Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema wamechukua hatua kuhakikisha wanakuza uandishi bunifu ili kudhibiti uingizwaji wa vitabu visivyo na maadili shuleni.
Hatua hizo ni pamoja na kukuza sekta ya uchapaji, kuongeza hifadhi ya vitabu katika maktaba ya taifa na kukuza utamaduni wa kujisomea kwa kutangaza kazi ambazo zimefanyika ili kuhifadhi historia na maadili ya nchi.
Ameyasema hayo Aprili 7,2025 wakati wa kutangaza orodha teule ya washindi wa Tuto ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu inayotarajiwa kutolewa Aprili 13 mwaka huu.
“Ni wajibu wetu kukuza uandishi ambao unachambua mazingira yetu, uandishi bunifu ni sehemu ya kulinda na kuhifadhi utamaduni wetu ndiyo maana tumechukua hatua za kuhakikisha tunakuza uandishi,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliandika vitabu, mashairi, alitafsiri vitabu vigumu na kwamba tuzo hiyo imepewa jina lake ili kumuenzi na kuwatia moyo waandishi wengine ili waweze kuandika na kutambuliwa.
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo hizo, Profesa Penina Mlama, amesema zilianzishwa mwaka 2022/2023 na Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ambapo wamekuwa wakipokea miswada mbalimbali na kukaa na majaji kuichakata ili kuwapata washindi.
Amesema tuzo za mwaka huu zimejikita katika nyanja nne yaani ushairi, riwaya, hadithi za watoto na tamthiliya.
“Tunafurahi mafanikio yamekuwa mazuri sana, Watanzania wengi wamejitosa katika kuwania tuzo hizi na tumeongeza tahadhari katika mchakato huu kuangalia miswada iliyoletwa kuhakikisha haikiuki vigezo vya kiuandishi na kazi hiyo imefanyika kwa ufanisi mkubwa,” amesema Profesa Penina.
Mkurugenzi Mkuu wa TIE, Aneth Komba, amesema waandishi watakaoshinda kazi zao zitachapwa na kuingia kwenye utaratibu wa kupata ithibati ya kamishna wa elimu kisha kutumika ahuleni kwenye matumizi ya mtaala.
Crédito: Link de origem
Comments are closed.