top-news-1350×250-leaderboard-1

Uwekezaji sekta za madini, kilimo watajwa kupaisha uchumi Chunya

Chunya. Uwekezaji wa Serikali katika kuboresha mifumo ya masoko katika sekta ya madini ya dhahabu na kilimo cha tumbaku katika mkoa wa kimadini wa Chunya, umetajwa kuchangia kuufanya mkoa huo kuwa kinara kwa tija ya uzalishaji kwa miaka mitatu mfululizo.

Hatua hiyo imetajwa kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi hususani kuchangia mapato ya Serikali ambayo huelekezwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, Mei 23, 2025, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nkung’ungu kilichopo katika Wilaya ya Chunya, kwenye mkutano wa hadhara baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya mbalimbali ya maendeleo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa ghala la kuhifadhi mazao lenye uwezo wa kuchukua tani milioni moja kwa siku, uliogharimu zaidi ya Sh200 milioni za mapato ya ndani ya halmashauri.

Miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya jengo la mama na mtoto na chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Isangawane kilichopo katika Kata ya Matwiga, uliogharimu Sh300 milioni, kati ya hizo Sh270 milioni kutoka Serikali kuu, sambamba na kukagua mradi wa shule ya sekondari Mayeka.

Awali, Dk Homera ametaja kwa upande wa sekta ya madini ya dhahabu, uzalishaji umeongezeka kutoka kilo 23 mpaka kilo 380 hadi 400 kwa mwezi.

Mbali na uzalishaji huo, bei ya madini ya dhahabu imepaa kutoka Sh70,000 mpaka 285,000, kwa gramu moja katika masoko Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Dk Homera amesema kwa upande wa zao la tumbaku, uzalishaji umeongeza kutoka kilo milioni 8 mpaka kilo milioni 16 – 20, lakini mikakati ni kufikia kilo milioni 30 hadi milioni 50 kwa msimu ujao.

“Mafanikio hayo ni kutokana na uwepo wa kampuni kadhaa za ununuzi na kwamba msimu huu bei ya tumbaku imepaa, kilo moja imeuzwa Dola 3.4 sawa na zaidi ya Sh9,000,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia, kuboresha na kuwekeza masoko ya uhakika ya mazao ya kimkakati hususani zao la tumbaku.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inaboresha na kusogeza huduma kwa wananchi ikiwepo uboreshwaji wa miundombinu ya barabara ili wakulima waweze kusafirisha mazao ya kimkakati.

Hata hivyo, kilio cha wananchi kulalamikia ubovu wa barabara za vijiji vya pembezoni kulimsukuma mkuu huyo wa mkoa kutoa maelekezo.

“Niagize Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kuanza mara moja usajili wa miundombinu ya barabara zote zinazopitisha mazao kutoa maeneo ya pembezoni kufikisha sokoni ili kuleta tija kubwa ya uzalishaji na kumuomba Mbunge wa Lupa kuleta maendeleo,” amesema.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka amesema katika kuunganisha masoko ya sekta ya kilimo, Serikali imefanya mambo makubwa ikiwepo huduma za mawasiliano maeneo yaliyokuwa na changamoto.

Masache amewatahadharisha wananchi kuwa makini katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, watu wanapita huko.

Mkazi wa Kijiji cha Nkung’ungu, Alphonce Joseph amemkumbusha Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka kuboresha miundombinu ya barabara za pembezoni ikiwa ni kumuenzi marehemu baba yake, Njeru Kasaka ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo.

“Masache wananchi tunakupenda na hatuna mashaka na wewe letu moja tu! Tupia jicho barabara za pembezoni kama sehemu ya kumuenzi baba yako, tunashindwa kusafirisha mazao kutoka mashambani kuingiza sokoni,” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.