Shinyanga. Vikongwe 138 nchini wameuawa katika kipindi cha mwaka 2024 huku imani za kishirikina zikitajwa kuchochea mauaji hayo.
Kufuatia matukio hayo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Khamis amelaani mauaji hayo huku akisema Serikali haitomfumbia macho atakayebainika kuhusika.
Akizungumza leo Juni 15, 2025 kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee ambayo yamefanyika kitaifa mkoani Shinyanga, Mwanaidi amesema kati ya mauaji ya vikongwe 130 yaliyotokea mwaka jana, matukio 29 ni ya wanaume na wanawake ni 101.
Amesema matukio hayo ni yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi, mwaka 2023. Hata hivyo mauaji ya aina hiyo yalikuwa juu mwaka 2013, ambapo vikongwe 152 waliuawa nchini, kati yao wanawake ni 116 na wanaume ni 36.

“Napenda kutoa wito kwa jamii kuacha kabisa kufanya matendo yanayoashiria ukatili dhidi ya wazee hivyo jamii inapaswa kuwalinda, kuwathamini na kuwahudumia, kila mmoja wetu anapaswa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika mara anapoona viashiria vya ukatili au vitendo vya ukatili dhidi ya wazee ili viweze kushughulikiwa mara moja,” amesema.
Ameitaka jamii kuacha kuamini imani za kishirikina na mali za urithi wa wazazi wao badala yake wafanye kazi ama kujiajiri badala ya kutegemea mali ambazo hawajazichuma jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine limechangia mauaji ya aina hiyo kutokea.
Akizungumzia kupungua kwa matukio ya mauaji ya vikongwe, naibu waziri huyo ametaja utolewaji wa elimu kwa umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, David Sendo amesema waganga wa kienyeji ambao hawajasajiliwa na wanaopiga ramli chonganishi ni miongoni mwa visababishi vya kuendelea kuwepo matukio ya aina hiyo huku akizitaka mamlaka husika kuchukua hatua.
Naye, Mwakilishi wa kikosi kazi cha kupinga ukatili kwa wanawake na watoto Mkoa wa Shinyanga, John Edi amesema mauaji ya wazee yameanza kupungua kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali .
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema baadhi ya vijana hawapendi kujishughulisha na kusubiri kuajiriwa jambo ambalo linasababisha wengine kuingiwa na tamaa na kuanza kudai mali za urithi kwa wazazi wao wakati bado wapo hai.
Crédito: Link de origem