top-news-1350×250-leaderboard-1

TFRA kuchochea uwekezaji viwanda vya mbolea

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetaja mwelekeo wake ni kuhamasisha uwekezaji zaidi katika viwanda vya mbolea ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2030.

Hayo yameelezwa leo Machi 19, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Joel Laurent wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelekea miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita.

Mkurugenzi huyo amesema mwelekeo wa Mamlaka hiyo ni kuimarisha mifumo ya usambazaji wa mbolea, kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.

“Na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika viwanda vya mbolea ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2030,” amesema Laurent.

Amesema katika miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya mbolea nchini imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwa na mafanikio makubwa ambayo yamechangia kuimarika kwa kilimo, biashara ya mbolea, na uwekezaji katika viwanda vya mbolea.

Amesema Mamlaka ya hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko muhimu, huku ikichangia katika kuongeza tija ya kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

“Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kiongozi anayejali maendeleo ya kilimo, ambapo ameendelea kutunga na kutekeleza sera zinazosaidia wakulima na wadau wote wa sekta hiyo,” amesema Mkurugenzi huyo.

Laurent amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, sekta ya mbolea imeshuhudia uboreshaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea ambao umewezesha wakulima kununua mbolea kwa bei nafuu.

“Huku pia wakulima wa mazao mbalimbali wakiendelea kunufaika na ruzuku hii kupitia mfumo wa kidijitali.Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), chini ya Wizara ya Kilimo, imefanikisha mafanikio mengi katika kudhibiti ubora wa mbolea na kuongeza idadi ya aina za mbolea zinazopatikana sokoni,”amesema.

Amesema Kupitia mfumo wa ruzuku ya mbolea, wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu, jambo ambalo limeongeza matumizi ya mbolea na kuchangia ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 19.98 hadi tani milioni 22.8, ongezeko la asilimia 14.

Aidha, sekta ya mbolea pia imeona ongezeko la biashara ya mbolea, ambapo wafanyabiashara waliopata leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020 hadi 7,302 mwaka 2025. Uzalishaji wa mbolea za ndani umeongezeka kwa kiasi kikubwa, na viwanda vya mbolea vimeongezeka kutoka 16 mwaka 2020 hadi kufikia 33 mwaka 2024, huku uwekezaji kutoka nje pia ukiongezeka.

Vilevile, Maabara ya kisasa ya mbolea imeanzishwa, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha ubora wa mbolea zinazozalishwa na kuingizwa nchini.

“Maabara hii pia itatoa huduma kwa nchi za jirani kama Malawi, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” amesema Mkurugenzi huyo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.