Hanang’. Watu 4,995 wa Kata ya Hidet, wilayani Hanang’ mkoani Manyara, watanufaika na mradi wa maji kutoka Ziwa Bassotughang baada ya kujengwa kwa mitambo ya kusafisha kwa matumizi ya binadamu.
Kujengwa kwa mradi huo kunaenda kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo hilo.
Baadhi ya wakazi wa Hidet, wakizungumza baada ya kuwekwa kwa jiwe la msingi la mradi huo leo Jumatatu Machi 24, 2025, wameeleza changamoto walizokumbana nazo kabla ya mradi huo kuanzishwa.
Julius Saktai, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amesema wanawake walikuwa wakihangaika kutafuta maji, lakini kupitia mradi huo changamoto hiyo itakuwa historia.

“Kwa kweli tunamshukuru mbunge wetu, Samwel Hhayuma, ambaye amejitahidi kuhakikisha mradi huu wa maji wa Bassotughang unatekelezwa,” amesema Saktai.
Amesema awali walikuwa wakitumia maji ya bwawa la Bassotughang, lakini baadaye ilishindikana kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu sahihi ya kusambaza maji kwa wakazi.
Mbunge wa Hanang, Samwel Hhayuma ameipongeza Serikali kwa kuwekeza kwenye mradi huo na kusaidia wakazi wa kijiji hicho kupata huduma bora ya maji safi na salama.
Amesema mradi huo ulisuasua kwa muda mrefu hatimaye mwaka huu umekamilika.
“Kuna wazee niliowaambia kuwa mradi huu wa maji wa Bassotughang utafanikiwa, lakini waliniambia sitaweza sasa wamekuja kunipongeza baada ya kuona utekelezaji wake,” amesema Hhayuma.
Aidha, amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kuwa na subira hadi kufanikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Hanang, Herbet Kijazi amesema mradi huo umegharimu Sh1.5 bilioni, fedha kutoka Serikali kuu.
Kijazi amesema mradi huo wa maji wa Bassotughang utawanufaisha wakazi 4,995 wa Kata ya Hidet.
Crédito: Link de origem