Na Malima Lubasha, Serengeti
Kampuni ya Beyond Wild Impact, inayofanya shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, imesaini makubaliano na uongozi wa Kamati ya Shule ya Msingi Mbirikiri kutoa dola 50,000 sawa na Sh 127 milioni kuboresha miundombinu ya shule hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kushindwa kuikamilisha.
Makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo yamefanyika hivi karibuni katika shule hiyo kati ya mwalimu mkuu Hamisi Mega na mwakilishi wa kampuni hiyo Meneja MacDonald Mlemwa ambapo ujenzi unatarajia kuanza mwezi huu kwa mujibu wa makubaliano.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa matundu 10 ya vyoo vya wanafunzi, ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya mwalimu mkuu na kukarabati madarasa matatu.
Akizungumza wakati wa kuingia makubaliano hayo, Mlemwa amesema hiyo ni mara ya pili kusaidia kuboresha miundombinu ya shule hiyo ukiwa ni mchango wa kampuni kusaidia vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Serengeti.
“ Mara ya kwanza tumesaidia kujenga matundu 10 ya vyoo,kujenga madarasa mawili, ,kukarabati darasa moja lililojengwa na Tasaf na ofisi ya walimu na kuendelea kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori,” amesema.
Amesema mbali na kusaidia kuboresha miundombinu hiyo, pia wametoa msaada wa kujenga zahanati kijijini hapo ili wananchi waweze kupata huduma za afya karibu na kutoa msaada wa madawati na kufadhili safari za walimu na wanafunzi kutembelea vivutio vya utalii ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“ Tumefanya makubaliano hayo kati ya kampuni na kamati ya shule kufuatia maombi yaliyotumwa na mwalimu mkuu wa shule nasi kama taasisi binasfi tulikaa na kukubaliana kusaidia sekta ya elimu katika kijiji ambao ni marafiki wa uhifadhi,” amesema Mlemwa.
Aidha Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mega amesema shule ina wanafunzi 570, walimu nane ikiwa na upungufu wa walimu sita, upungufu wa nyumba vya madarasa nane na kufafanua kuwa uongozi na kamati ya shule wanafanya jitihada mbalimbali kutafuta wadau ili kupunguza changamoto ya miundombinu.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbirikiri, Thomas Mgaya amesema Halmashauri yake ya kijiji kwa kushirikiana na kamati ya shule watahakikisha wanasimamia mafanikio yanayopatikana hapo shuleni kuunga mkono jitihada zinazoletwa na mkuu wa shule akisaidiana na walimu wake na kuomba wadau wa elimu ndani ya hifadhi ya Serengeti kusaidia kijiji hicho hasa katika sekta za elimu, afya na maji.
Crédito: Link de origem