindana na pengine hata kuzidi harufu ya vyakula vya jadi vinavyopikwa na wauzaji wa mitaani.

Afrika, bara lenye urithi tajiri wa upishi, linashuhudia mabadiliko makubwa ya lishe,  ambayo sasa yanaleta wasiwasi kwa wataalamu wa afya.

Kadri miji inavyoendelea kukua na migahawa ya kimataifa kuingia katika masoko ya ndani, Waafrika wengi wanapendelea vyakula vya haraka na vilivyosindikwa badala ya vyakula vya asili vilivyojaa nafaka, mboga, na protini safi. 

Matokeo yake ni kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kama unene kupita kiasi, kisukari na shinikizo la damu.

Kwa mujibu wa Taarifa za uendeshaji wa huduma za afya nchini (Mtuha), Tanzania ilikuwa na  wagonjwa kisukari 674,399 mwaka 2023.

Ongezeko  vyakula vilivyosindikwa

“Hapo zamani tulikuwa tunakula vyakula vya asili na safi,” anasema Dk Amina Njeri, mtaalamu wa lishe ya afya ya umma jijini Nairobi na kuongeza: “Sasa, kutokana na urahisi na matangazo makali ya kibiashara, watu wengi wanakula vinywaji vya sukari, tambi za haraka, na vitafunwa vya kukaangwa.”

Ni rahisi kuelewa mvuto wa vyakula hivi hasa kwa mwonekano wake wa kuvutia, lakini tafiti zinaonesha kuwa vyakula hivi vimejaa mafuta mabaya, sukari nyingi, na chumvi kupita kiasi, hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa yanayohusiana na mitindo ya maisha.

Watu hawashughulishi miili

Mabadiliko haya ya lishe yanaenda sambamba na kupungua kwa mazoezi ya mwili. 

Katika miji mingi ya Afrika, safari ndefu, kazi za kukaa, na ukosefu wa maeneo ya burudani vinachangia mtindo wa maisha wa kutojishughulisha kimwili.

“Vijijini, watu bado wanatembea umbali mrefu na kufanya kazi za kilimo.Lakini mijini, watu hukaa siku nzima na hutegemea magari hata kwa umbali mfupi, anasema Dk Njeri.

Kwa mujibu wa Profesa Mohamed Janabi  ili kuushughulisha mwili kwa mazoezi mfano ya kutembea, mtu anatakiwa kutembea hatua 10,000 ndani ya saa 24.

‘’ Badala ya watu kutembea, sasa wanapanda pikipiki, bajaji, magari na kushiriki zaidi michezo ya kompyuta wakiwamo watoto.

La kushangaza, wakati baadhi ya watu wanakula vyakula vingi visivyo na afya, wengine bado wanakabiliwa na utapiamlo. 

Hali hii inajulikana kama “mzigo wa mara mbili wa utapiamlo”  ambapo baadhi ya watu katika familia wana uzito kupita kiasi, huku wengine, hasa watoto, wakikosa virutubisho muhimu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa Afrika iko katika hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kuwa sababu kuu ya vifo, ikiipiku ile ya magonjwa ya kuambukiza.

Baadhi ya wanaharakati wa lishe wanahamasisha kurejea  milo ya jadi ya Kiafrika iliyojaa mfano mtama, ulezi, mboga za majani, kunde, na matunda safi.

 Mlo huu si tu kwamba ni bora kiafya, bali pia unasaidia kuhifadhi mazingira.

Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali pia yachukue hii kama changamoto ya kufanya kazi. 

Inatia moyo kuona hapa nchini zipo  kampeni za kuelimisha umma  ili kupunguza matumizi ya sukari na chumvi. 

Kwa nchi kama Afrika Kusini, sheria zinataka kuwe na alama za onyo kwenye bidhaa zenye sukari nyingi.

Kampeni hizi za kuleta mabadiliko ya kurudi tulipotoka, hata hivyo zinahitaji sera madhubuti, utoaji hamasa na elimu kwa umma.

“Tunahitaji kuwekeza katika elimu ya lishe shuleni, kuendeleza kilimo cha ndani, na kuhakikisha vyakula vyenye afya vinapatikana kwa bei nafuu. La sivyo, tutalea kizazi kinachokula sana lakini hakina virutubisho vya kutosha,” anaeleza Dk Njeri.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.