Tano zidisha kwa mbili ni kumi, mbili zidisha kwa tano ni kumi pia. Wakati hamsini gawanya kwa tano ni kumi, na hata mia moja gawanya kwa hamsini ni kumi.
Unaona, kila hesabu tunayopiga jibu lake linarudi kwenye kumi. Ina maana hakuna njia moja ya kuipata kumi, unaweza kukokotoa kwa namna tofauti tofauti na bado jibu likarudi lilelile, kumi.
Itazame kumi kama furaha, itazame kumi kama malengo, itazame kumi kama ajira unayoitamani, itazame kumi kama familia ya ndoto yako, itazame kumi kama kitu chochote unachotamani kukipata hapa duniani. Kisha jiambie kwamba, hakuna njia moja ya kukipata kitu hicho.
Akija mtu mwenye mke na watoto, akakwambia ili kupata furaha duniani inabidi uoe na upate watoto, usimbishie kwa sababu huo ni uzoefu wake, lakini pia usimkubalie haraka kwa sababu hakuna njia moja ya kutafuta kumi.
Hayati John Magufuli, Mungu ailaze roho yake pema peponi alikuwa ni Rais aliyepigiwa kura kama Rais.
Mama Samia amekuwa ni rais kupitia umakamu rais, lakini mwishowe, wote, Samia na Magufuli wamekuwa marais, yaani namaanisha kuna njia nyingi za kuipata kumi.
Ronaldo ameshinda Ballon d’Or nyingi sana, na Messi pia ameshinda Ballon d’Or nyingi, lakini wote wamezipata kutoka katika timu tofauti, Messi akiwa Argentina na Barcelona, Ronaldo akicheza Ureno na Madrid, lakini mwishowe wote wana Ballon d’Or. Yaani namaanisha, hakuna njia moja ya kuipata kumi.
Nilipata kazi Mwananchi kama mwanafunzi niliyetoka chuo kuja kufanya majaribio nikiwa simjui mtu yeyote hapa ndani, lakini kuna wengine wamepata kazi kwa kuanza kama waajiriwa, wengine walitonywa kuhusu nafasi za kazi na rafiki zao, wakatuma maombi ya kazi, wakaitwa, wakafanya interview na mwishowe wakazipata nafasi walizonazo. Bado narudi pale pale, kwenye kutafuta kumi hakuna njia moja.
Kama lengo lako ni kuipata kumi, hakikisha unajifunza njia walizotumia watu wengine kuipata, na hata njia walizotumia watu walioshindwa kuipata, kisha changanya zote hizo na zitumie kujifunza jinsi gani unaweza kubuni njia zako za kuifikia kumi yako.
Wakati unafanya yote haya hakikisha kumi za watu wengine hazikuumizi moyo. Hakikisha kumi za watu wengine hazikupotezi ‘focus’ yako, hakikisha kumi za watu wengine hazikufanyi ujione kama vile wewe si chochote.
Kama ambavyo kuna njia nyingi za kupata kumi. Ndiyo na wewe utaipata kwa njia yako, na kwa muda wako ukifika.
Crédito: Link de origem