Dodoma. Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Geofrey Kiliba ameiomba Serikali kuweka utaratibu mpya wa kulipa ada mara mbili kwa muhula hali itakayosaidia wanafunzi kusajiliwa na kuendelea na masomo kwa urahisi.
Kiliba ametoa maombi hayo leo Juni 14, 2025, wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya Tahliso, yaliyoongozwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Amebainisha kuwa kwa sasa ada hulipwa mara moja kwa muhula katika vyuo vyao, lakini wanapendekeza kuwepo na utaratibu wa kulipa ada mara mbili kwa muhula ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kusajiliwa na kuendelea na masomo kwa urahisi zaidi.
Kiliba amesema wanaamini kuwa kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan changamoto zao zinaweza kutatulika na kuwa na mazingira bora zaidi.
“Napongeza juhudi za kuongeza ‘boom’ kutoka Sh8500 hadi Sh10,000, tunaomba Serikali itusaidie kuhakikisha inaboresha maisha ya wanafunzi nchini kwa kuongeza fedha ya kujikimu kutoka Sh10000 hadi Sh12,000 kwa siku,”amesema.
Mbali na fedha za kujikimu kwa wanafunzi pia, Kiliba ameomba Serikali kuondoa sharti la wanafunzi wa vyuo vya ufundi (Veta) kuvaa sare za shule.
“Tunaomba Serikali iangalie namna itakavyowezesha uwepo wa mafunzo katika wizara mbalimbali pindi wanapomaliza mafunzo,” amesema.
Tahadhari ya siasa za uchochezi
Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi wa vyuo nchini, kutokujihusisha katika siasa zenye misingi ya uchochezi, kubeza na kubagua wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Mbali na hilo, Majaliwa amewaonya kujiepusha na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya Kitanzania.
“Kauli zozote zile ambazo zinakwenda kutugawa nyie wasomi muwe mstari wa kwanza kutafakari na kukemea zisiwe za kuvuruga amani na kuwasambaratisha kwa sababu Serikali ipo imara,” amesema.
Pia, amewataka wasomi hao kuhakikisha kuwa wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi wanatumia mbinu ziitakazoifanya nchi iendelee kuwa salama wakati wote.
Amewataka kutumia busara katika kuchagua viongozi ambao watalisaidia taifa letu kusonga mbele.
“Nimefurahishwa sana na ujumbe wenu kuwa mpo tayari kushiriki uchaguzi huo kwa amani, utulivu na uadilifu, kwa lengo la kuchagua viongozi bora, waadilifu, na wanaotanguliza masilahi ya nchi yetu mbele,”amesema.
Amesema Serikali iko imara na wakati wote itaendelea kusimamia utawala wa sheria, misingi ya kudumisha umoja, mshikamano na amani kama nguzo muhimu za maendeleo.
Majaliwa amewaagiza wanafunzi hao kuzingatia maadili nanidhamu katika taasisi zao.
“Muwe mfano mzuri kwa jamii. Tambueni kuwa Taifa zima linawaangalia ninyi kama kioo cha jamii. Sambamba na masomo hakikisheni mienendo na maadili yenu vinaendana na ustaarabu wa kuelimika kwenu,” amesema.
Pia, amewasihi viongozi kutumia busara na hekima katika kutatua migogoro ya wanafunzi kwa kushirikiana kwa karibu na mamlaka za chuo ili msingi wa uongozi wao ulenge katika kuboresha mazingira ya utoaji wa taaluma.
Amesema wanafunzi wote kuwa na moyo wa kujituma na kujitolea katika jamiii inayowazunguka na kuwa mfano bora.
Pia, amewasitiza na kuwaelekeza wanafunzi wote juu ya kuzingatia matumizi salama ya teknolojia za kidigiti hususani mitandao ya kijamii.
Kadhalika amezitaka taasisi zote za elimu ya kati na juu ambazo hazijaanzisha madawati ya Jinsia zihakikishe hilo ifikapo Julai 30, 2025.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema wizara inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo 2024 ambapo katika utekelezaji wake wamefanikiwa kuhuisha mitalaa na miongozo mbalimbali.
Ametaja miongozo hiyo ni mwongozo wa Taifa wa tuzo na sifa linganifu za kitaaluma, mwongozo wa mafunzo endelevu ya walimu kazini wa mwaka 2020 na mwongozi ya mkakati wa Taifa wa teknolojia ya kidijitali katika elimu.
Kipanga amesema miongozo ya ukaguzi wa vipawa na vipaji wa mwaka 2025, mwongozo wa utekelezaji wa elimu ya amali katika shule za sekondari wa mwaka 2025 pamoja na mwongozo wa mafunzo ya amali kwa wanafunzi wenye mahitaji wa mwaka 2025.
Amesema wameandaa pia mfumo wa kieletroniki wa tathimini ya ujifunzaji kwa lengo la kurahisisha upimaji wa wanafunzi katika shule za msingi.
“Miongozo hii inalenga katika kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini inaziongatia viwango vya kitaifa na kimataifa na kuwajengea wahitimu ujuzi unaohitajika,” amesema.
Amesema pia wizara inaendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali ili ziendane mahitaji ya sasa ya kisekta na kwamba miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kufanya mapitio ya sheria ya elimu ili kuendana na matakwa ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023.
Kipanga amesema maoni mbalimbali ya wadau kuhusu sheria hiyo yanaendelea kukusanya maoni ya rasimu na marekebisho ya Sheria ya Veta.
Marekebisho meninge ni ya Sheria ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea) na Bodi ya Huduma ya Maktaba na Marekebisho ya kifungu cha 58 cha Sheria ya Vyuo Vikuu naKanuni ya 33 ya Kanuni ya Vyuo Vikuu bado yanaendelea.
“Lengo ni kuongeza ufanisi wa taasisi za elimu zitekeleze majukumu kwa kuzingatia muktadha wa sasa wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na zinaendana na mabadiliko ya kikanda na kimataifa,” amesema.
Crédito: Link de origem