Sherehe za sikukuu, mbali na kutoa fursa kwa watoto kucheza na kufurahi, pia ni wakati mzuri wa kutoa mafunzo kuhusu ushirikiano na kusaidiana kati ya wakubwa na wadogo.
Wiki ijayo, watoto wa Zanzibar, kama wenzao wa Bara, wanatarajiwa kumiminika kwenye viwanja kusherehekea Sikukuu ya Idd el-Fitr baada ya kumaliza mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Hata hivyo, hali ya viwanja vya sikukuu imebadilika sana ikilinganishwa na zamani, huku mabadiliko haya yakihusishwa na ukuaji wa teknolojia na uwazi wa kijamii.
Miongoni mwa mabadiliko ni mitindo ya mavazi na watoto kuzurura peke yao bila uangalizi, licha ya kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi yao.
Mabadiliko haya yameathiri si tu mandhari ya viwanja vya sikukuu, bali pia tabia na desturi za watu wa Visiwani.
Hadi miaka ya 1990, viwanja vilijaa watoto jioni, lakini walitakiwa kuondoka kabla ya jua kutua. Usiku ulikuwa ni muda wa watu wazima kutembelea viwanja, tofauti na sasa ambapo watoto wadogo wanachanganyika na watu wazima hata nyakati za usiku.
Zamani, kuanzia saa 8 mchana hadi jioni, watoto waliburudika kwa michezo mbalimbali, kama vile bembea. Vyakula vilivyopatikana vilikuwa vya asili kama mbatata za urojo, bajia, tambi za kukaanga, mishikaki, matunda, biskuti, chokoleti na vinywaji vya asili kama vile sharubati ya ukwaju, machungwa, ndimu, embe na mabungo.
Siku hizi, hata hivyo, vinywaji vya asili vimepungua, nafasi yao ikichukuliwa na soda za chupa na makopo. Aidha, baadhi ya bidhaa kama biskuti na chokoleti zinauzwa zikiwa zimepitwa na muda wa matumizi, hali inayoweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Michezo ya watoto kama vile karagosi na wachekeshaji maarufu, akiwemo “Bape”, sasa imepotea na nafasi yake kuchukuliwa na burudani kama muziki wa disko na ngoma za watu kukata viuno.
Nyimbo zinazochezwa viwanjani mara nyingi zina maudhui ya mahaba, ambazo si sahihi kwa watoto, kwani hazina mafunzo ya tabia njema au kuwahimiza kusikiliza wazazi na walimu.
Wazazi wanapaswa kujiuliza wanawafundisha nini watoto wanaposhuhudia michezo yenye maudhui yasiyofaa, kama vile uongo unaotumiwa kumdanganya mume ili kupata fursa ya kukutana na mpenzi mwingine.
Zamani, vitu vya kuchezea vilikuwa vya kitoto kama mabofu, sanamu za watoto, magari ya plastiki, na bastola bandia za kurusha maji. Siku hizi, bunduki za kuchezea zinafanana na zile halisi zinazotumika vitani, huku pia kukiwa na makombora, roketi, na ndege bandia za kubeba mabomu.
Biashara ya vifaa hivi vya vita haijengi utamaduni mzuri kwa watoto, badala yake inawafanya waone vita na vurugu kama mambo ya kawaida katika maisha, jambo ambalo limechangia matatizo ya matumizi mabaya ya silaha katika mataifa ya Magharibi.
Wahenga walituasa: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Viongozi wa serikali, kwa kushirikiana na wazazi na taasisi za kiraia, wanapaswa kuchunguza kwa kina uuzaji wa silaha bandia kwa watoto katika viwanja vya sikukuu na madukani ili kuepusha athari mbaya za baadaye.
Pia, watoto wadogo hawapaswi kuruhusiwa kuchanganyika na watu wazima nyakati za usiku katika viwanja vya sikukuu. Wazanzibari wanapaswa kutafakari athari za mabadiliko haya na kuhakikisha viwanja vya sikukuu vinarejea kuwa mazingira salama na ya kufurahisha kwa watoto.
Vilevile, ni muhimu kuweka ukaguzi wa bidhaa ili kuzuia uuzaji wa vyakula vilivyopitwa na muda wa matumizi kama biskuti na chokoleti, kwani afya za watoto zinapaswa kupewa kipaumbele kuliko faida ya wachache wanaoingiza bidhaa hizi nchini.
Zaidi ya hayo, mtindo wa kuwavisha watoto mapambo ya dhahabu kama vile vidani, bangili na herini unapaswa kupigwa marufuku, kwani unawafanya kuwa waathirika wa uhalifu kama vile uporaji na wizi.
Sikukuu inapaswa kuleta furaha kwa watoto na wazazi, si kuwa chanzo cha matatizo na hatari.
Crédito: Link de origem