top-news-1350×250-leaderboard-1

Sh381 bilioni zakusanywa hatifungani Zanzibar Sukuk

Unguja. Wakati dirisha la awamu ya kwanza likifungwa katika uwekezaji wa hatifungani inayofuata misingi ya Kiislam (Zanzibar Sukuk), zaidi ya Sh381 bilioni zimekusanywa.

Dirisha la kwanza lilifunguliwa Machi 7, 2025 na ilikadiria kukusanya Sh300 bilioni kwa awamu hiyo.

Hayo yamebainika leo Aprili 29, 2025 wakati wa kufungwa kwa dirisha hilo na kukabidhi fedha hizo serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Salum amesema katika awamu ya kwanza ya uwekezaji huo walikadiria kukusanya Sh300 bilioni ni sawa na asilimia 128.33 ya makadirio.

“Zaidi ya watu 400 wamewekeza, kati ya hao wanaume ni asilimia 78 na wanawake 56, taasisi asilimia saba huku taasisi za umma zikiwa 23 na binafsi sita.

Kwa mujibu wa wataalamu, Zanzibar ndio nchi ya kwanza kutoa hatifungani hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali ina mpango wa kuanzisha soko la mitaji la Zanzibar ambalo litachangia katika kupatikana mitaji ya kuwekeza kwenye biashara na miradi mikubwa ya Serikali.

Kulingana na hatua zinazoendelea, Dk Mwinyi amesema Serikali itakuja na kila aina ya mpango wa kuweza kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ikizingatiwa kuwa Zanzibar kuna miradi mingi ya maendeleo inayohitaji kutekelezwa.

 “Zanzibar imekuwa kituo kikubwa cha kujifunza kwa nchi na Serikali zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na taasisi za kifedha juu ya uwekezaji wa hati fungani unaofuata misingi ya sharia,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, tayari wameshaanza kupata maombi kwa baadhi ya nchi kutaka kujifunza na namna gani ya kuliendesha jambo hilo.

Amesema, ni dhahiri kuwa tukio hilo la ufungaji wa dirisha la kwanza la uwekezaji ni uthibitisho kuwa wameweza kufikia malengo waliojiwekea.

Dk Mwinyi amewaambia wawekezaji walioshiriki katika mpango huo wa Sukuk ya Zanzibar kuwa, ni wa miaka saba ambao unategemea uwekezaji wa mali halisi na unaofuata misingi ya sharia.

Amewatoa hofu wawekezaji akisema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mambo kadhaa ambayo ni pamoja na mapato ya kila mwaka kwa wawekezaji yatalipwa kwa wakati.

“Kiasi chote cha mtaji kilichowekezwa kitalipwa kwa ukiamilifu baada ya miaka saba kwa wakati uliopangwa,” amesema Dk Mwinyi.

Fedha hizo zilizopatikana zitapelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya miundombinu ya barabara Unguja na Pemba, Bandari Jumuishi ya Mangapwani, kituo cha matibabu ya saratani ya Binguni na kumalizia kazi ya ujenzi wa Terminal II ya Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman Karume.

Amesema, kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza fursa za kuimarisha maisha ya wananchi, utoaji wa huduma bora za kijamii na kukuza uchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza kwa niaba ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Katibu Mkuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii Tanzania, Meshack Bandawe alipongeza Serikali kwa kuwapa fursa ya kuwekeza kupitia Sukuk akisema ni moja ya maeneo salama kwa uwekezaji.

Amesema uwekezaji huo una manufaa makubwa kwani unakwenda kuongeza nguvu za kuboresha miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii kwa Zanzibar.

“Naamini uwekezaji huu unakwenda kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na miundombinu yake na kuongeza ustahamilivu wa mifuko ya hifadhi na kuitunisha kwa ajili ya kuboresha mafao ya wanachama wake,” amesema.

Awali akitoa taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi Mtendaji Zanzibar Treasury Sukuk 1 Limited (SPV), Dk Masoud Rashid Mohammed, amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza utoaji wa Sukuk ya kwanza ya Serikali.

Amesema Zanzibar imeweka historia sio tu kwa kufunga awamu ya kwanza ya uwekezaji wa Sukuk na kukabidihi fedha kwa Serikali, bali pia kusherehekea hatua kubwa za mabadiliko katika safari ya kuimarisha mbinu mbadala za fedha za maendeleo jumuishi na uwajibikaji wa misingi ya sharia.

“Program hii ya Sukuk hiyo inaashiria sio tu ufanisi wa kifedha bali pia uaminifu wa wananchi na uadilifu katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inafanywa na serikali,” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.