top-news-1350×250-leaderboard-1

TLS, mawakili wa Serikali wasaini ushirikiano masuala ya kisheria

Dar es Salaam. Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi amesema Serikali itashirikiana na vyama viwili vya mawakili katika masuala ya kisheria, utatuzi wa migororo, kupeana uzoefu, ujuzi na mafunzo kwa lengo la kusimamia utawala wa sheria na kulinda usalama wa nchi.

Dk Possi amesema, Juni 13, 2025 wakati akishuhudia utiani saini makubaliano ya ushirikiano huo baina ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika ( TLS) na Chama cha Mawakili wa Serikali ( TPBA).

“Sababu ya utiaji saini wa makubaliano haya kati ya TLS na TPBA ni kushirikiana katika nyanja mbalimbali kama kusimamia utawala wa sheria, usalama wa nchi, rasilimali na uchumi, kwa sababu tumeona dunia imebadilika na kuna ukuaji wa teknolojia kama akili bandia na vitu vingine,” amesema Dk Possi.

Maeneo mengine watakayoshirikiana ni uandaaji wa mikataba ya uwekezaji, kuendelea maadili ya mawakili, kufanya kazi kwa karibu na Mahakama na utatuzi wa migogoro nje ya Mahakama.

Pia taasisi hizo zitashirikiana katika kutumia fursa zilizopo katika utengemano, namna bora ya kuisaidia Serikali kwa kutoa ushauri utakaosaidia nchi, kusaidia sekta binafsi katika masuala ya kodi, bima ya afya, mikataba na kukuza taaluma ya wanasheria.

“Nasisitiza tu isiwe hili ni eneo la kwanza, bali tutaendelea kufanya ushirikiano kwa masilahi mapana ya taifa”

Rais wa TLS, Bonifance Mwabukusi amesema ushirikiano huo utakuwa nyenzo muhimu katika masuala ya kisheria na kutatua migogoro ya kisheria.

“Tuna imani kupitia mwanzo huu mpya, itakuwa ni namna bora zaidi ya kuona TLS tunafanya kazi hasa katika maeneo ya msaada wa kisheria, tunaifikiaje jamii kwenye kutoa msaada wa kisheria na masuala ya haki za kibinadamu” amesema.

“Ili wakili aende kuwa mwanasheria wa Serikali, lazima uwe wakili, kwa hiyo nyie nyumbani kwenu ni TLS, huku mlipo ni kazini tu, nyie ni mabalozi wetu”

Amefafanua kuwa nia ya uwepo wanasheria ni kuwepo kwa utawala wa kisheria, haki za binadamu na utawala bora.

“Sheria ndiyo eneo kubwa la kivita kwa sasa, kwa sababu kupitia uwekezaji, kupitia mahusiano ya kimataifa, kupitia mashirikiano ya uamuzi ngazi ya kitaifa, kikanda, sisi wanasheria tuna wajibu mkubwa sana, lakini tukiwa na ukaribu wa pamoja kati ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,  TPBA na TLS, tutajenga imani zaidi na kuona namna bora ya kushirikiana katika mchakato wote ya kisheria inayohusu taifa letu” amesema.

“Ndio maana huwa napenda kusema taaluma yetu sisi ni mabalozi wa Mungu kwa namna kile tunachokifanya kwa umma ambacho ni haki. Kwa hiyo sisi ndio watu tunaomkosea Mungu moja kwa moja, ukiacha kutekeleza majukumu yako dhambi yako ni ya moja kwa moja na ukitekeleza majukumu yako kikamilifu, thawabu yako ni ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu,” anasema na kuongea.

Mwabukusi amesema wanapoungana na kutekeleza uelewa wa moja kwa moja wanatuleta ukaribu na kuondoa mambo ambayo yalikuwa yanatengeneza kujiona kuwa hawawezi kufanya kazi pamoja.

Anasema wakijifunza kwa pamoja, kesi nyingi zinazokwenda mahakamani zitaisha na migogoro mingi ya kisheria itatatuliwa kwa njia ya usuluhishi bila wahusika  kwenda mahakamani.

“Kwa hiyo sisi tunaposaini hivi ni utayari wetu sasa tutashirikiana katika kuhakikisha kuna kuwa na utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria katika taifa letu. Tutakuwa tayari kufanya kazi na Serikali, wadau mbalimbali wa maendeleo ili tujenge taifa letu lenye amani, utulivu na usawa,” amesema.

Makamu wa rais wa TPBA, Wakili Debora Mcharo amesema makubaliano hayo ni muhimu na kwamba yatawanganisha katika masuala ya kisheria na kuongeza weledi.

“Kujenga weledi kwa wanachama na kuleta utulivu katika nchi, kwani tutatumia taaluma yetu kutoa ufafanuzi katika masuala muhimu ya kisheria pale kunapotokea upotoshwaji wa mambo mbalimbali ya kisheria,” amesema Mcharo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.