Dar es Salaam. Kila mzazi ana matamanio ya kumpata mtoto wa jinsi aipendayo awe wa kike au wa kime na wengi huhoji atafanyaje.
Wataalamu wa afya wametaja mbinu za kisayansi za kupata mtoto wa kike au wa kiume, kwa kutumia kalenda ya hedhi ya mwanamke.
Mtaalamu wa afya ya mama na mtoto kutoka kituo cha Waridi Fertility Solutions kinachojihusisha na afya ya uzazi, Dk Rose Masonda amesema kulenga mtoto wa kiume au wa kike inahitaji uwe na mzunguko wa hedhi unaoeleweka.
Amesema mzunguko unaoeleweka husaidia mama kuwa na ufahamu sahihi wa siku ya yai lake kupevuka.
“Mfano kama mzunguko wako ni wa siku 28, siku ya yai lako kupevuka itakuwa ni ya 14.
“Kama utalenga mtoto wa kiume basi utashiriki hiyo siku ya 13 hadi ya 16 ili mbegu za kiume ziwahi kulifikia yai na kulirutubisha kabla za kike hazijafika,” amesema.
Dk Masonda amesema kama utataka kulenga mtoto wa kike basi wenza watashiriki hasa zaidi siku ya 11 na wakichelewa wafanye ya siku 12.
Amesisitiza kuwa mbegu za kiume hata kama zitawahi basi zitakufa ndani ya saa 48 ambayo ni sawa na siku mbili.
“Kama mbegu zitamwagwa siku ya 11 za kiume zitakufa siku ya 13. Kwa kuwa mbegu za kike zinadumu kwa saa 72 yaani siku3 zenyewe zitakuwa bado zinaishi,” amesema na kuongeza;
“Hivyo kama utashiriki ya 11 na yai lako linapevuka siku ya 14 uhakika wa kubeba mimba ya mtoto wa kike unakuwa ni mkubwa.”
Dk Masonda amesema suala ni kujua yai lako linapevuka lini ni kufanya hesabu.
Sayansi inaeleza kuwa mtoto wa kiume hupatikana kupitia mbegu au ‘chromosomes’ XY na kwamba wa kike hupatikana kupitia mbegu XX.
Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha afya kishiriki cha sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili amesema kisayansi mbegu ya kiume ukilinganisha na mbegu ya kike ya kiume ambayo ni XY ina mbio kali zaidi kuliko ya kike yaani XX.
“Mwanaume hutoa mamilioni ya mbegu kwa mshindo mmoja, lakini mbegu za kiume huwa za kwanza kulifikia yai, lakini zinakufa mapema ukilinganisha na za mtoto wa kike.”
Amesema kama wanandoa wanahitaji kupata mtoto wa kiume ni vizuri akakutana na mwanamke siku moja kabla au siku ambayo yai linapevushwa ili kupata mtoto anayemtaka.
“Wakikutana siku nne au tano kabla yai halijapevushwa asilimia kubwa ni kupata mtoto wa kike. Hivyo muhimu mama ili akamilishe hilo ajue mzunguko wake wa hedhi, kufahamu siku ambayo yai linapevushwa, bila kujua siku kawaida inakuwa siyo rahisi kufanikisha,” amesema.
Dk Mashili amesema uwezekano wa kuwa na mtoto wa kike au wa kiume bado unategemea na namna mfumo wa homoni na mgawanyiko wa mbegu ya mama na baba utakavyokuwa.
“Unaweza kupata wa kike au wa kiume na hupangi wewe ila inategemea, wapo wanaofanya tafiti wanaongelea suala la mlo na muda wa kukutana wenza,” amesema.
Amesema kwenye muunganiko wa mbegu za kiume na yai mwanaume anatoa XY na mwanamke ni XX, mtoto anaweza akachukua X au Y kutoka kwa baba lakini atachukua X peke yake kutoka kwa mama kwa hiyo kama atachukua X kwa baba kwa maana atakuwa mtoto kike na akichukua Y atakuwa wa kiume.
“Ieleweke kwamba anaweza kuchukua Y kwa baba na X kwa mama akapaswa kuwa wa kiume ila akawa wa kike ndiyo maana tunasema kuna uwezekano mkubwa wa kuwa mtoto wa kiume na siyo lazima,” amesema.
Crédito: Link de origem