top-news-1350×250-leaderboard-1

Umeme wa jotoardhi kuunganishwa giridi ya Taifa 2030

Dar es Salaam. Tanzania imelenga kuunganisha nishati ya jotoardhi kwenye gridi ya taifa ifikapo mwaka 2030 ili kuwa na umeme wa uhakika unaotokana na nishati jadidifu.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Dira ya Tanzania 2025 inayosisitiza maendeleo endelevu ya nishati kama nguzo ya mabadiliko ya kiuchumi.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Machi 14, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba katika mjadala wa viongozi wanaoshiriki mkutano wa Kimataifa wa nishati endelevu kwa wote (SEforALL) unaofanyika katika jiji la Bridgetown nchini Barbados.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ndiye ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.

“Lengo letu ni kuunganisha nishati ya jotoardhi kwenye gridi ya taifa ifikapo 2030, suala hili ni miongoni mwa azma yetu pana ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo 2030 ili kuondokana na uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo 2050.

“Hii ni kutokana na Sera ya Taifa ya Nishati ya Tanzania 2015 yenye Mpango Mkuu wa Nishati 2020 pamoja na tamko la Dar es Salaam la “Mission 300” katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa 2025,” amesema Mramba.

Amesema mikoa 16 nchini Tanzania itanufaika na maendeleo ya nishati ya jotoardhi, na kuifanya kuwa msingi wa mkakati wa nishati endelevu.

Naye, Waziri wa Nishati wa Shirikisho la St. Kitts na Nevis, Konris Maynard amesema kuwa nchi zinatakiwa ziwe tayari kukuza matumizi ya jotoardhi na kuhama katika katika matumizi ya nishati zisizo salama kwa mazingira.

Aidha amewataka wadau walioshiriki mkutano huo kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati ya jotoardhi.

Tanzania imebarikiwa kuwa na uwezo mkubwa wa nishati ya jotoardhi, unaokadiriwa kuwa zaidi ya 5,000 MW za umeme na 15,000 MW za nishati ya joto.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.