Shirika la Posta laingia mashirikiano na Bahati nasibu ya taifa ili kuongeza huduma ya michezo ya kubahatisha
Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la Posta Tanzania limeingia mashirikiano na Bahati Nasibu ya Tanzania ikiwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa haraka wa huduma za bahati nasibu ya taifa na kuongeza wigo kwa watumiaji wa michezo ya kubahatisha nchini.
Akizungumza mapema hii leo Machi 20, 2025 jijini dar es salam, Mkurugenzi wa Biashara za Kielektroniki na Huduma za Kifedha wa Shirika la Posta Tanzania, Constantine Kasese amesema kupitia upatikanaji wa majukwaa ya bahati nasibu katika ofisi zao, itasaidia kuleta urahisi wa upatikanaji wa tiketi za michezo ya kubahatisha na kuchangia juhudi za taifa za kuwainua wananchi.

Aidha, Kasese amesema kuwa Kwa kutumia miundombinu madhubuti ya Shirika la Posta Tanzania, Bahati Nasibu ya Taifa inalenga kutoa michezo iliyo rafiki, rahisi na yenye uwazi kwa washiriki wote, ikiimarisha dhamira yake ya kuboresha maisha kwa watanzania nchini.
” Tumejikita katika kuwaunganisha watu na huduma muhimu kote nchini. Ushirikiano huu unawiana na maono yetu ya kutoa huduma zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu”. Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ithuba Tanzania, Kelvin Koka amesema dhamira yao ni kuhakikisha kila mtanzania anaweza kushiriki katika michezo ya kubahatisha.
Amesema kupitia mtandao wa Shirika la Posta Tanzania watafanikiwa kuwafikia watu wote nchini na kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki katika michezo ya kubahatisha.
Crédito: Link de origem