Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetaja mikakati yake ya kuendelea kuongeza mapato ili kuiwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kwa Watanzania.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema Machi 12, 2025, jijini Dodoma kuwa mamlaka hiyo imefanikiwa kuvuka malengo ya makusanyo kwa asilimia 104% katika kipindi cha miezi nane kuanzia Julai 2024 hadi Februari 2025.
“TRA imekusanya shilingi trilioni 21.20, ikilinganishwa na lengo la trilioni 20.42, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 17 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita,” amesema Mwenda.
Ameeleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la shilingi trilioni 9.28, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 78% tangu mwaka wa fedha 2020/21 kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani.
Kamishna Mwenda ametaja mikakati mbalimbali inayotekelezwa na TRA, ikiwa ni pamoja na:
Kutekeleza maagizo ya Rais Samia kuhusu usimamizi wa kodi nchini. Kuimarisha mifumo ya kodi kwa ndani na forodha, kupitia IDRAS na TANCIS, ili kuongeza ulipaji wa hiari. Kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia elimu kwa umma na kuboresha huduma kwa walipa kodi kwa kutumia teknolojia ili kupunguza usumbufu.
Aidha, TRA imevuka malengo ya kila mwezi kwa miezi minane mfululizo, jambo linalodhihirisha mafanikio ya juhudi za mamlaka hiyo katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
Kamishna Mwenda ameahidi kuendelea kuimarisha mifumo ya kodi na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha TRA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Crédito: Link de origem