Dar es Salaam. Wakati ufanisi wa kazi wa Bandari ya Dar es Salaam ukitajwa kuongezeka, wadau mbalimbali wa biashara wamevutiwa kuitumia katika shughuli zao.
Miongoni mwa yanayochochea ufanisi huo ni kupungua kwa muda wa meli za makontena kusubiri kuingia bandarini humo, ambapo Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Machi 10, mwaka huu akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwa sasa ndani ya siku moja au mbili meli inaingia, tofauti na siku saba zilizokuwa awali.
Kampuni zilizovutiwa na ufanisi huo ni China Metal Storage and Transport Company (CMST), Henry Bath & Son Ltd, na Metals & Minerals Africa Trading, ambapo zimetembelea Tanzania kwa mwaliko wa DP World na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kushirikiana katika uwekezaji mwishoni wiki iliyopita.
“Leo tumewakaribisha wawakilishi wa kampuni kubwa tatu za kimataifa zinazoongoza katika biashara ya metali duniani. Lengo kuu ni kutaka waje kuona na kutambua fursa kubwa zilizopo katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuona namna ya kuwekeza au kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Martin Jacob, Mkurugenzi Mtendaji wa DP World Tanzania.
Jacob aliongeza kuwa: “Tuna uhakika kuwa Bandari ya Dar es Salaam itanufaika, na kutakuwa na maboresho katika mnyororo wa usafirishaji—siyo tu ndani ya nchi, bali pia kwa nchi zisizo na bandari zinazoitumia Bandari ya Dar es Salaam.
“Ikumbukwe kuwa awali, kampuni hizi hazikuwahi kuingia kwenye soko la utoaji wa huduma katika bara la Afrika, lakini sasa zinakuja kwa mara ya kwanza kutokana na ushirikiano wa sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ikichagizwa na ufanisi na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika bandari hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Henry Bath & Son Limited, Peter Waszkis, alisema: “Tumekuja hapa kukutana na wadau wakuu na kuangalia njia bora za kuingia kwenye soko hili, hususan katika sekta ya usafirishaji na miundombinu. Tuna hamasa kubwa kuhusu Afrika, na Dar es Salaam iko katika eneo muhimu ndani ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hivyo ni lazima tuwe hapa.”
“Kwa Afrika, hii ni sehemu yetu ya kimkakati inayofuata. Kwa sasa hatuna uwepo wowote barani hapa, lakini tunaangalia Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu,” alisema Wang Haibin, Rais wa CMST.
CMST ni kampuni kubwa duniani katika sekta ya uhifadhi wa madini ya chuma, huku Henry Bath & Son Ltd ikiwa ni miongoni mwa kampuni tano zinazoongoza duniani katika biashara ya chuma, ikiwa na mapato ya zaidi ya dola bilioni 170 kwa mwaka na shughuli zake zikiwa katika mabara matano—isipokuwa Afrika. Sasa, kampuni hiyo inafikiria kuingia katika soko la Afrika.
Crédito: Link de origem