top-news-1350×250-leaderboard-1

THRDC wapendekeza kuwepo muafaka wa kitaifa kabla ya uchaguzi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umependekeza kuwepo kwa muafaka wa kitaifa kabla ya Uchaguzi Mkuu unaoatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.j

Mtandao huo pia umeainisha masuala 10 ya kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unakuwa huru na wa haki.

Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amewaambia waandishi wa habari leo Aprili 11,2025 kuwa ni muhimu mchakato wa muafaka uanze mapema ili kutoa nafasi ya vyama vya siasa na Watanzania kuelekeza nguvu katika kujiandaa na uchaguzi.

“Tunapendekeza muafaka huu wa kitaifa uyakusanye makundi yote ya kijamii kama viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa na taasisi za kiserikali. Mchakato huu usimamiwe na wazee wenye uzalendo na hekima na wasiokuwa na masilahi yoyote na uchaguzi.

“Tunashauri wadau wote washiriki mchakato huu wakiwa na roho inayoamini katika dhana ya maridhiano…msingi wa muafaka uwe ni kwenye mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika uchaguzi,” amesema Wakili Olengurumwa.

Ameainisha masuala 10 ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi wasiwe watumishi wa Serikali pekee, tabia za maofisa wa uchaguzi kufunga ofisi hasa wagombea wa uchaguzi wanaporudisha fomu, wagombea kutoka vyama vya upinzani kuenguliwa na suala la mawakala kutoapishwa au kuondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.

Masuala mengine ni makosa ya kiuchaguzi kutambulika kama makosa ya jinai, matumizi ya nguvu kutoka vyombo vya dola wakati wa uchaguzi, mapungufu ya sheria na kanuni za uchaguzi, uwazi katika mchakato wa kuandikisha wapigakura na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi pamoja na suala la usalama wa kura na utoaji wa matokeo.

“Tunalishauri Taifa na viongozi wote wa nchi, vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi kuona umuhimu wa kuweka tofauti zetu pembeni na kuwa na muafaka wa kitaifa kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi ujao.

“Tunashauri wanasiasa wote nchini wakati huu wa kuelekea uchaguzi wajitahidi kuchuja aina za matamshi wanayotoa, vyombo vya dola viepuke kwa namna yoyote ile kutumia mamlaka yao vibaya kwa kuingilia uhuru wa vyama vya siasa kufanya siasa hapa nchini,” amesema Olengurumwa.

Mratibu huyo wa Kitaifa THRDC amesema falsafa ya 4R ni wakati wake kutumika ipasavyo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kukiwa na umoja, uhuru, haki na mshikamano.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.