Tabora. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeingia mkataba na mkandarasi mzawa wa Kampuni ya Samota Limited kujenga mradi wa skimu ya umwagiliaji wa Mwamapuli, Kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga Mkoa wa Tabora wenye thamani ya Sh26.9 bilioni.
Mkataba huo umeingiwa leo Jumatano, Juni 4, 2025 katika hafla iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha na utatekelezwa kwa miaka miwili.
Mradi huo unalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 630 hadi kufikia 2,397 huku zaidi ya wakulima 2,470 wakitarajiwa kunufaika kutokana na mradi huo.
Chacha amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa ufanisi na kwa muda wa makubaliano na kuzingatia uhitaji wa wananchi.
“Serikali ina nia njema, lengo ni mradi umalizike kwa wakati ili uweze kuanza kuwanufaisha wananchi,” amesema.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, mhandisi wa umwagiliaji Mkoa wa Tabora, Francis Mgangalula amesema utekelezaji huo utahusisha shughuli mbalimbali ikiwamo ujenzi wa barabara za shambani, ujenzi wa ofisi ya Tume, nyumba ya meneja wa skimu na ununuzi wa gari moja kwa ajili ya usimamizi wa mradi.
“Mradi huu ni mkubwa ambao Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wake, niwasihi wananchi baada ya kukamilika, tuutunze kwa ajili ya kilimo endelevu,” amesema.

Mwakilishi kutoka Kampuni ya Samota Limited, Ahmed Salumu ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na ubora unaotakiwa kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Crédito: Link de origem