top-news-1350×250-leaderboard-1

Serikali kujikita zaidi katika utafiti kuboresha sekta ya afya

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Serikali imesema itaendelea kuimarisha mfumo wa utafiti katika sekta ya afya kwa kutenga fedha mahsusi, kutumia matokeo ya tafiti, na kusimamia kwa karibu utekelezaji wake, ili kuhakikisha huduma bora za afya zinaendelea kutolewa kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 4, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Seif Shekilaghe, kwa niaba ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama, wakati akifungua Kongamano la Kisayansi katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa mwaka 2025.

Prof. Shekilaghe amesema kuwa utafiti kuhusu magonjwa ya binadamu ni nguzo muhimu katika maboresho ya huduma za kinga na tiba, na kwamba Serikali itaendelea kuyatumia matokeo ya tafiti hizo katika kupanga na kutekeleza sera bora za afya.

“Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa msaada wa tafiti hizi. Dhamira yetu ni kuimarisha sekta ya afya kwa kutumia utafiti kama nyenzo ya mabadiliko chanya,” amesema Prof. Shekilaghe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Afya na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dk. Rashid Mfaume, alisema Serikali inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia maboresho ya sekta ya afya, ikiwemo kuviwezesha vituo vya afya kuandaa mipango yao wenyewe na kuwa na mifumo thabiti ya upatikanaji wa bidhaa za afya.

“TAMISEMI imeanza rasmi kusimamia utekelezaji wa Sera ya Bima ya Afya kwa Wote. Tunaishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais kwa kuimarisha rasilimali watu ambapo katika kipindi cha miaka minne zaidi ya watumishi 25,000 wameajiriwa. Pia, hospitali mpya 129 zimejengwa, na zaidi ya majengo 14 ya kisasa yameongezwa,” amesema Dk. Mfaume.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Maghembe, alisema haiwezekani kuadhimisha Wiki ya Afya bila kuwa na majadiliano ya kitaaluma yanayolenga kuboresha huduma za afya.

Amesema forum hiyo imewakutanisha wataalamu mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kupata mawasilisho ya kitaalamu, na kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa zaidi katika sekta hiyo.

“Kaulimbiu ya mwaka huu inayosema ‘Tulipotoka, Tulipo na Tuendako katika Sekta ya Afya’ inalenga kutupatia dira ya namna ya kuimarisha sekta hii muhimu kwa ustawi wa taifa. Tumeandaa majadiliano kutoka kwa watafiti wabobezi na wale wanaoelekea kuwa wabobezi,” alisema Dk. Maghembe.

Naye Mkuu wa Shule ya Uuguzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Steven Kigusi, alisema taasisi yao ni mdau muhimu katika kuendeleza wataalamu wa afya nchini, hasa katika nyanja za udaktari na uuguzi.

“Tunaendelea kuboresha elimu ya afya ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania wengi zaidi,” amesema Prof. Kigusi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Edwin Swai, alisisitiza kuwa WHO itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya afya.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.