top-news-1350×250-leaderboard-1

Sh43 milioni za AHF kuimarisha udhibiti maambukizi ya Ukimwi

Musoma. Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, Healthcare Foundation (AHF), limekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh43 milioni kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Mara.

Msaada huo unaojumuisha pikipiki, kompyuta, printa, simu za mkononi, luninga na vifaa vingine, umetolewa kwa ajili ya kusaidia kazi za uhamasishaji, ufuatiliaji na utoaji huduma kwenye wilaya za Rorya na Tarime.

Akikabidhi vifaa hivyo leo Jumatano Mei 7, 2025 kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya, Meneja Mkazi wa AHF Tanzania, Aika Mtui amesema msaada huo umelenga kuboresha huduma kwenye vituo vya afya vya Utegi na Changuge wilayani Rorya pamoja na Kituo cha Afya Nyangoto kilichopo wilayani Tarime.

“Lengo letu ni kusaidia kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi na kuchochea matokeo chanya kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi. Tunaamini vifaa hivi vitawasaidia wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ikiwemo kuwafikia wagonjwa waliokatisha matibabu na kuhifadhi taarifa muhimu za afya,” amesema Mtui.

Kwa upande wake, Mratibu wa huduma za kudhibiti Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini mkoani Mara, Dk Omari Gamuya amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo na kubainisha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU mkoani humo bado kipo juu.

“Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022/2023, Mkoa wa Mara una kiwango cha maambukizi cha asilimia tano, ambacho kiko juu ya wastani wa kitaifa. Hivyo msaada huu umetolewa wakati muafaka,” amesema Dk Gamuya.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo,  Kusaya amesema msaada huo ni muhimu kwa kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika mapambano ya Ukimwi.

Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa mkoa huo wameitaka Serikali na wadau kuongeza juhudi katika kuzuia maambukizi mapya, wakieleza kuwa kasi ya kampeni za Ukimwi imepungua sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Nakumbuka miaka ya 2000 kulikuwa na kampeni nyingi kupitia vyombo vya habari na mikusanyiko ya watu, lakini sasa hali hiyo haipo tena. Hii ni hatari kwani kuna watu wanaamini Ukimwi haupo,” amesema Yasini Mohamed.

Naye Yasinta Damas amesema kampeni za mara kwa mara zitasaidia vijana kupata uelewa wa namna ya kujikinga na madhara ya Ukimwi, huku John Odhiambo akihoji ukimya uliopo kwa sasa ukilinganisha na harakati za zamani ambazo zilisaidia sana kupunguza maambukizi.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.